Kimbembe: Diamond, Harmonize wakichuana mtandaoni
- Diamond aongoza kwa wafuasi wengi kwenye mtandao wa YouTube na abaki kuwa msanii wa muziki mwenye wafuasi wengi zaidi Afrika.
- Harmonize ampiku Diamond kwa kuwa na maudhui mengi ya video Youtube.
- Rayvanny aliyeanza muziki rasmi mwaka 2015, ampiku Harmonze aliyemtangulia mwaka mmoja kwa kuwa na wafuasi wengi.
Dar es Salaam. Bila shaka ni ngumu siku kupita bila kusikiliza muziki ukiwa nyumbani au katika shughuli zako.
Kama hautasikiliza wewe mwenyewe kwa hiari yako, basi utakutana nao kwenye vyombo vya usafiri na hata barabarani ambako kuna maduka na shughuli mbalimbali. Huwezi kukwepa kusikiliza muziki.
Jambo hilo ndilo linawapa nguvu mwanamuziki wanapoingia studio kuhakikisha wanatengeneza nyimbo ambazo zitapendwa na kuwa kipaumbele kwenye spika za wananchi pale wanapowaza kusikiliza muziki.
Hali hiyo pia huzidisha mchuana baina ya wanamuziki kuhakikisha kila siku wanateka mioyo ya mashabiki waliopo katika kada mbalimbali wakiwemo wanaotumia mtandao wa Youtube.
Nukta (www.nukta.co.tz) inakuletea uchambuzi uliopo kati ya wasanii watatu wa Bongo Fleva wa Tanzania yaani Naseeb Abdul (Diamond Platnumz), Rajab Kahali (Harmonize) na Raymond Mwakyusa (Rayvanny) ambao wamekuwa wakigonga vichwa vya wafuasi wao mtandaoni.
Mnyukano huo ni wa kupigania kiti cha enzi cha kutawala wafuasi, watazamaji wa chaneli zao na maudhui wanayoweka katika mtandao huo ambao umekuwa kiungo muhimu kwa watengeneza maudhui ya video duniani.
Wafuasi katika mtandao wa YouTube
Kwa kipengele hiki, Diamond Platnumz amekimbiza akiwa na wafuasi milioni 4.1 kwenye mtandao wa Youtube. Idadi hiyo ya wafuasi inamfanya kuwa msanii mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mtandao huo kwa wasanii wa muziki barani Afrika akifuatiwa na Davido wa Nigeria mwenye wafuasi milioni 2.
Rayvanny ana wafuasi milioni 1.98 katika mtandao huo huku jeshi maarufu kama Harmonize akiwa na wafuasi milioni 1.97.
Diamond Platnumz anabaki kuwa msanii mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mtandao wa YouTube barani Afrika akifuatiwa na Davido wa Nigeria.
Idadi ya watazamaji kwenye chaneli zao
Kwa mara nyingine, Diamond Platnumz ana watazamaji wengi zaidi tangu ajiunge YouTube Juni 2011.
Msanii huyo anayetamba zaidi na kibao cha Yope (remix) kilicho na watazamaji milioni 110 ana jumla ya watazamaji bilioni 1.1 kwenye mtandao huo huku kati yao, 31.9 milioni amewapata siku 30 zilizopita.
Harmonize anamfuatia kwa mbali Diamond baada ya kujinyakulia watazamaji milioni 445 tangu ajisajili Youtube Oktoba, 2015 na kati ya watazamaji hao, milioni 19.6 wamepatikana siku 30 zilizopita.
Rayvanny anafunga orodha hii akiwa na watazamaji milioni 366 tangu ajiunge Youtube Machi 2016 na ndani ya siku 30 zilizopita, msanii huyo aliyetamba zaidi na kibao cha Tetema cha mwaka 2019 amejinyakulia watazamaji milioni 17.1.
Wingi wa maudhui mtandaoni
Kipengele hiki kimeongozwa na Harmonize ambaye kwenye mtandao wa YouTube ana jumla ya video 699 na video iliyotazamwa zaidi ikiwa ni ya wimbo wa Kwangwaru wenye watazamaji milioni 69 hadi kufikia jana (Septemba 1, 2020)
Harmonize amempita kidogo Diamond Platnumz ambaye chaneli yake ya Youtube ina jumla ya video 664 ambapo Yope ndiyo inampeperushia bendere ya umaarufu zaidi. Rayvanny anafunga orodha kwa kuwa na video 521 kwenye chaneli yake na ndani ya siku 30 zilizopita amepakia (upload) video 12.
Zinazohusiana
- Hawa ndiyo wanamuziki wa kike wanaotikisa dunia kwa wafuasi wengi Youtube
- Wanafunzi vyuo vikuu waugeukia muziki kutoka kimaisha
- Kwangwaru ya Harmonize inavyotikisa Youtube
Vipi kasi ya umaarufu kwenye chati za Google?
Chati za umaarufu za Google Trends ni chati zinazoonyesha kiwango cha ufuatiliwaji na umaarufu wa kitu, mtu na mahala kwenye mtandao wa kitafutio cha vitu mtandaoni cha Google.
Uchambuzi wa Nukta umempambanisha Diamond, Rayvanny na Hamonize kwenye chati hizo tangu mwaka 2016 hadi leo asubuhi (Septemba 2, 2020) na haya ndiyo matokeo:
Fahamu kuwa, namba zinawakilisha kiwango cha umaarufu cha msanii ikilinganishwa na namba 100 ambayo ndiyo kilele cha umaarufu kwenye chati za Google Trends
Mwenendo wa Diamond, Harmonize na Rayvanny mtandaoni tangu Januari 1, 2016 hadi Septemba 2, 2020. Picha| Google trends.
Diamond amefikia kilele hicho mara moja ndani ya miaka Minne ambapo aligota kwenye umaarufu wa Google Trends Machi, 2018.
Hata hivyo, kati ya Rayvanny na Harmonize, hakuna aliyewahi kumpiku Diamond katikia chati hizo za umaarufu mtandaoni. Wasanii hao wote walikuwa lebo moja ya Wasafi kabla ya Harmonize kuondoka na kuanzisha lebo yake.
Pia, chati za Google Trends zinamtaja Harmonize kama msanii anayekimbizana na Rayvanny ambapo kwa wastani, umaarufu wa Harmonize umegota kwenye namba 15 huku Rayvanny akiwa kwenye namba 10.
Wakati wawili hao wakipishana kidogo, umaarufu wa Diamond unawakilishwa na namba 41 chini ya 100.
Unahitaji kufahamu wanamuziki wa kike wanavyopigana vikumbo Youtube? Usikose kusoma Nukta Habari.
Latest