Idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya malikale yashuka, mapato yapaa

June 24, 2019 6:48 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi hiyo imepungua kwa viwango tofauti kwa miaka miwili mfululizo ya 2017 na 2018.
  • Sababu kubwa ni kupungua kwa ziara za mafunzo ya wanafunzi wanaotembelea vivutio hivyo.
  • Serikali yasema imeanza kuboresha miundombinu ya vivutio hivyo ili kuvutia watalii wengi zaidi.

Dar es Salaam. Wakati sekta ya utalii ikiendelea kukua na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa (GDP), idadi ya watalii wanaotembelea malikale imeporomoka kwa miaka miwili mfululizo iliyopita.

Kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008, malikale ni rasilimali za urithi wa utamaduni ziinazoshikika na zisizoshikika; zilizo nchi kavu na majini. 

Rasilimali  hizo ni pamoja na masalia ya zana za mawe, metali, miti na mifupa; visukuku vya binadamu, mimea na wanyama; michoro  ya miambani, makuburi, ngome za kujilinda; na maeneo ya matambiko.

Vitabu vya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2017 na 2018, vinaeleza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya malikale imepungua kwa viwango tofauti katika kipindi hicho cha miaka miwili iliyopita. 

Mwaka jana, wageni 53,596 walitembelea vivutio vya malikale nchini ikilinganishwa na wageni 64,709 waliotembelea vivutio hivyo mwaka 2017, sawa na upungufu wa asilimia 17.2. 

Hali kama hiyo ilishuhudiwa mwaka 2017 ambapo idadi ya wageni ilishuka kwa asilimia 37.1 ikilinganishwa na wageni 102,879 waliotembelea vivutio hivyo mwaka 2016. 

Sababu kubwa ya kushuka kwa idadi ya wageni, kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, ni kupungua kwa ziara za kimafunzo za wanafunzi kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini.

Lakini ubora wa malikale unaathiriwa na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kuenea kwa hali ya jangwa na mmomonyoko wa ardhi, na uchomaji moto ovyo wa mistu ili kupata ardhi ya kilimo. 


Zinazohusiana:


Hali hiyo inatoa changamoto kwa mamlaka husika na wadau wengine kuongeza juhudi za kutangaza aina hiyo ya vivutio muhimu vya kihistoria. 

Mbali na matangazo, hali hiyo inawapa kibarua wadau hususan Serikali kuendelea kutunza mazingira na kubuni vivutio vipya vya utalii ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Tanzania. 

Wakati idadi ya wageni wanaotembelea malikale ikipungua, mapato yaliyotokana na viingilio vya wageni kwenye vivutio hivyo yameongezeka kwa asilimia 25.8 hadi kufikia Sh157.2 milioni mwaka uliopita kutoka Sh125 milioni mwaka 2017. 

“Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa siku ambazo watalii walikaa nchni,” inasomeka sehemu ya Kitabu cha Hali ya Uchumi kwa mwaka 2018.

Ripoti ya utafiti wa wageni wa nje ya nchi mwaka 2017 (International Visitors’ Exit Survey Report 2017) inaeleza kuwa wageni wanaotembelea Tanzania hukaa nchini kwa wastani wa siku 10 (10 nights). 

Magofu ya mji wa Kaole yaliyopo Wilaya ya Bagamoyo ambayo yamekuwa kivutio kikubwa cha watalii Afrika Mashariki. Picha|Mtandao. 

Licha ya idadi ya wageni wanaotembelea malikale kupungua, mji wa Kaole uliopo katika Wilaya ya Bagamoyo ndiyo unaoongoza kutembelewa na wageni wengi ukifuatiwa na mapango ya Amboni yaliyopo mkoani Tanga. 

Mathalani, mwaka jana, Kaole ilitembelewa na wageni 13,977 sawa na asilimia 26.07 ya wageni wote waliotembelewa vivutio hivyo na kuiingizia Serikali Sh33.34 milioni. 

Mji wa Kaole ni kati ya miji ya zamani ya kihistoria ya pwani ya Afrika Mashariki katika karne ya 13. Mji huu ulikua kwa sababu ya kutanuka kwa biashara na muingiliano wa wafanyabiashara wazawa na kutoka nje. 

Hata hivyo, Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kuendeleza maeneo ya malikale kupitia mashirika ya ili kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kiutalii na kuongeza mchango katika Pato la Taifa. 

“Mkakati huo unahusisha kuboresha miundombinu ya vituo hususan vituo vya kumbukumbu na taarifa, kuweka huduma muhimu kwa watalii, ofisi na barabara ili viwe na muonekano unaovutia na kufikika kwa urahisi,” alieleza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2019/2020. 

Katika mwaka 2019/2020, wizara itakarabati miundombinu ya vivutio sita vya malikale ikiwemo michoro ya Kolo wilaya ya Kondoa, magofu ya Kaole na Mji wa Zamani wa Bagamoyo natTembe la Livingstone (Tabora).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW