Kwanini mjamzito haruhusiwi kutoa damu

November 18, 2026 3:27 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na mwili wa mwanamke kuhitaji damu zaidi na madini ya chuma.

Dar es Salaam. Mimba ni kipindi ambacho mwili wa mwanamke hupitia mabadiliko makubwa ya kibaiolojia ambayo mwisho wa siku huleta maisha mapya duniani.

Miongoni mwa mabadiliko yanayotokea ndani ya kipindi hicho ambacho hudumu kwa miezi tisa ni kupungua ama kuongezeka kwa damu ambayo ina jukumu la kusafirisha oksijeni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Katika kipindi hicho baadhi ya watu hujiuliza ikiwa ni salama kwa mama mjamzito kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Emmanuel Masali kutoka Hospitali ya Kitonka jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa kuchangia damu wakati wa ujauzito kunaweza kuhatarisha afya ya mama na mtoto.

Pamoja na maoni ya daktari huyo baadhi ya miongozo ya afya ya kimataifa ikiwemo ya Shirika la Afya Duniani (WHO)  inazuia wajawazito, wanawake wanaonyonyesha kuchangia damu.

Zifuatazo ni sababu tano za kwanini mjamzito haruhusiwi kutoa damu kwa mujibu wa wataalamu wa afya nchini Tanzania na miongozo ya kimataifa.

Kuongezeka kwa mahitaji ya damu na madini ya chuma mwilini

Moja ya sababu kuu zinazofanya mama mjamzito asiruhusiwe kuchangia damu wakati wa ujauzito, ni mwili wa mama kuongeza kiasi cha damu ili kukidhi mahitaji yake na ya mtoto anayekua tumboni.

Pia, madini ya chuma yanahitajika kwa ajili ya kutengeneza hemoglobini, protini inayosaidia kusafirisha oksijeni kwenye damu.

Taasisi ya Taifa ya Afya ya Marekani (NIH) inaeleza kuwa mahitaji ya madini ya chuma huongezeka wakati wa ujauzito kutokana na mahitaji ya mama, mtoto na kondo la nyuma.

Mama mjamzito hapaswi kuchangia damu wakati wa ujauzito, kwani mwili wake unahitaji damu ya kutosha kumhudumia yeye na mtoto aliye tumboni.Picha| Ai| Fatuma Hussein.

Iwapo mama atachangia damu katika kipindi hiki, anaweza kupunguza zaidi akiba ya madini ya chuma na kuongeza uwezekano wa kupata upungufu wa damu, hasa kama tayari alikuwa na kiwango kidogo cha madini hayo.

“Mama akishakuwa mjamzito huwa ‘tume categorize’ katika ‘session’ tatu… Kuna mabadiliko yake katika damu na upungufu wa damu kwa sababu mtoto kama mtoto anatumia madini chuma ya mama, na mama pia anatakiwa azalishe madini chuma katika ‘component’ ya damu.” anaeleza Dk Masali.

Kuongeza hatari ya upungufu wa damu kwa mama

Upungufu wa damu ni mojawapo ya changamoto zinazoweza kuwapata wanawake wakati wa ujauzito. Hali hii hutokea pale ambapo kiwango cha hemoglobini kinakuwa chini ya kiwango kinachotarajiwa kwa kuzingatia hatua ya ujauzito na vigezo vya kitabibu.

Miongoni mwa sababu zinazochangia tatizo hilo ni mahitaji makubwa ya madini ya chuma, upungufu wa virutubisho, magonjwa ya maambukizi na sababu nyingine za kiafya.

Wakati mtu anapochangia damu, kiasi fulani cha chembe nyekundu za damu huondolewa mwilini na huchukua muda kurejesha chembe hizo.

Wakati wa ujauzito, mwili wa mama huhitaji damu zaidi pamoja na madini ya chuma ili kuzalisha chembechembe nyekundu za damu zinazosaidia kusafirisha oksijeni kwa mama na mtoto anayekua tumboni. Picha| Ai| Fatuma Hussein.

Upungufu mkubwa wa damu wakati wa ujauzito unaweza kumfanya mama apate uchovu uliokithiri, kizunguzungu, mapigo ya moyo kwenda kasi na kupungua kwa uwezo wa mwili kusafirisha oksijeni jambo ambalo ni hatari kwa mama mjamzito.

Dk Masali anasisitiza kuwa mama mjamzito anahitaji kulindwa dhidi ya changamoto zinazoweza kuongeza mahitaji ya mfumo wake wa damu.

Kulinda upatikanaji wa oksijeni, virutubisho kwa mtoto aliye tumboni

Mtoto aliye tumboni hutegemea mfumo wa damu wa mama kupata oksijeni na virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji wake. Uhamishaji huo hufanyika kupitia kondo la nyuma, ambalo ni kiungo muhimu kinachounganisha mahitaji ya mtoto na mwili wa mama.

Damu husafirisha oksijeni na virutubisho muhimu, huku kondo la nyuma likiwa na jukumu la kuratibu ubadilishanaji wa mahitaji hayo kati ya mama na mtoto.

Mahitaji makubwa ya damu na madini ya chuma wakati wa ujauzito yanaweza kuongeza hatari ya mama kupata upungufu wa damu, hali inayoweza kuathiri afya yake na maendeleo ya mtoto aliye tumboni. Picha|Ai |Fatuma Hussein.

Iwapo mama atakuwa na upungufu wa damu, uwezo wa damu kusafirisha oksijeni unaweza kupungua, jambo linaloweza kusababisha hatari ya mtoto kuzaliwa kabla ya wakati, kuwa na uzito mdogo wakati wa kuzaliwa na matatizo mengine ya ukuaji.

Akifafanua umuhimu wa damu katika ukuaji wa mtoto, Dk Masali anasema “Tunategemea’ flow’ ya damu kutoka kwa mama kupitia kondo imfikie mtoto. Damu ndiyo imebeba ‘nutrients’ (virutubishi) zote. Damu ndiyo imebeba hadi ‘oxygen supply’ kwenda kwa mtoto.”

Uhitaji wa akiba ya damu kwa ajili ya ujauzito na kujifungua

Ujauzito na kujifungua ni michakato inayohitaji maandalizi makubwa ya mwili wa mama. Katika kipindi hiki, mwili unahitaji kuwa na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kawaida ya ujauzito pamoja na uwezekano wa kupoteza damu wakati wa kujifungua.

Baadhi ya wanawake hupata upotevu mkubwa wa damu wakati wa kujifungua, hali inayoweza kusababisha dharura ya kitabibu inayohitaji matibabu ya haraka na wakati mwingine kuongezewa damu.

Kwa hiyo, ni muhimu mama kuingia katika kipindi cha kujifungua akiwa na kiwango kizuri cha hemoglobini na akiba ya madini ya chuma.

Akiba ya damu katika vituo vya afya ni muhimu kwa ajili ya kuwahudumia wajawazito na wanawake wanaojifungua, hasa pale wanapopata matatizo ya kutokwa na damu nyingi. Picha| Ai | Fatuma Hussein.

Ni wakati gani huruhusiwa kuchangia damu?

Kwa utaratibu wa kawaida, mama haruhusiwi kuchangia damu katika kipindi chote cha ujauzito, bila kujali kama yupo katika miezi ya mwanzo, ya kati au ya mwisho.

Baada ya kujifungua, mama anahitaji muda wa kupona na kurejesha damu na madini ya chuma yaliyopotea. Mwongozo wa tathmini ya wachangiaji damu wa NBTS wa mwaka 2015 uliotolewa na Wizara ya Afya ulieleza kipindi cha kusubiri cha wiki sita katika mazingira yaliyotajwa, huku mama aliyepata damu ya kuongezewa akitakiwa kusubiri miezi 12.

Hata hivyo, wiki sita hazimaanishi kila mama anaruhusiwa kuchangia moja kwa moja baada ya muda huo. Anapaswa kupata tathmini na ushauri kutoka kwa wataalamu wa huduma za damu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
18 Nov, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
18 Nov, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
18 Nov, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
RC Chalamila: Nyumba za ibada zijengwe kwa kuzingatia mipango miji.

RC Chalamila: Nyumba za ibada zijengwe kwa kuzingatia mipango miji.

Nukta TV

JKT: Nafasi haziuzwi, hakuna upendeleo wala kurudia mafunzo

JKT: Nafasi haziuzwi, hakuna upendeleo wala kurudia mafunzo

Nukta TV

Noti za Sh1,000 na Sh2,000 kuchakaa haraka, nini kifanyike? wananchi wafunguka

Noti za Sh1,000 na Sh2,000 kuchakaa haraka, nini kifanyike? wananchi wafunguka

Nukta TV