Karsan atangaza kustaafu ukurugenzi UTPC
- Ameutumikia muungano huo kwa miaka 19.
- Awataka wanahabari kuzingatia maadili ya habari.
Mwanza. Mkurugenzi wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan amesema anatarajia kustaafu kazi hiyo ifikapo Desemba mwaka huu baada ya kuitumika kwa muda wa miaka 19.
Karsan aliyekuwa akizungumza wakati akifungua mkutano wa kuthibitisha kanuni za maadili ya uandishi wa habari mtandaoni na vyombo vya habari vya kawaida leo Juni 17 2022, Karsan amesema amechukua uamzi huo toka mwaka jana na tayari taratibu za kumpata mkurugenzi mpya atakayeiongoza taasisi hiyo umeshafanyika.
Amesema uamuzi wa kustaafu ameuchukua toka mwaka jana na hajasurutishwa na mtu na kwamba anawaachia vijana kuendesha taasisi hiyo ambayo imeanzishwa mwaka 2003.
“Nilichukua uamuzi wa kustaafu toka mwaka jana ambapo nilishirikisha viongozi kutoka bodi ya wakurugenzi ambao baada ya kuwaeleza matakwa yangu walinitaka niendelee kuwepo hadi mwishoni mwa mwaka huu, na baada ya kustaafu nitakuwepo nikimwangalia mkurugenzi mpya kwa takribani miezi mitatu,” amesema Karsan huku akiwataka waandishi wa habari kutoa ushirikiano kwa mkurugenzi huyo ambaye tayari ameshapatikana.
Soma zaidi:
- Teknolojia inavyotumika kuokoa mazingira
- Teknolojia ya kutengeneza matofali kwa taka za plastiki yaingia sokoni
- Taka za kielektroniki zinavyotafuna mazingira ya Tanzania
Amesema toka UTPC ianzishwe zipo changamoto nyingi ambazo amekutana nazo ambazo zimeifanya taasisi hiyo kuwa imara.
Mkurugenzi huyo amewataka waandishi wa habari kuzingatia kanuni na maadili ya uandishi wa habari na kuwa chachu katika kuisaidia jamii katika masuala ya chanjo ya Uviko-19 pamoja na Sensa ya Watu na Makazi.
“Hivi sasa wapo watu wanataka kukimbia makazi yao wakiamini siku ya Agosti 23 ndiyo siku ambayo watapelekewa chanjo nyumbani kwao, hivyo niwaombe waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha umma umuhimu wa zoezi la sensa,” amesema Karsan
Mkurugenzi huyo pia amewataka waandishi kujitokeza kwenda kuchanja ili kuwa na afya bora.
Awali Afisa Programu, Victor Moleka amesema kupitia mradi wa ulinzi na usalama wa waandishi wa habari wanapokuwa kazini na kwamba wamepanga kuwafikia waandishi wa habari 100 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Dodoma Dar es Salaam na Geita.
Amesema lengo ni kuwasaidia waandishi hususan wanaoripoti habari za mtandaoni kufuata maadili ya uandishi wa habari.
Latest
