Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Wataalam wanasema matumizi ya mitandao ya kijamii kwa wingi katika ndoa yanaweza kusababisha talaka, ugomvi usioisha na kutokuaminiana.
- Kuwa muwazi kwa kuongea na mwenza wako kuhusu utendaji wa mitandao ya kijamii ili kuimarisha mahusiano katika jamii.
- Jifunze kujiuliza kabla hujachukua maamuzi yoyote yanayoweza kuhatarisha uhusiano wako kwa ulichokiona kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mwenzi wako.
Dar es Salaam. Ukuaji wa teknolojia hasa matumizi ya mitandao ya kijamii sio kitu kigeni katika ulimwengu huu lakini kuna faida na hasara zake hasa katika muingiliano na mahusiano ya watu katika jamii.
Kupitia mitandao ya kijamii watu wamekua wakiigiza maisha kwa kuonyesha vitu visivyo halisi, jambo linaloleta mkanganyiko katika kutofautisha kinachoonekana katika mitandao ya kijamii na maisha binafsi ya watu.
Wapo wanaorusha picha mtandaoni zikiwaonyesha wakiwa na furaha katika mahusiano yao mpaka mtu mwingine ambaye ana changamoto za mahusiano akafikiri yuko sehemu isiyo sahihi.
Wengine wanaonyesha magari na nyumba za kifahari lakini hawaonyeshi vyanzo vya mapato yao na usiyefahamu kwa undani dhana ya mitandao ya kijamii unaweza kufikiri kuna sehemu unakosea katika kupambana na hali yako ya kimaisha.
Hali hiyo inaleta changamoto hata katika maisha ya wanandoa au watu walio katika mahusiano ya kimapenzi, na kutamani wanayoyaona katika mitandao yatokee kwenye maisha yao halisi.
Usiwe mtumwa wa mitandao ya kijamii na kutaka kushindana na watu na maisha yao, hasa ukiwa kwenye mahusiano ambayo yanaweza kuvunjika kwasababu tu ya kutamani maisha wanayoyaishi wengine.
Kila mmoja anajua sababu zake za kujiunga Facebook, Instagram, Twitter au mitandao mingine, hivyo uwe makini katika kuindesha, usifanye mitandao ikuendeshe na kuharibu mahusiano yako yawe ya kifamilia, kikazi au kijamii.
Mitandao ya kijamii ikitumika vizuri inaweza kuwa sababu ya kukuletea furaha na mawazo chanya. Picha| The insider.
Wataalam wa masuala ya familia taasisi ya McKinley Irvin Family Law wanasema matumizi ya mitandao ya kijamii hasa katika ndoa yanaweza kusababisha talaka, ugomvi usioisha na kutokuaminiana.
Lakini kabla ya kufikia katika talaka au kuachana kwa sababu ya matumizi ya mitandao ya kijamii inapaswa mtu kujifunza vitu vichache vitakavyoweza kukusaidia katika mahusiano yako.
Kuwa muwazi kwa kuongea na mwenza wako kuhusu utendeji wa mitandao ya kijamii na yeye msikilize anachotaka. Kuna watu ambao wanapenda kuonyesha mahusiano yao kwenye mitandao na wapo ambao hawapendi.
Hivyo ni vyema kuzungumza ili kutokuharibu mahusiano yenu. Kila mtu akianza kufanya anachotaka na bila makubaliano maalum kunaweza kusababisha mahusiano kuvunjika.
Inayohusiana: Apps hizi kukuepusha na uteja mitandao ya kijamii
Kuwa muwazi kuzungumza na mwenza wako kama kuna kitu umekiona mtandaoni kuhusu yeye na hujakipenda. Hii itasaidia kujenga mahusiano yenu na kupunguza nafasi ya kuwa na vitu vinavyokukwaza.
Mfano umekuta mkeo au mumeo anachati na mtu kwa lugha ambayo huielewi acha kukaa na vitu moyoni, mwambie kwa utaratibu na upole kuwa jambo fulani hulipendi au ajirekebishe kuliko kulimbikiza vitu moyoni.
Tambua tofauti ya maisha yenu binafsi na ya kijamii yaani usiache maisha binafsi yaendeshwe na mitandao ya kijamii.
Wapo ambao wakigombana ndani ya nyumba wanaamishia ugomvi wao kwenye mitandao ya kijamii, hii haileti picha nzuri kwa watu wanawaheshimu au wanaowazunguka. Jifunze kuwa na mipaka madhubuti usifanye mitandao ikutawale.
Jifunze kujiuliza kabla hujachukua maamuzi yoyote yanayoweza kuhatarisha uhusiano wako kwa ulichokiona kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mwenzi wako.
Hivyo ni muhimu kuwa na mizani ya kupima matumizi ya mitandao ya kijamii ili usiharibu mahusiano yako.
Watafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha intaneti na teknolojia cha Pew nchini Marekani wanaeleza kuwa asilimia 67 ya wanandoa wanajua nywila (password) za wenzi wao. Hivyo kama unajiamini mnaweza kubadilishana password zenu kujenga uaminifu na kuwa huru katika mahusiano yenu.
Lakini usisahau kuwa mitandao ya kijamii ipo na haitaondoka leo wala kesho hivyo ni kujipanga na uaminifu ndiyo vinavyoweza kukusaidia ukawa salama kwenye mahusiano yako.