Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
Baadhi ya nembo mbalimbali maarufu za biashara ulimwenguni. Picha ya Mtandao.
- Utafiti wa kujua mlengwa mkuu wa bidhaa au huduma zako na hali halisi ya soko vitakufanya upunguze vihatarishi lukuki ikiwemo kupunguza kiwango cha hasara.
Ni kawaida kwa sasa kusikia kuwa kampuni fulani au mtu fulani ni nembo bora ya biashara ama ‘brand’ kwa Kiingereza.
Neno hilo siyo jipya sana miongoni mwetu kwa kuwa ujasiriamali unahamasishwa. Masuala ya Brand yamekuwepo miaka zaidi ya 200 iliyopita hasa karne ya 18 baada ya bara la Ulaya kushuhudia mapinduzi makubwa ya viwanda yaliyochagiza uzalishaji mkubwa wa bidhaa.
Tofauti na awali, uzalishaji huo ulileta bidhaa nyingi sokoni na zinazofanana jambo lililowalazimu wafanyabiashara kuweka nembo zao ili wateja waweze kutofautisha kati ya bidhaa moja na nyingine na kupata umiliki sokoni.
Mbali na mapinduzi ya viwanda, historia ya biashara ya watumwa inaeleza kuwa watu walikuwa wakichukuliwa na kupelekwa utumwani Marekani kwenye mashamba ya wakoloni. Ili kuleta urahisi wa utambuzi, ndugu zetu hao walikuwa wakipigwa chapa mwilini na kuthibitisha umiliki wa watumwa.
Vilevile katika historia ya jamii za kifugaji barani Afrika tena hadi sasa kuna utamaduni wa wafugaji walio wengi kuiwekea alama mifugo yao kwenye ngozi. Hatua hiyo hufanywa ili kuondoa mkanganyiko wa kutambua wanyama hao. Mifano yote hii inaonyesha nguvu na namna brand ilivyokuwa na ilivyoanzishwa na misingi yake sokoni.
Katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia vitu vingi vimekuwa vikibadilika na kuwa vya kipekee kabisa. Yote hayo ni maboresho tu ya kile cha zamani kwa kuwa kisingeendana na wakati wa sasa.
Soma zaidi: Mbinu zinazowaweza kuwasaidia wajasiriamali kuchangamkia fursa zilizowazunguka
Kuna mambo ya msingi ambayo mfanyabiashara hutakiwa kuyazingatia anapoamua kuanzisha biashara yake na kukuza brand husika. Miongoni mwa vitu hivyo ni;-
Bainisha wateja unaowakusudia
Hii imekuwa ni changamoto kubwa kwa wafanyabiashara. Baadhi wamekuwa na mitaji na kuanzisha biashara zao bila kupata tafsiri sahihi ya huduma au bidhaa zao. Mara nyingi hawajui mlengwa mkuu wa bidhaa.
Uelewa wa mteja wako mkuu utakusaidia vitu vingi vikiwemo uchaguzi wa lugha sahihi ya kufikisha ujumbe kuhusu huduma au bidhaa. Pili, itakusaidia kuandaa mazingira rafiki kulingana na kundi unalolilenga na mwisho itakusaidia namna ya kuendana na nyakati na mabadiliko yote yanayoendelea kwenye soko hili la kiushandani.
Ukianzisha biashara bila kuzingatia haya kuna uwezekano mkubwa ukakwama mbeleni na sababu kuu ni kushindwa kutambua mlengwa mkuu wa bidhaa au huduma zako ili umpe vitu ambavyo anavitaka kupata faraja.
Uelewa wa mteja wako mkuu utakusaidia vitu vingi vikiwemo uchaguzi wa lugha sahihi ya kufikisha ujumbe kuhusu huduma au bidhaa
Weka ahadi zinazotekelezeka
Wafanyabiashara wamekuwa wakipanga matarajio makubwa kwa wateja ambayo wakati mwingine hayapo kwenye bidhaa au huduma husika. Hii ni mbaya kwa kuwa uanchowaahidi wateja wako lazima wakikute ili kuongeza uaminifu.
Biashara ni kama siasa ukiahidi kitu na ukashindwa kukitekeleza siku ya mwisho wapiga kura watakuuliza ulituambia hili na lile, viko wapi?
Vile vile kwenye biashara mimi nikija kwenye kibanda chako nikiwa na fikra kuwa chakula ni cha moto halafu nikakuta ni cha baridi ni lazima nihoji. Hii inashusha sana mahusiano ya bidhaa na mtumiaji na kuporomosha imani juu ya biashara husika.
Jitose kwenye utafiti wa watumiaji wa bidhaa
Utafiti wa kina juu ya mahitaji na tabia za watumiaji (Consumers behavior survey) ni muhimu kufanywa na mfanyabiashara kabla ya kuanzisha biashara yako katika eneo husika. Katika hatua hii kuna maswali wapaswa kujiuliza yakiwemo tabia za watumiaji wa huduma katika eneo husika. Je, wanapendelea kitu gani. Je, mazingira hayo ni rafiki kwa biashara kwa kuzingatia sera na imani za eneo hilo? Kuna mitazamo gani ya kijamii juu ya biashara mpya na vitu kama hivyo?
Aina hii ya utafiti itakusaidia kufanya maandalizi sahihi katika sehemu sahihi na kufanya uwekezaji sahihi wa kibiashara.
Mambo hayo matatu yana mashiko sana katika mafanikio ya kujenga nembo ya biashara yako. Biashara nyingi zimekufa na moja ya sababu kubwa ni uwekezaji ulifanyika bila utafiti wa kina. Mwisho wa siku kila kitu kinachotokea huwa ni sehemu ya kujifunza wakati awali ulikuwa na muda wa kuchambua kabla ya kuwekeza. Utafiti unasaidia kupunguza vihatarishi vya kibiashara na kuyamaliza madhara yote yanayoweza kujitokeza leo kama bahati mbaya.
Kuna msemo mmoja wa Kiingereza unaosema kuwa ‘a strong brand is built under strong market share investigation’. Ikiwa ni maana kuwa brand imara hujengwa kwenye mazingira yenye taarifa za kina juu ya soko husika.
Charles Nduku maarufu kama Mr Brand ni mkufunzi wa wajasirimali katika masuala ya masoko na uhamasishaji wa kimaisha. Kwa mawasiliano, maoni na ushauri wasiliana naye kupitia +255762918153 au baruapepe mrbrandtz@gmail.com.