Maagizo ya Majaliwa kupunguza migogoro ya wakulima, wafugaji
- Ni Serikali kutafuta suluhu ya utumiaji wa ardhi.
- Wizara zinazohusika zatakiwa kukaa pamoja
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushiriki kikamilifu katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ili kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Ametoa wito huo leo Septemba 7, 2021 baada ya kufungua mkutano wa wadau wa sekta ya mifugo wa siku mbili unayofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es Salaam.
“Hakikisheni wafugaji wanaelimishwa na kuhamasishwa kufuga kulingana na maeneo waliyonayo. Halmashauri nazo zihamasishe ufugaji ambao hautochochea migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema kuwa sekta ya mifugo ni moja ya sekta muhimu na ya kipaumbele kwa Serikali na lengo la kuiwezesha sekta hiyo kuchangia ipasavyo katika kuwakwamua wananchi kiuchumi na kutoa malighafi katika viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.
Pia ameziagiza mamlaka za Serikali za mitaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kutenga, kupima, kusimamia na kuendeleza maeneo ya malisho pamoja na kuwahamasisha wafugaji waboreshe mifugo yao ili kuongeza tija katika uzalishaji.
“Viongozi na Watendaji wa Serikali hakikisheni mnashirikiana kwa karibu na sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kuwawezesha kuwekeza na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho, malambo, maeneo ya malisho na visima vya maji,” amesema Majaliwa.
Aidha, amesema kuwa uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo uimarishwe ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo sambamba na kuhamasisha wafugaji kutumia mifugo bora iliyofanyiwa tafiti za kuonyesha kuwa na tija zaidi.
Waziri Mkuu pia ametoa wito kwa jamii ya wafugaji kuacha tabia ya kuwapa watoto kazi ya kuchunga mifugo badala yake wajikite katika kuhakikisha watoto hao wanapata elimu bora kwa manufaa yao ya baadaye.
Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema lengo la mkutano huo ni kutoa nafasi kwa wadau wa sekta binafsi kufahamu kwa undani fursa zilizopo katika sekta ya mifugo, kupata uzoefu wa pamoja na kufahamu changamoto na kujadili namna ya kuziondoa.
Habari hii imeandikwa na Medlini Kuya na Nuru Abdallah.
Latest