Mambo ya kuzingatia kabla ya kusaini mkataba
- Pata muda mzuri wa kuusoma na kuelewa vipengele vyote vya mkataba.
- Tafuta mshauri au mwanasheria kupata ufanunuzi kwa baadhi ya vitu usivyoelewa.
- Hakikisha una nakala ya mkataba ili kuhifadhi kumbukumbu.
Mikataba kwenye maisha ya kila siku ni suala ambalo halikwepeki. Mikataba imekua sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania wa kawaida na yule wa hali ya juu.
Tunakutana na mikataba kwenye upangaji wa nyumba, ununuzi wa vyombo vyo moto, ununuzi wa viwanja na mashamba bila kusahau mikataba ya kibiashara na ajira.
Hivyo basi suala la kufahamu na kuelewa mikataba halikwepeki, litakufuata kwa namna yoyote ile. Ni vyema kujifunza na kufahamu vitu kadhaa vya kuzingatia wakati na kabla ya kusaini mkataba wa aina yoyote ile.
Vifuatavyo ni vigezo vya kuzingatia kabla ya kusaini mkataba wowote:
- Soma vizuri mkataba
Unapaswa kusoma mkataba wako vizuri kabla ya kuamua kuweka saini yako. Kusoma mkataba itakusaidia kuelewa vizuri vipengele vya mkataba huo na kuwa makini navyo na kuweza kutambua changamoto au faida kwa upande wako. Kusoma kwa umakini kunaamanisha kusoma kila kurasa ya mkataba wako na kuelewa vizuri kilichoandikwa.
- Omba nakala ya mkataba
Mkataba wowote unakua na nakala zaidi ya moja kwa ajili ya kuwapa wahusika wa mkataba huo. Ni vyema kuomba kupatiwa nakala ya mkataba ili uweze kusoma kwa utulivu ukiwa peke yako au na mshauri wako. Pia inakupunguzia presha wakati wa kusoma mkataba husika, hii itakusaidia kufanya maamuzi sahihi juu ya mkataba husika bila kuwa na haraka.
Kila mkataba una masharti yake. Kabla ya kusaini soma, elewa ili usipate changamoto mbeleni. Picha|Unasplash.
3. Jadiliana kwa kina
Hakikisha unajadiliana kwa kina na upande wa pili kabla ya kuweka saini kwenye mkataba husika. Majadiliano hayo ni pamoja na kuzingatia yale ambayo unyahitaji kuyaona kwenye mkataba husika ambayo yana maslahi na upande wako kimkataba. Majadiliano yanaweza kufanya baadhi ya vipengele vya mkataba kubadilishwa na kuwekwa vile ambavyo vinaakisi mahitaji yako kwa upande wako.
- Pata ushauri wa kisheria
Ukiona kuna ukakasi kwenye kipengele chochote cha mkataba, usisite kuwasiliana na mwanasheria wako kwa ufafanuzi kabla ya kuamua kusaini mkataba huo. Vipengele vingi vya mkataba vinawekwa na mtu kwa maslahi yake na siyo kwa maslahi ya upande mwingine. Ufafanuzi wa mwanasheria utasaidia kuyaweka mambo mengi katika uwazi zaidi na kukuweka katika sehemu sahihi na salama.
5. Jipe muda
Kufikiria kwa muda kwa yale ambayo yamo kwenye mkataba wako yatakupa nafuu ya kuwa na Amani na uelewa wa kile kilichomo kwenye mkataba na kusaini mkataba ukiwa mwenye utulivu. Papara haina umuhimu wakati wa kusaini mkataba. Kuepusha hayo unapaswa kujipa muda mzuri wa kutafakari kilichomo kwenye mkataba.
- Usiombe ushauri kwa mtu anayekupa mkataba
Popote pale ambapo kuna shida yoyote kwenye kipengele cha mkataba usijaribu kuomba ufafanuzi kwa mtu ambaye amekupa mkataba huo. Kimsingi yeye anakua ameandaa vigezo kwa masharti na manufaa yake. Kumuuliza jambo lolote lile ni kumpa nafasi ya kukushauri kwa vile itakua ina manufaa kwake.
Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule,
Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini
Twiter: @Hamzaalbhanj
Instagram: @Hamzaalbhanj
Mob: 0717521700