Maeneo ya umma yapimwe kuepusha migogoro ya ardhi
- Hiyo pia itasaidia maeneo hayo kutambulika kisheria.
Dar es Salaam. Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Misungwi, imeagiza ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha inapima maeneo ya taasisi za umma ili kuondoa migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza.
Akizungumza wakati alipofanya ziara ya kukagua na kutembelea miradi ya maendeleo kwenye wilaya hiyo, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Michael Smart amemwagiza Mkurugenzi kuhakikisha anafanyia kazi suala hilo ili maeneo ya umma yaweze kutambulika.
Kauli ya Mwenyekiti hiyo imekuja baada ya taasisi za elimu ya sekondari Jitihada, Misungwi na Kituo cha afya Koromije kueleza maeneo hayo kutotambulika mipaka halisi ya taasisi hizo hali inayosababisha wananchi kuyavamia.
Mkuu wa shule ya sekondari Jitihada, Rachel Matinde amesema miongoni mwa changamoto zinazoikumba shule hiyo ni pamoja na eneo la shule hiyo kutopimwa.
Changamoto hiyo pia ilielezwa na Mkuu wa shule ya sekondari Misungwi, Thomas Makoye ambaye alisema eneo hilo halijapimwa na halina uzio wa shule hali inayochangia wanafunzi wanaoishi bweni kukaa kwa wasiwasi.
” Tunaomba maeneo yetu yapimwe na tupatiwe hati ili tuyatambue kwakuwa kuna baadhi ya watu wanayavamia na kudai mipaka yao ndiko inakoishia,” amesema Rachel
Akizungumzia suala hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Kashinje Machibya amesema watalifanyia kazi suala hilo ili maeneo yote ya taasisi yapimwe.
Machibya amekiri kuwa maeneo mengi ya taasisi za umma hayajapimwa na mkakati ni kuhakikisha yaanza kupimwa na kupatiwa hati za umiliki.
” Kwa kuanza tunaanza kushirikisha kamati ya mipango miji ili ianze mchakato wa kupima maeneo yote ya taasisi za umma, vitendea kazi vya upimaji vipo ni suala tu la kuweka mipango vizuri,” amesema Machibya.
Latest
