Kardinali Pengo ang’atuka, Ruwa’ichi kushika madaraka
- Nafasi yake imechukuliwa na aliyekua Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Mwanza, Thaddeus Ruwa’ichi.
- Taarifa ya kuteuliwa kwa Askofu Ruwa’ichi limetolewa leo baada ya Papa Fransisko kuridhia ombi la Kardinali Pengo kustaafu.
Dar es Salaam. Askofu Mkuu Mwandamizi, Thaddeus Ruwa’ichi ameteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam akichukua nafasi ya mtangulizi wake Kardinali Polycarp Pengo ambaye amestaafu na hivyo kuwa Askofu Mkuu wa tatu mzawa tangu nchi ipate uhuru.
Taarifa ya kuteuliwa kwa Askofu Ruwa’ichi limetolewa leo (Agosti 15, 2019) baada ya Papa Francis kuridhia ombi la Kardinali Pengo kustaafu.
Katika taarifa hiyo, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Charles Kitima amesema kuwa Baba Mtakatifu amekubali ombi la Mwadhama Polycarp Pengo la kustaafu katika majukumu ya kuliongoza Jimbo kuu la Dar es salaam.
Agosti 9, 2019 katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuzaliwa kwake, Kardinali Pengo aliwaambia waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwamba anasubiria wakati wowote kumtii Baba Mtakatifu Francis atakapomwambia kupumzika katika utume wa kiaskofu.
Kardinali Pengo anachia madaraka ikiwa ni miaka 27 tangu alipochukua uongozi kutoka kwa Kardinali wa kwanza na Askofu Mkuu wa kwanza mzawa wa Jimbo kuu la Dar es salaam, hayati Kardinal Laurean Rugambwa Julai 22, 1992.
Akiwa ni Askofu Mkuu wa pili mzawa, Pengo ameacha parokia zaidi ya100 katika jimbo hilo na mafanikio mengine lukuki.
Soma zaidi: Mabilionea kulijenga upya kanisa la Notre Dame Ufaransa
Askofu Mkuu Ruwa’ichi ni nani?
Askofu Mkuu mpya, Ruwa’ichi ni miongoni mwa wanafunzi wa Kardinali Pengo ambaye alimfundisha katika Seminari Kuu ya Kipalapala pamoja na mwanafunzi wake mwingine Askofu Almachius Vincent Rweyongeza wa Jimbo Katoliki Kayanga.
Askofu Mkuu, Ruwa’ichi aliteuliwa na Papa Francis kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Kuu la Dar es Salaam Juni 22 mwaka jana kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa jimbo hilo leo.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi, Ruwa’ichi ambaye ni mtawa wa Shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini (Wafransisko) alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania.
Kardinali Polycarp Pengo (kushoto) akiwa na Askofu Mkuu mpya, Thaddeus Ruwa’ichi (katikati). Picha|Mtandao.
Kwa uteuzi huo anakuwa Askofu Mkuu wa tatu mzalendo ambaye ni mtawa.
Alizaliwa Desemba 30, 1953 katika kijiji cha Mulo mkoani Kilimanjaro. Baada ya masomo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe Novemba 25 1981.
Februari 9, 1999, askofu huyo, aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu na kuwekwa wakfu Mei 16, 1999.
Januari 15, 2005, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na kusimikwa Februari 19, 2005. Miaka mitano baadaye Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alimteua kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza kabla hajateuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Latest
