Magufuli ateua Katibu mpya Wizara ya Kilimo
- Amemteua Gerald Kusaya aliyekuwa Mwenyekiti wa timu iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge mkoa wa Tanga.
- Anachukua nafasi ya Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemteua Gerald Kusaya kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo akichukua nafasi ya Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Taarifa iliyotolewa leo (Machi 5, 2020) na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu inaeleza kuwa kabla ya uteuzi huo, Kusaya alikuwa Mwenyekiti wa Timu iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge mkoa wa Tanga.
“Uteuzi wa Kusaya unaanza mara moja leo tarehe 5 Machi 2020,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
U T E U Z I. pic.twitter.com/LMucPFOl3h
— Gerson Msigwa (@MsigwaGerson) March 5, 2020
Timu hiyo iliyokuwa na wajumbe 13 ilihusisha maafisa kutoka ofisi mbalimbali za Serikali iliwasilisha ripoti yake Machi 1, 2020 kwa Waziri Mkuu kuhusu uchunguzi iliofanya kwenye tasnia ya mkonge kati ya Novemba 29, 2019 na Februari 7, 2020.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, uchunguzi huo maalum ulihusu masuala mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mkonge, bei ya zao la mkonge katika soko la ndani na nje ya nchi.
Pia, ilichunguza kuhusu mali za iliyokuwa Mamlaka ya Mkonge Tanzania, ubia kati ya kampuni ya Katani Limited na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), utendaji kazi wa kampuni ya Katani Ltd na pia utendaji kazi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).
Mwenyekiti wa timu hiyo, Kusaya alisema timu yake ilibaini kuwa kampuni ya Katani Ltd tangu mwanzo ilikuwa na mgongano wa kimaslahi na kupelekea kuhujumu uchumi.
Timu hiyo ilipendekeza kuwa Serikali itoe fedha kwa ajili ya kazi ya kuyapima upya mashamba matano ya Mwelya, Ngombezi, Hale, Magunga na Magoma ili wananchi wanaoendelea kutumia mashamba hayo kwa kukodishwa na Bodi ya Mkonge kama ilivyokubalika kwenye Baraza la Mawaziri mwaka 2005 ili waweze kupewa hati ndogo (leasehold tittle).
Pia, ilipendekeza nyumba 30 zilizopo eneo la Muheza, ambazo baadhi zilitolewa kwa wananchi waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Mkonge na baadhi kuachwa kwa ajili ya makazi ziendelee kuwa mali ya wananchi hao kwa kuwa eneo hilo kwa sasa lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
“Nyumba 22 zilizoko ndani ya mashamba ya mkonge na maeneo ya kiwanda cha TANCORD ziendelee kubaki mali ya Serikali na nyumba iliyoko katika kiwanja namba 176 eneo la Bombo iliyohamishwa kwenda kwa Ndg. Salum Shamte irejeshwe Serikalini kwa njia ya urekebishaji wa daftari la Msajili wa Hati,” alisema Kusaya wakati akiwasilisha ripoti yake.
Latest