Majaliwa awakalisha kiti moto TADB, wakuu wa mikoa malipo ya wakulima wa korosho

January 16, 2019 9:19 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema TADB ihakikishe inabadilisha mfumo wake ili kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho ambao wameshahakikiwa.
  • Mpaka sasa malipo yamefanyika kwa tani 92,000 ikiwa ni chini ya nusu ya korosho yote iliyopo ghalani inayofikia tani 206,000.
  • TADB Imesema fedha iliyolipwa kwa wakulima wa korosho hadi sasa ni Sh306 bilioni kwa wakulima zaidi ya 156,000.

Dar es Salaam. Waziri MKuu, Majaliwa ameitaka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) ihakikishe inabadilisha mfumo wake ili iweze kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho ambao wameshahakikiwa.

Amesema Serikali bado inapokea malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu suala la malipo ya korosho kwani kwa kawaida malipo ya mkupuo yote huwa yamekamilishwa ifikapo Januari 10 ya kila mwaka.

Ametoa agizo hilo leo (Januari16, 2019) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Japhet Justine katika kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, Dodoma.

Wakuu wa mikoa hiyo mitatu walikuwa kwenye mikoa yao na Mkurugenzi Mkuu wa TADB, alikuwa Dar es Salaam.

“Hakikisha mnaharakisha malipo ya wakulima lakini pia suala la uhakiki linabaki palepale ili tuwalipe wakulima wanaostahili,” amemweleza Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Justine na kuongeza kuwa,

“Hili zoezi la uhakiki na malipo, lilianza Novemba 27, 2018 na leo ni tarehe 16 Januari, 2019 na hatujafika hata asilimia 50, maana yake zoezi hili tutalimaliza Aprili mwanzoni. Haiwezekani! Tunapata lawama kutoka kwa wakulima wa korosho kwa sababu hii kasi ni ndogo; na haya siyo malengo ya Mheshimiwa Rais, aliyetaka korosho zinunuliwe na Serikali.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  wakuu wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma  katika kakao alichokiitisha kwa njia ya video akiwa ofisini kwake jijini Dodoma, Januari 16, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amehoji kwa nini benki hiyo haishirikiani na vyama vikuu (unions) au vyama vya msingi (AMCOS) ili kubaini idadi halisi ya wakulima na idadi kamili ya kiasi walichovuna kwa sababu kila AMCOS ina wanachama wake wanaojulikana.

“Zao la korosho lina mfumo wa ushirika. AMCOS ziko kwenye ngazi ya vijiji na unaweza kukuta AMCOS moja ina wanachama zaidi ya 200, sasa bila kupitia kwenye hizi AMCOS unawezaje kujua kila mkulima amevuna kilo ngapi na anadai kiasi gani kwa kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko pekee?,” amehoji Majaliwa.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, mpaka sasa malipo yamefanyika kwa tani 92,000 ikiwa ni chini ya nusu ya korosho yote iliyopo ghalani inayofikia tani 206,000.  

 Ameitaka benki hiyo izishirikishe AMCOS na UNIONS pindi malipo yanapofanyika ili kubaini changamoto zilizopo ili kuharakisha malipo hayo.

“Mfumo unaotumika sasa unapeleka malipo moja kwa moja kwenye akaunti ya mtu binafsi, kwa hiyo AMCOS wanakuwa hawana taarifa, na wao pia wanachangia kushiriki kutoa malalamiko,” amesema.

Katika kuhakikisha malipo ya wakukima yanawafikia mapema, amesema nimeongea na wakurugenzi wa CRDB na NMB na kuwasisitiza kuwa suala la miamala ya malipo ya korosho lifanywe mchana na usiku ili malipo yakamilike kabla ya Januari mwishoni.


Zinazohusiana:


Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Jusine amesema fedha iliyolipwa kwa wakulima wa korosho hadi sasa ni Sh306 bilioni kwa wakulima zaidi ya 156,000.

 “Korosho zilizolipwa hadi sasa ni tani 920,700 ambazo ni wastani wa asilimia 44,” amesema na kubainisha kuwa zaidi Sh11 bilioni zimekwama kulipwa kwa sababu taarifa za kibenki zinaonyesha kuna matatizo hasa kwenye majina ya wakulima.

 “Majina ya waliopeleka mzigo, yanatofautiana na majina ya akaunti za benki. Majina yaliyokataliwa na mfumo wa kibenki yatabandikwa kwenye vyama vya msingi ili wakulima wakarekebishe taarifa zao,” amesema.

Hata hivyo, amesema takriban Sh15 bilioni zimelipwa kwa watoa huduma ambao ni wasafirishaji, wapagazi na wenye maghala.

 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW