Kujipiga selfie kunavyosababisha magonjwa ya akili, vifo
- Kujipiga picha kwa kutumia simu mara kwa mara na kuziweka mtandaoni kunahusishwa na ugonjwa wa akili wa ‘Selfitis’ na wakati mwingine unasababisha vifo.
- Wataalam wawataka wanaojipiga picha kwenye maeneo hatarishi kuchukua tahadhari.
Tunaishi katika dunia ambayo watu wengi wanapenda kujipiga picha ‘selfie’na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kutunza kumbukumbu na kuwashirikishe wapendwa wao matukio muhimu katika maisha.
Tabia hiyo ya kujipiga selfie inatajwa kuwa ni mapinduzi makubwa ya tasnia ya upigaji picha duniani. Kwa kutumia simu yako ya mkononi unapata picha nzuri zenye muonekano tofauti.
Pamoja na uzuri wake kuna matokeo hasi ambayo yanaweza kujitokeza kwa mtu pale anapotumia vibaya teknolojia hiyo ikiwemo kupata ugonjwa wa akili na kufariki dunia.
Baadhi ya watu wanaojipiga selfie huamini kuwa picha zinawaongezea kujiamini, kukubalika na kusikilizwa, kuondoa msongo wa mawazo, kutengeneza kumbukumbu ya eneo alilotembelea, kuongeza ukaribu na ushindani kwa watu wanamfuatilia kwenye mitandao ya kijamii.
Lakini watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham Trent cha nchini Uingereza wanahusisha tabia ya kujipiga picha iliyopitiliza na ugonjwa wa akili wa ‘Selfitis’.
Waligundua tatizo hilo baada ya taarifa kulipotiwa na vyombo vya habari mwaka 2014 zilizotolewa na Chama Cha Marekani cha Tiba ya Akili kuwa kujipiga picha mara kwa mara ni moja ya dalili za kupata ugonjwa wa akili.
Watafiti hao walipoiona habari hiyo walifanya utafiti zaidi na kuthibitisha kuwa watu wengi wanaopenda kujipiga picha wana maradhi ya Selfitis.
Walitumia sampuli ya watu 400 ambapo waligawanywa kwenye makundi matatu ili kuangalia tabia zao za upigaji picha kwa kutumia simu za mkononi.
Kujipiga selfie ni burudani na ni njia ya kutunza kumbukumbu kwa uwapendao lakini usipotumia vizuri teknolojia hiyo inaweza kukusababishia magonjwa ya akili na kifo. Picha|Mtandao.
Washiriki wote walitoka nchi ya India ambako kuna matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na idadi kubwa ya watu wanaofariki kutokana na kujipiga picha ‘Selfie’ kwenye maeneo hatarishi kama majengo marefu, kwenye madaraja na mito.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa kwenye Jalida la International Journal of Mental Health and Addiction ambapo walibaini hatua tatu ambazo mtu hupitia mpaka kupata ugonjwa huo.
Watu waliopo hatua ya kwanza, hawa hujipiga picha mara tatu kwa siku lakini hawaziweki kwenye mitandao ya kijamii. Wale waliopo hatua ya pili hujipiga picha mara tatu kwa siku na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.
Hatua ya mwisho ambayo ni hatari ni ya watu ambao hawawezi kujizuia na hujipiga picha wakati wote na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii zaidi ya mara sita kwa siku.
Tabia ya kujipiga picha huanza taratibu kutoka hatua ya kwanza na mazoea yakizidi mtu hufika hatua ya tatu ambayo huathirika kisaikolojia na hujipiga picha kwa wingi na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kupata faraja kwa wanaomzunguka kwasababu anaamini hawezi tena kuishi bila kujipiga picha.
Zinazohusiana:
Mtafiti Dk Jonarthan Balakrishnan aliyeshiriki katika utafiti huo anaeleza katika ripoti ya utafiti huo kuwa, “Watu wenye maradhi hayo wanakosa ujasiri, wanajitahidi kuwa sehemu ya watu wanaowazunguka na wanaonyesha tabia za uraibu kama watu wengine.
“Ni matumaini kuwa tafiti nyingine zitafanyika ili kuelewa jinsi watu wanavyoingia kwenye hizo tabia na nini kifanyike kuwasaidia wale ambao wameathirika zaidi.”
Licha ya kusababisha magonjwa ya akili, Kujipiga selfie ni kisababishi cha vifo vya mshtuko wa moyo ambavyo hutokana na watu hao kujipiga picha kwenye maeneo hatarishi na muda usiofaa.
Kama wewe ni mpenzi wa selfie chukua tahadhari wakati wa kujipiga picha hasa kwenye maeneo hatarishi ambayo yanaweza kugharimu uhai wa maisha yako kama barabarani, sehemu ya miiniko ya juu kama pembezoni mwa ghorofa, kingo za mito au bahari na maeneo mengine yafananayo.