Lucy Protas: Msichana aliyepania kuinua michezo shuleni

September 27, 2018 10:08 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Anatumia jukwaa la michezo kuwakutanisha wanafunzi kushirikiana na wenzao katika shughuli mbalimbali za kijamii.
  • Tafiti zinaonyesha watoto hawapati muda wa kucheza kwasababu ya ukosefu wa vifaa na viwanja vya michezo shuleni.

Dar es Salaam. Lightness George (9) mwanafunzi wa shule ya msingi Moga ya jijini Dar es Salaam ana ndoto ya kuwa daktari wa binadamu.

Katika kutimiza ndoto yake hulazimika kujiwekea nidhamu ya kusoma kwa bidii. Ratiba yake ya siku nzima huanza alfajiri ya saa 11:00 ambapo hutoka kitandani ili ajiandae kwenda shule ikiwemo kuoga na kupata kifungua kinywa na kuwahi basi la shule ambalo hupita karibu na nyumba yao iliyoko Bunju.

Akifika shuleni siku yake yote huitumia katika masomo ya darasani. Vipindi huisha saa 10 jioni hapo ndipo hurudi nyumbani akiwa mchovu na huishia kufanya kazi za nyumbani na kuangalia katuni na michezo ya runinga ikiwa ni sehemu ya kuburudika na kutafuta msawazo wa fikra.

Lakini Lightness anakosa haki ya msingi ya kucheza ambayo ina mchango mkubwa wa kumsaidia kutimiza ndoto yake. 

Kwa mujibu wa Sheria ya mtoto ya Mwaka 2009, mzazi, mlezi, ndugu au mtu au taasisi yeyote inayomlea mtoto ina wajibu wa kumtunza mtoto kwa kumpatia haki na mahitaji mbalimbali ikiwemo nafasi ya kucheza na kupumzika.


Zinahusiana:

 Njia rahisi kwa wazazi, wanafunzi kujua matokeo ya shule za sekondari. Soma Elimu Yangu


Mtaalam wa Saikolojia, Christian Bwaya anabainisha kuwa michezo ni shughuli zisizo rasmi anazozifanya mtoto kwa lengo la kufurahi na kuburudika. 

Mfano wa shughuli hizi ni kubembea, kuteleza, kuogelea, kuendesha baiskeli, kucheza mdako, ‘rede’, mpira, kukimbia, kuruka na kuvuta kamba, nyimbo, maigizo na kadhalika.

Lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia na wingi wa shughuli za masomo, watoto wengi nchini akiwemo LIghtness wanakoseshwa haki ya kucheza jambo linalowaweka katika hatari ya kupata magonjwa na kuathiri utendaji wa akili na uwezo wa kufikiri. 

Hali hiyo ndiyo imemuibua Lucy Protas (26) kufufua tena ari na muamko wa wanafunzi waliopo shuleni kupenda michezo na kuwahimiza wazazi kuwapa muda watoto kushirikiana na wenzao katika shughuli mbalimbali za kijamii.

“Muda wa wanafunzi kucheza na kujishughulisha na shughuli za nje ya madarasa ulipungua na walishauliwa kukaa madarasani,” anasema Lucy.

Mwanzilishi wa Sport for Change, Lucy Protas (katikati) akiwa na baadhi ya wanafunzi wa kike katika hatua za kuhimiza michezo mashuleni. Picha| Tai Tanzania.

Akiwa mwalimu wa somo la michezo katika shule mojawapo mkoani Arusha, Lucy alikuwa akifundisha kwa nadharia ya michezo darasani lakini wanafunzi walikuwa hawapati muda wa kuyatendea kazi waliyofundishwa.    

Jambo hilo lilimfanya kuona haja ya kupambana ili kuhimiza wanafunzi wapate muda kwa ajili ya michezo, kupanua ufahamu wa wanafunzi na kuwaongezea uwezo wa kuwasiliana, kushirikiana na kuimarisha miili yao.

“Ilinisumbua sana hasa nilipowaza kuwa mwanafunzi huamka saa kumi na moja, apitiwe na gari ya shule afike shule saa moja na nusu na aanze kusoma hadi saa kumi atakaporudi nyumbani,” anasema Lucy

Kero hiyo iliyokuwa inaumiza moyo wake, ilimuongezea kiu ya kuanzisha jukwaa la michezo la ‘Sports for Change’ ili kuhamasisha michezo kwa vijana waliopo shuleni.

Kupitia jukwaa ‘Sport for Change’ wanafunzi wenye umri wa miaka 5 hadi 18 hujumuika pamoja kucheza na kujifunza elimu ya uzazi, “Niliacha kazi yangu na kuanzisha jukwaa hili kwaajili ya kuwapa watoto nafasi ya kucheza na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali.”

Lucy anaamini michezo hufungua milango ya fursa mbalimbali za kibunifu na kuendeleza vipaji vya wanafunzi kwasababu katika michezo wanajifunza mambo mengi kwa lugha rahisi inayoeleweka. 

Mpaka sasa timu ya Sports for change  imefanikiwa kuzifikia shule mbalimbali ikiwemo shule ya sekondari ya Bethsadia iliyopo jijini Dar es salaam ambapo wanafunzi wa rika tofauti hujumuika na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uzazi wa mpango na mabadiliko wanayokutana nayo wakati wanaingia ukubwani.

 
              

Hata hivyo, ndoto ya Lucy kufufua matumaini ya michezo shuleni inaweza kuchelewa kutimia ikizingatiwa kwamba  katika mtaala wa Elimu ya Msingi, kuna somo linalohusiana na michezo linaloitwa ‘Haiba na Michezo’ na shule nyingi zinadai kufundisha somo hilo lakini shule nyingi hazina viwanja vya michezo vinavyofaa na vifaa vya michezo. 

Kwa mujibu wa Utafiti wa Ufuatiliaji wa Uwazi wa taasisi ya Twaweza uliotolewa mwaka 2011, Shule moja katika kila shule nne zilizotafitiwa imeripoti kuwa haina kiwanja cha michezo. 

Pamoja na hilo, shule nyingi kati ya zile zenye viwanja vya michezo zimeonesha kuwa viwanja hivyo haviko katika hali inayokidhi mahitaji ya michezo kutokana na kukosa vifaa muhimu.

Daniel Susuma, mkazi wa Jijini Dar es salaam  anasema ni wakati kwa Serikali na jamii kuinua mwamko wa michezo mashuleni na kuacha kuwazuia watoto wanapopigania haki yao ili wafaidike na fursa zilizopo kwenye michezo.  

“Watu wengi tu ni mifano ya kuwa vipaji vyao vimewafikisha pale elimu isingeweza kuwafikisha. Wakina Samatta na wengineo, ni michezo ndio imewaweka hapo walipo,” anasema Susuma.

Enable Notifications OK No thanks