Majaliwa awakumbusha wakuu wa mikoa, makatibu tawala mipaka ya madaraka yao
- Awataka kuzingatia mipaka ya madaraka yao ikiwemo sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kuendeleza nidhamu katika utumishi wa umma na kutoa huduma bora kwa wananchi.
- Awataka viongozi hao wawe mfano bora wa kuigwa, waadilifu, watenda haki, kufuata sheria pamoja na kufahamu na kuheshimu miiko ya uongozi.
- Pia wamepewa jukumu la kusimamia amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuzingatia mipaka ya madaraka yao ikiwemo sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kuendeleza nidhamu katika utumishi wa umma.
Ametoa maagizo hayo leo (Desemba 3, 2018) wakati akifungua mafunzo ya uongozi yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wakasimamie kikamilifu mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa amenukuliwa akisema baada ya mafunzo hayo Serikali inatarajia watasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na wao wenyewe watakuwa kioo katika kuzingatia miiko ya utumishi wa umma.
“Mkadumishe uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi anao mchango katika kuboresha utendaji kwenye kituo chake cha kazi. Nina matarajio makubwa kuwa mtadumisha uhusiano mzuri kikazi na viongozi wa juu na pia uhusiano wa diplomasia ya heshima na viongozi wengine ndani ya mihimili yetu mitatu,” amesema Majaliwa.
Amewataka viongozi hao wahakikishe kila mmoja wao anaandaa mpango kazi unaoainisha shughuli zake za kila siku ili kuongeza weledi katika kuwatumikia wananchi.
Pia viongozi hao wametakiwa wasimamie nidhamu kazini na uwajibikaji wa watumishi kwa wananchi, ambapo pia amewasihi watende haki kwa wananchi na watumishi walio chini yao na wawapokee na kuwahudumia kwa staha, wasikilize kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Zinazohusiana:
- Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho.
- Majali atoa maagizo mazito ubora vya vyoo, utunzaji wa mazingira
Amebainisha kuwa wanatakiwa kusimamia amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote kwani amani na utulivu ndiyo itawezesha nchi kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
“Tunakumbushwa sisi viongozi tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila kubagua jinsia, kabila, dini, rangi ya ngozi, mtu atokako ndani ya nchi ilimradi hajavunja sheria; wala ubaguzi mwingine wa aina yoyote. Tunaaswa tuwahudumie watanzania wote kwa usawa,” amesema Majaliwa.
Kuhusu mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo, Majaliwa amesema zitawawezesha viongozi hao kupata fursa ya kutafakari na kujitathmini kuhusu hatua za kujiimarisha zaidi kiuongozi na kiutendaji ikiwemo kubadilika kwa mtazamo na kujirekebisha endapo watabaini maeneo waliyokuwa wakikosea tangu walipokabidhiwa ofisi hadi sasa.
Mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinahusu majukumu na mipaka ya kazi, ambapo watajifunza namna ya kufanya kazi bila mikwaruzano isiyo na tija baina yao na viongozi wa mihimili mingine ya dola, viongozi wa kisiasa na watendaji wengine Serikalini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa Jijini Dodoma leo. Picha|Michuzi.
Mada nyingine inahusu hisia na mahusiano mahali pa kazi, ambapo itawawezesha kujiimarisha katika mbinu za kuwaongoza watumishi walio chini yao kwa kujenga na kudumisha mshikamano na ushirikiano wa pamoja.
“Mada itafafanua pia namna mnavyotegemeana na watumishi wa kada na ngazi mbalimbali katika kutimiza majukumu yenu. Ni muhimu sana kufanya kazi kama timu moja ili muweze kuyafikia malengo ya taasisi kwa upana wake na si malengo ya mtu au kiongozi mmoja,” amesema Majaliwa.
Katika mada inayohusu muundo wa Serikali na namna inavyofanya kazi watauelewa vizuri zaidi muundo wa Serikali ulivyo na jinsi unavyofanya kazi. Pia wataielewa vizuri zaidi itifaki na kuheshimiana kwa ngazi mbalimbali kutoka Waziri, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara hadi wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Prof. Joseph Semboja amesema mafunzo hayo ya wiki moja yatajikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kufanya maamuzi ya kimkakati yanayozingatia mahitaji na manufaa mapana ya sasa na ya baadae kwa jamii.
Ametaja eneo la pili kuwa ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kuongoza rasilimali watu na kusimamia rasilimali nyingine ili kutekeleza kikamilifu na kwa mafanikio maamuzi ya kimkakati waliyoyafanya katika kipengele cha kwanza.
“Eneo la tatu ni la kuimarisha uwezo wa washiriki katika kujijengea sifa binafsi za uongozi ili awe na ushawishi kwa wananchi anaowaongoza. Hili ni jambo la msingi, kiongozi mwenyewe awe mfano bora wa kuigwa. Awe muadilifu, mtenda haki, mfuata sheria na taratibu pamoja na kufahamu na kuheshimu miiko ya uongozi.”
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika; Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Josephat Kandege pamoja na maafisa wengine wa Serikali.