Jinsi Dalali App inavyoweza kukuondolea usumbufu wa kutafuta nyumba, kiwanja
- Inamuunganisha mtu anayetafuta nyumba na mtandao wa madalali nchi nzima.
- Watumiaji hawahitaji kulipa fedha zaidi ya mara moja kwa mmiliki wa nyumba, kiwanja au shamba.
- Changamoto iliyobaki ni kuwajengea uwezo watumiaji kuchangamkia fursa ya teknolojia ya mtandaoni.
Dar es Salaam. Makazi mazuri ni moja ya hitaji la kila mtu. Ni miongoni mwa haki za msingi anazotakiwa kuzipata binadamu yeyote ili kumuhakikishia ustawi mzuri wa maisha yake. Makazi ni pamoja na kuwa na nyumba nzuri ya kuishi iwe ya kupanga au unayomiliki yenye miundombinu muhimu kama maji, umeme na hata njoo bora.
Lakini kila mtu ana mapendekezo ya aina ya nyumba anayohitaji kukidhi matakwa yake binafsi na watu wanaomzunguka. Kwa wengine nyumba ni ufahari na heshima.
Kwa wanaotafuta nyumba kuna njia mbalimbali ikiwemo kuzunguka mitaani na dalali. Kwa wanaopendelea kutumia teknolojia ya kisasa hawana haja ya kuingia mtaani kusaka nyumba bali popote walipo wanaweza kupata nyumba nzuri kulingana na bei, ukubwa na ubora wa nyumba yenyewe.
Dalali App iliyotengenezwa na vijana wawili wahitimu wa Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM), George Mushi na Ezekiel Nyamle inakuwezesha kupata nyumba, viwanja na mashamba kwa kukutanisha na madalali wenye uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya makazi.
Kwa kutumia simu janja unaweza kuwasiliana na madalali mbalimbali kulingana na mahitaji yako. Dalali App ina madalali 28 ambapo 11 kati yao ni madalali wakubwa wanaoweka picha za nyumba kila siku mtandaoni na 17 huweka kwa msimu kulingana na upatikanaji wa nyumba na eneo unalotaka kuishi.
Huduma hiyo imejikita kuhudumia wakazi wote waliopo Tanzania kupitia mtandao wa madalali wanaopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.
Muonekano wa Dalili App inayokuwezesha kupata nyumba inayoendana na uwezo wa kulipia. Picha| Dalili App.
Kutokana na urahisi wa kuitumia , Dalili App imewavutia watu wengi ambapo inatajwa kuwa suluhisho la malalamiko dhidi ya madalali wa mtaani ambao hutoza gharama kubwa za kukutafutia nyumba. Lakini inaokoa muda wa kutafuta mawasiliano ya dalali.
“Programu yetu ni rahisi kutumia wakati wowote kwas ababu inamwezesha mteja kupata huduma wakati wowote,” amesema Reuben Mbwiga mmoja wa Wasimamizi wa Dalali App.
Mbwiga anabainisha kuwa App yao inamwezesha mtu kulipa kodi moja kwa moja kwa dalali aliyemtafutia nyumba na kumepusha na usumbufu wa kulipa fedha mara mbili yaani kama ilivyo kwa madalali wengine wanaohitaji malipo zaidi ya mara moja.
Baadhi ya wananchi wa Dar es Salaam wameiambia Nukta kuwa wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wanapokutana na madali wa mtaani ambao huwatoza pesa ya kuzunguka kutafuta nyumba na ikiwa nyumba imepatikana basi mpangaji analazimika kumpa dalali kodi ya mwezi mmoja.
Ujio wa Dalali App ni muendelezo wa kutumia teknolojia ya simu za mkononi kutafuta suluhisho la changamoto za kijamii hasa katika miji mikubwa na kuwarahishia watu maisha.
Hata hivyo, Mbwiga na wenzake wana kazi kubwa ya kufanya kuiendeleza App yao ili iwafikie watu wengi ikiwemo kutoa elimu ya jinsi ya kuitumia na kuitangaza zaidi kupitia njia mbalimbali za mawasiliano na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Tumepanga kuwekeza kiasi flani cha pesa ili kuweza kufanya programu hii ikue na kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi,” amesema Mbwiga.
Muonekano wa Dalili App inayokuwezesha kupata nyumba inayoendana na uwezo wa kulipia. Picha| Dalili App.
Latest