Mama aacha kazi kumlea mwanae mwenye usonji

April 4, 2022 9:46 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link

Elly Kitali akicheza na mtoto wake Chadron ambaye ana usonji. Picha| UN News Video.


  • Ni Elly Kitali anayeishi na mtoto mwenye usonji.
  • Awasisitiza wazazi wa kiume kutokimbia wake zao na watoto wenye usonji.
  • Ugonjwa huo huwaathiri zaidi watoto wa kiume.

Dar es Salaam. Wakati wazazi wengine wakikata tamaa au kuwatelekeza watoto wao wenye usonji, Elly Kitali, ambaye ni mama wa watoto wawili ameamua kuweka kando taaluma yake ili kumlea mtoto wake wa kiume mwenye usonji aitwaye Chadron. 

Kitali anasema kuwa tabia ya Chadron kwa ujumla ilikuwa ni ngumu kuielewa kwani ilikuwa ni tofauti na watoto wengine.

“Kwa mara ya kwanza nilitambua Chadron ana usonji, alipokuwa na umri wa miaka mitatu na tulitegemea Chadron atakuwa na uwezo wa kuzungumza maneno machache hata mama au baba, yaani awe na mawasiliano, lakini haikuwa hivyo,” anasema Elly wakati akohojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa.

Usonji ni tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea.

Ugonjwa huo ambao kwa Kiingereza unajulikana kama “Autism” humfanya mtoto kuwa na kasi ndogo ya ukuaji wa akili tofauti na ukuaji wa mwili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa usonji  hukumba mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 duniani.

WHO inaongeza kuwa watoto wa kiume huathirika zaidi kuliko watoto wa kike, ambapo mtoto mmoja kati ya 44 anaishi na hali ya usonji, huku mtoto mmoja wa kiume kati ya watoto wa kiume 127 ana usonji.


Zinazohusiana:


Wazazi hugundua mtoto ana usonji baada ya kuonyesha tabia zisizo za kawaida ikiwemo kutotamka maneno ya kitoto anapotimiza umri wa mwaka mmoja, kupiga piga mikono, kung’ang’ania vitu, kutikisa kichwa mara kwa mara, pamoja na kutumia nguvu sana.

Dalili nyingine ni kuparua wengine, kujiumiza mwenyewe kwa kujing’ata, kujikwaruza na kurusha vitu.

Wataalam wanasema kuwa hali  hiyo hufanya wazazi kuathirika kisaikolojia, huku wengine wakiamua kuwatelekeza watoto hao.

Kutokana na hali hiyo, elimu inaendelea kutolewa katika jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo maadhimisho ya siku ya usonji duniani ambayo hufanyika April 2 kila mwaka, ili kuongeza uelewa kwa wazazi na jamii kuhusu usonji.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa hamasa nyingi hutolewa kwa wazazi wenye watoto wa hali ya usonji, ikiwemo kujiunga katika makundi ya kusaidiana ambayo husaidia wazazi kwa wazazi kupeana uzoefu ambao wamepitia.

Vilevile, wataalam huwapa wazazi msaada wa kisaikolojia, pamoja na familia kuhamasishwa kutoa ushirikiano kwa kumjumuisha, kumjengea ujuzi na ushiriki mtoto mwenye hali ya usonji katika familia.

Elly anasema anapata ushirikiano kutoka kwa mume wake, ndugu na marafiki na anawashauri wazazi hasa wa kiume wasikimbie wake zao na watoto wenye usonji.

“Katika harakati zangu za kusaidia wazazi wenye watoto wenye usonji kama mimi nimekutana na wanawake wengi ambao wamekimbiwa na waume zao, hii tabia si  nzuri na inawasababishia maisha ya shida hasa mtoto mwenye usonji,” anasisitiza Elly. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW