Magufuli atoa maagizo mazito ujenzi kituo cha mabasi Dar
- Amtaka mkandarasi kukamilisha kituo hicho kipya cha Mbezi Luis Novemba, 2020.
- Ahoji matumizi ya fedha za mradi huo ikiwemo kuongezeka kwa bajeti kutoka Sh51 bilioni hadi Sh71 bilioni.
- Kituo hicho kikamilika kitaongeza fursa za ajira na mapato ya Jiji la Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameitaka kampuni ya Hainan International Limited inayojenga kituo kipya cha mabasi ya mikoani cha Mbezi Luis Jijini Dar es Salaam kukamilisha ujenzi huo Novemba mwaka huu, huku akihoji kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa kituo hicho kitakachokuwa na uwezo kuchukua magari 3,456.
Mradi huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 85 ulitarajiwa kukamilika Julai 2020, lakini imeshindikana kutokana na mkandarasi huyo kudai kuwa janga la Corona (COVID-19) lilikwamisha baadhi ya shughuli za ujenzi.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Oktoba 8, 2020) wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kituo hicho, amesema anataka kuona kituo hicho kinakamilika haraka kwa sababu Corona siyo sababu ya msingi kumzuia mkandarasi kutimiza wajibu wake.
Dk Magufuli aliyeambatana na Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera amesema anatoa muda hadi mwezi Novemba 2020 kwa mkandarasi kukamilisha na kukabidhi mradi huo.
“Nataka mradi huu kabla ya mwezi wa 11 uwe umemalizika. Hakuna extension (kuongezewa muda). Wafanye kazi usiku na mchana. Umeme upo, maji yapo, watu wa kufanya kazi wapo, pesa zipo, hakuna sababu ya kusingizia Corona mbona hawajavaa hata barakoa hapa?,” amesema Dk Magufuli.
Agizo hilo la Rais linakuja baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Sulemani Jafo kusema kuwa kituo hicho kinarajiwa kukamilika ifikapo Januari, 2021.
Amesema ikiwa mkandarasi huyo atashindwa kukabidhi kituo Novemba, Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano ianze kumkata mkandarasi huyo fedha ya ucheleweshaji mradi.
“Mkataba ulitakiwa umalizike mwezi wa saba leo ni mwezi wa 10 na Waziri (Selemani Jafo) alikuwa anazungumza hapa wanatakiwa kukabidhi mwezi wa kwanza. Hii siyo haki,” amesisitiza Rais.
Stendi hiyo inatarajiwa kutoa ajira takriban 10,000 na kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kukusanya mapato ya Sh10.2 kwa mwaka. Picha| Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam
Ahoji kuongezeka kwa gharama za ujenzi
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amehoji sababu za kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa kituo hicho hadi kufikia Sh71 bilioni kutoka Sh51 bilioni zilizopitishwa awali.
“Huu mradi nitaufuatilia vizuri mimi halafu mtaona kama hamtatapika kama kuna hela zozote mlizoziweka. Sh71 bilioni ni nyingi. Tukaidhinisha Sh51 bilioni leo ninaambiwa Sh71 bilioni. Inawezekana hiyo kazi iliyoongezwa ni muhimu.
“Nimeambiwa na Waziri kuna daraja. Sasa daraja la kugharimu Sh21 bilioni? nitaliangalia na lenyewe nilione hilo daraja,” amesema Magufuli aliyehimiza Wakandarasi kuthamini muda na fedha za mradi huo.
Soma zaidi
- Mnada wa korosho kuanza Oktoba 9
- Tanzania, Malawi zafungua ukurasa mpya ushirikiano kibiashara
- Mambo yatakayokusaidia kutunza chakula nyumbani
Uwezo na faida za kituo hicho
Rais wa Malawi, Dk Chakwera ambaye amezindua ujenzi wa kituo hicho amesema kitakuwa kiungo muhimu cha biashara na mawasiliano baina ya nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Mradi huu wa stendi ya kimataifa ni kiashiria kuwa watu wetu wanaweza kushirikiana lakini pia kusafiri kwa uhuru siyo tu kwa nchi zetu mbili lakini pia kwa jumuiya nzima ya SADC,” amesema Rais huyo.
Kituo hicho kitakapokamilika kitasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika kituo cha Ubungo na kusababisha kero kwa watumiaji wa kituo hicho.
Waziri Jafo wakati akitoa taarifa ya kituo cha Mbezi Luis amesema kitakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi 3,456 huku kikiwa na eneo linalotosha kuegesha magari 1,000 kwa siku na kuhudumia nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, Congo DRC, Rwanda na Burundi.
Pia kinatarajiwa kutoa ajira takriban 10,000 na kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kukusanya mapato ya Sh10.2 kwa mwaka.
Mpaka sasa, wakati ujenzi wa mradi huo ukiendelea, watu 600 wakiwemo mafundi na mafundi wasaidizi wamepata ajira huku ukinufaisha viwanda vya Tanzania baada ya kutumia malighafi za ujenzi zinazozalishwa nchini.
Latest
