Hizi ndizo kampuni 10 zenye ubunifu zaidi Afrika, MPedigree imo

March 25, 2020 3:17 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kampuni inayowasaidia wananchi kutambua bidhaa feki kwa kutumia simu za mkononi.
  • Inaendesha mradi wa kubaini pembejeo feki za kilimo nchini Tanzania.
  • Imeshika nafasi ya pili ya ubunifu Afrika. 

Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia ya kimataifa ya mPedigree inayowasaidia wananchi kubaini bidhaa feki kwa kutumia simu za mkononi imetajwa kuwa miongoni mwa kampuni 10 za teknolojia zenye ubunifu wa kiwango cha juu barani Afrika kwa mwaka 2020.  

mPedigree yenye makao makuu Ghana na kufanya kazi katika nchi mbalimbali duniani imekuwa ikiwasaidia wananchi kubaini bidhaa feki zikiwemo dawa kwa kutumia simu za janja na za kawaida ili kulinda maslahi na afya za walaji.

Kwa Tanzania inawasaidia wakulima kubaini pembejeo feki za kilimo ikiwemo dawa na mbegu ili kuhakikisha wanazalisha mazao yenye ubora ili kupata kipato cha kuendesha familia. 

Katika orodha hiyo  (The 10 most innovative companies in Africa for 2020) iliyotolewa na kampuni ya Fast Company, mPedigree imeshika nafasi ya pili baada ya kuchuana vikali na kampuni ya Twiga Foods ambayo imeshika nafasi ya kwanza. 

Twiga Foods ya nchini Kenya imeshika nafasi ya kwanza kutokana na umahiri wake wa kutumia soko la mtandaoni ambalo linatoa fursa kwa watu kununua bidhaa huku likiwaunganisha wakulima na wanunuzi wa mjini wa mazao. 

Mkurugenzi Mtendaji wa mPedigree, Bright Simons ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa huo ni ushindi siyo tu kwa kampuni bali kwa wabia wote ambao wamekuwa wakishirikiana nao kuwasaidia wananchi kuepukana na bidhaa bandia zisizokidhi viwango.

“Tumepata nguvu nyingine ya kusonga mbele,” amesema Simons na kubainisha kuwa bado wataendelea kuboresha maisha ya watu kwa kutumia teknolojia rahisi ya simu.


Soma zaidi:


Kampuni zingine ambazo zimeingia 10 bora ya kampuni zenye ubunifu zaidi wa teknolojia Afrika ni pamoja na Copia Global ya Kenya, PiggyVest (Nigeria), Mpost (Kenya), Tizeti (Nigeria), Tongoro (Senegal), Lumkani (Afrika Kusini), Kobo360 (Nigeria) na 54Gene ya nchini Nigeria. 

Katika mradi wa kubaini pembejeo feki za kilimo nchini Tanzania, mPedigree inashirikiana na chemba ya biashara ya Jumuiya ya Soko la Pamoja la nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (Comesa) ili kupanua teknolojia ya ulinzi wa pembejeo za kilimo katika eneo lote la Comesa hasa kwa nchi ambazo hazikuwepo katika jumuiya hiyo.

Licha ya kuwa Tanzania siyo mwanachama wa Comesa, lakini teknolojia hiyo imewafikia pia wakulima nchini.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW