Kuna nini Ngorongoro? Rais Samia ateua bosi mpya ndani ya miezi 7
- Amteua Dk Elirehema Doriye kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro.
- Dk Doriye anakuwa bosi wa pili kuteuliwa ndani ya miezi saba.
- Bosi huyo anasubiriwa kusafisha ‘nyumba’ ambayo CAG abaini uwepo wa madeni, hasara.
Dar es Salaam. Kuna nini Ngorongoro? Hili ni moja ya maswali mtu anaweza kujiuliza kutokana na bandika bandua inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) baada ya kumteua bosi mpya akiwa ni wa pili kuongoza taasisi hiyo ndani ya miezi saba.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu Mei 6, 2024, Rais Samia alimteua Dk Elirehema Doriye kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa mamlaka hiyo akichukua nafasi ya Richard Kiiza aliyefurushwa Machi, 2024.
Kiiza ndiye kiongozi aliyekaa muda mchache zaidi kulinganisha na viongozi wengine wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Kiiza alitenguliwa na Rais Samia miezi mitano tu tangu ashike wadhifa huo Oktoba 2023 akichukua nafasi ya mtangulizi wake Dk Freddy Manongi, Mhadhiri mstaafu wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Mweka aliyeongoza NCAA kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2013.
Dk Doriye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) tangu Julai, 2019 hadi Novemba 2023 alipoondolewa na Rais Samia kwa sababu ikielezwa kuwa “atapangiwa kazi nyingine”.
Soma zaidi:BOA Bank Tanzania yateua bosi mpya mwanamke
Yanayomsubiri Dk Doriye NCAA
Bosi huyo mpya atakuwa na kazi ya kusafisha taasisi hiyo kwa kuwa anaingia madarakani katika kipindi ambacho NCAA inakabiliwa na madeni na hasara kwa mujibu wa Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2022/23 inayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).
Ripoti hiyo inabainisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2022/23 mamlaka hiyo ilipata hasara ya Sh19.1 bilioni kutoka faida ya Sh13.86 bilioni mwaka 2021/22.
Suala lingine linalomsubiri Dk Doriye ni utekelezaji wa zoezi la kuwahamisha Wamasai kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda maeneo mengine yaliyopangwa na Serikali ikiwemo Msomera mkoani Tanga.
Uhamishaji huo unaoelezwa na Serikali kuwa unafanywa kwa hiari unakosolewa vikali na watetezi wa haki za binadamu wa ndani na nje ya nchi wakidai kuwa unavunja haki za binadamu ikiwemo kutowashirikisha watu wa eneo hilo.
Tangu kuanza kwa zoezi hilo Juni 2022, limekuwa likiibua mijadala kutoka kwa wadau mbalimbali na wanaharakati hususani katika mitandao ya kijamii huku Serikali ikibainisha kuwa lengo la kuwahamisha ni kulinda ekolojia ya hifadhi ya Ngorongoro na kuipa nafasi jamii hiyo kufanya shughuli nyingine za maendeleo mbali na ufugaji.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali Mobhare Matinyi, hadi kufikia Januari, 2024 jumla ya kaya 677 zenye watu 3,822 na mifugo 18,102 zimehama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia katika kijiji cha Msomera.
Idadi hiyo ya kaya zilizohamia Msomera ni sawa na asilimia 3.1 ya lengo la Serikali kuhamisha kaya 22,000 zilizopo Ngorongoro.
Hata hivyo, ripoti ya CAG imetoa angalizo kuwa huenda zoezi hilo lisikamilke kwa wakati kutokana na kukosewa kwa makadirio halisi ya bajeti ya kuwahamisha wakazi hao.