Kiswahili ndiyo mpango mzima kusaka wateja wengi Tanzania: Ripoti

August 27, 2018 3:36 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Utafiti wabaini kuwa “Kiswahili ndiyo lugha ya wateja Tanzania”.
  • Utafiti wa FSDT wa mwaka 2017 unaeleza kuwa takriban robo tatu ya Watanzania wanaweza kusoma na kuandika Kiswahili ikilinganishwa na robo tu ya wanaoweza kufanya hivyo katika Kiingereza.
  • Licha ya Kiswahili kuwa lugha ya biashara, bado wafanyabiashara watatakiwa kutumia lugha zingine kuvutia wateja wengi zaidi.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wenye mpango wa kutumia Kiingereza katika matangazo ya biashara na utoaji wa huduma nchini wajipange kubadili mikakati yao baada ya utafiti kubaini kuwa “Kiswahili ndiyo lugha ya wateja Tanzania”.

Ripoti ya utafiti wa masuala ya kifedha ya Finscope ya mwaka 2017 inabainisha kuwa watu saba kati 10 (asilimia 72) nchini wanaweza kusoma na kuandika Kiswahili vyema ikilinganishwa na takriban watatu tu kwa kila 10 wanaoweza kufanya hivyo katika Kiingereza.

Kwa mujibu wa utafiti huo, ni asilimia 27 tu ya Watanzania wanaweza kusoma na kuandika Kiingereza huku asilimia saba pekee wanaweza kusoma lugha hiyo ya kigeni.

Katika utafiti huo uliofanywa kati ya Aprili na Julai mwaka jana, imebainika kuwa Watanzania wawili kati ya watatu (asilimia 66) hawawezi kusoma wala kuandika Kiingereza ikiwa ni kiwango kikubwa ikilinganishwa na wale wanaoshindwa kufanya hivyo katika Kiswahili. Ni mtu mmoja tu kati ya wanne (asilimia 25) ambaye hawezi kuzungumza wala kuandika Kiswahili.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ili kutoa huduma kwa kundi kubwa la watu, taasisi za kifedha zinahitaji kufahamu lugha ambazo wateja wao huwa huru zaidi kuitumia.

“Hii ndiyo sababu iliyofanya utafiti wetu kuwauliza washiriki maswali ya msingi kabisa kwa kusoma na kujibu kwa kuandika.

“Matokeo yanaonyesha kuwa Watanzania wengi wanauelewa mkubwa katika lugha ya Kiswahili kuliko Kiingereza,” inasomeka sehemu ya ripoti ya utafiti huo ambao hufanywa na Taasisi ya ukuzaji sekta ya fedha Tanzania (FSDT) kwa ushirika na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar.

Licha ya Kiswahili kuwa lugha ya biashara, bado wafanyabiashara watatakiwa kutumia lugha zingine kuvutia wateja wengi zaidi ikizingatiwa kuwa utafiti huo unaeleza kuwa robo ya Watanzania au asilimia 25 hawawezi kusoma wala kuandika Kiswahili.

Matokeo ya utafiti huo huenda yakawa msaada kwa wafanyabiashara wengi nchini ambao hupendelea kutumia Kiingereza katika majina ya biashara na maelezo ya bidhaa bila kuwepo tafsiri ya Kiswahili.

Bila shaka kama unataka kufanya biashara unajua ni lugha gani ya ‘kudaka’ wateja zaidi Tanzania.

Enable Notifications OK No thanks