Magufuli: Ucheleweshaji wa ujenzi bomba la mafuta unaumiza
- Amesema ucheleweshaji wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga unaumiza ikizingatiwa Tanzania imejitoa kwa kiwango kikubwa kufanikisha mradi huo.
- Amesema kama mradi huo utazidi kuchelewa utapunguza fursa za ajira katika nchi hizo mbili.
- Rais Museveni amesema atahakikisha mradi huo unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Dar es Salaam.Rais John Magufuli amesema ucheleweshaji wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga unaumiza ikizingatiwa Tanzania imejitoa kwa kiwango kikubwa kufanikisha mradi huo ikiwemo kupunguza kodi zilizokuwepo kisheria.
Katika hotuba yake leo, wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda, Dk Magufuli ameonekana kukerwa na ucheleweshaji huo akimweleza Rais Yoweri Museveni akubali kutoa “sadaka” kwa baadhi ya mambo kwa faida ya baadaye.
“Naomba niwape siri leo nilikuwa namuuliza Mzee Museveni mbona unachelewesha hili bomba? Kwa sababu ya huko ambako umekataa Dola za Marekani 600 wakati utakuwa unatengeneza Dola za Marekani 80 bilioni. Sacrifice (itoe sadaka) hiki kidogo ucreate (utengeneze) ajira na utapata fedha nyingi in a long term (kwa muda mrefu),” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliyeonekana kukerwa na jambo hilo amesema wadau wote wanapaswa kusonga mbele katika biashara kwa kuwa katika biashara huwezi kupata faida ya hali ya juu bila kujitoa na kugawana kidogo.
“Unapaswa kupoteza kidogo ili upate kingi,” Rais Magufuli ameeleza katika hotuba yake na kuongeza kuwa “nimeona nizungumze hili kwa sababu linauma.”
Soma zaidi: Tanzania, Uganda sasa kukamilisha mikataba ya bomba la mafuta mapema 2019.
Rais Magufuli, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kusukuma mradi huo mkubwa wa mafuta Afrika Mashariki, amesema ilibidi kupeleka mabadiliko ya sheria bungeni ili kuweza kuendana na mahitaji ya kikodi na kufanikisha ujenzi wa bomba hilo.
Amesema tayari mradi wa bomba hilo umeshaanza kuajiri watu wakiwemo wanaofanya upembuzi yakinifu na kuchelewesha zaidi kunazidi kupunguza fursa za ajira katika nchi hizo mbili ikizingatiwa kuwa idadi ya watakaopata ajira ni zaidi ya 20,000.
“Kwa hiyo bomba hili halitakiwi kuchelewa. Haijalishi sababu za kuchelewesha mradi huo zinahusisha wawekezaji lakini lazima tuhakikishe masuala yote yanayokwamisha yametafutiwa uvumbuzi ili tuanze mradi mapema iwezekanavyo,” amesema Dk Magufuli.
Katika hotuba yake leo, wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda, Dk Magufuli ameonekana kukerwa na ucheleweshaji huo akimweleza Rais Yoweri Museveni akubali kutoa “sadaka” kwa baadhi ya mambo kwa faida ya baadaye.Picha|Mtandao.
Katika hotuba hiyo ambayo ilijumuisha pia maneno ya vichekesho, Dk Magufuli amesema anatamani watumishi wa Tanzania wangehamia Uganda na wale Uganda wahamie nchini angalau kwa mwezi mmoja ili awashughulikie.
Rais Yoweri Museveni amesema mafuta yapo tangu miaka milioni mbili na atahakikisha yanazalishwa.
“Hili jambo la mafuta lipo…na lipo chini ya Serikali ya Uganda na tumeshakubaliana na Serikali ya Tanzania kuhusu bomba la mafuta. Tumefurahishwa na tunashukuru kwa Rais Magufuli kwa kutoa kanuni na msamaha kwa kitozo na kikodi kwa kampuni za mafuta na kampuni ya bomba ili kuhakikisha mradi una manufaa.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Uganda haitochelewesha mradi huo,” amesema Rais Museveni.
Latest
