Kifaa kipya chabuniwa Tanzania kupunguza majanga ya moto yatokanayo na hitilafu ya umeme
- Kifaa hicho kinapunguza uwezekano wa majanga ya moto katika majengo ya biashara na makazi ya watu ambayo husababishwa na hitilafu za moto.
- Kampuni ya Tanzania yashirikiana kusanifu kifaa hicho ambacho hupangilia nyaya za umeme katika mfumo rafiki usioweza kushika moto kwa kasi.
Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu wanaosumbuliwa na tatizo la nyumba kupata hitilafu ya umeme au vifaa vyako kuharibika kutokana na mpangilio usio sahihi wa nyaya za umeme.
Hali hiyo inaweza kuwa inawasumbua wamiliki wa majengo makubwa ya biashara au ofisi ambayo yana vifaa vingi na mzunguko mkubwa wa umeme na kulazimika kuingia gharama kubwa za kukarabati na kununua vifaa vipya kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Basi matatizo hayo yatakuwa historia baada ya wataalamu wa Uhandisi Umeme kutafiti na kuja na suluhisho la kuharibika kwa vifaa vya umeme.
Suluhisho hilo ni kifaa kinachojulikana kama ‘DK Cable Junction Box” ambacho huwa kwenye boski maalum la plastiki, ambapo kazi yake kubwa ni kusimamia muunganiko wa nyaya mbalimbali zinazounganisha vifaa vya umeme na kielktroniki katika nyumba au majengo makubwa.
Teknolojia hiyo rahisi imebuniwa na kampuni ya Gemin Investment ya Jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na kampuni nyingine ya Hensel kutoka Ujerumani.
Ugunduzi wa kifaa hicho ulifanyika mwaka 2003 na kukidhi viwango vya ubora vya Shirika la Viwango Duniani kinakuhakikishia usalama wa vifaa vyako na nyumba yako kwa ujumla kutokana na uwezo wake wa kuzuia milipuko au moto kutokea.
Sifa yake kuu ni kustahimili aina zote za moto kwa muda mrefu kwa kutumia malighafi za “Metric Knockouts” zinachotengenezwa kulingana na asili ya kiunganishi cha nyaya “DIN” chenye ukubwa tofauti.
Mkurugenzi Mkuu wa Gemin Investment, Neema Kibasa amesema kifaa hicho ni suluhisho katika maeneo yenye kushika moto haraka kama vituo vya mafuta,“kifaa hiki ni kizuri sana kutumika katika vituo vya mafuta kwasababu moto unaweza kutokea na kikastahimili kusababisha hitilafu kwa haraka.”
Amebainisha ni vema watumiaji wa vifaa vya umeme kujihadhari mapema kwa kutafuta njia za rahisi za kudhibiti madhara yatokanayo na umeme ili kuokoa mali na maisha ya watu kabla tatizo halijatokea.
Technologia hii imesaidia pia mashirika ya zima moto yanayotumika sana katika hitilafu za umeme zinazojitokeza mara kwa mara katika baadhi ya sehemu.
Takribani miaka miwili iliopita iliwahi kutokea ajali iliosababishwa na umeme jijini Dar es Salaam, Ubungo na hii ni baada ya waya wa umeme kudondoka ghafla, hivyo kwa teknolojia hii inasaidia kama kuna hitilafu yoyote inayoweza kujitokeza kwa mpangilio usio sahihi wa nyaya.
‘DK Cable Junction Box” katika muonekano wake. Picha | Tulinagwe Malopa.
Latest



