Karafuu yachangia kushuka kwa mauzo ya nje Zanzibar

February 6, 2019 2:45 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Karafuu zikiandaliwa kwa ajili ya matumizi. Zao hilo ambalo ni kiungo maarufu ni moja ya mazao mkuu ya biashara visiwani Zanzibar na huingiza fedha nyingi za kigeni. Picha|Mtandao.


  • Mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi Zanzibar yalishuka hadi Dola za Marekani 205.5 milioni (zaidi ya Sh468.5 bilioni) kwa mwaka ulioishia Novemba 2018 kutoka Dola Milioni 210 (zaidi ya Sh478.8 bilioni) Novemba 2017.
  • Ripoti mpya ya uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania yaeleza kuwa mauzo ya karafuu yalishuka zaidi ya mara mbili na nusu ndani ya mwaka mmoja. 
  • Hata hivyo, mauzo ya mwani, samaki yazidi kupaa.

Dar e Salaam. Thamani ya mauzo ya nje ya bidhaa na huduma visiwani Zanzibar imeshuka kidogo kwa Dola za Marekani takriban milioni tano ndani ya mwaka mmoja ikichagizwa zaidi na kuporomoka kwa mauzo ya karafuu yaliyoshuka kwa zaidi ya mara mbili na nusu.

Ripoti ya uchumi ya mwezi Desemba 2018 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi karibuni inabainisha kuwa mauzo ya nje ya bidhaa na huduma Zanzibar ilikuwa Dola za Marekani milioni 205.5 (zaidi ya Sh468 bilioni) kwa mwaka ulioshia Novemba 2018 ikilinganishwa na Dola za Marekani 210 (zaidi ya Sh478 bilioni) kipindi kama hicho mwaka 2017.

Hali hiyo, kwa mujibu wa BoT, ilisababishwa na kushuka kwa mapato ya mauzo ya nje ya karafuu na bidhaa nyinginezo.

“Thamani ya mauzo ya nje ya karafuu ilishuka hadi kufikia Dola za Marekani 18.3 milioni (Sh41.7 bilioni) mwaka ulioishia Novemba 2018 kutoka Dola za Marekani 48.1 milioni (Sh109.6 bilioni) iliyorekodiwa Novemba 2017 baada kushuka kwa kiasi cha uuzaji wa karafuu nje ya nchi kutokana na mwenendo wa msimu wa zao hilo,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.


Zinazohusiana: 


Karafuu ni zao la biashara  linaloongoza kwa kuingiza fedha za kigeni visiwani Zanzibar na kuchangia kuongeza vipato vya wakulima na mapato kwa Serikali.

Hata wakati karafuu ikishuka katika kipindi hicho, BoT imesema mapato ya mauzo ya nje ya mwani (Seedweeds) yaliongezeka mara mbili kutokana na kupaa kwa kiasi cha mzigo uliouzwa nje ya nchi katika kipindi hicho.

Kilimo cha mwani, kilichoanzishwa Mashariki mwa pwani ya Zanzibar mwaka 1989, kimekuwa moja ya vyanzo muhimu vya mapato kwa wakazi wa vijijini visiwani humo.

“Mapato ya mauzo ya nje kutoka kwenye samaki na bidhaa zitokanazo na samaki yaliongezeka vyema kutokana na mahitaji makubwa ya samaki hususan dagaa (anchovies) ambazo mara nyingi huuzwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC),” ripoti hiyo inaeleza.

Kilimo na uvuvi ni shughuli kuu za kiuchumi za wakazi wa Zanzibar zikifuatiwa na utalii unaozidi kukua kwa kasi.

Enable Notifications OK No thanks