Hizi ndiyo tofauti kati ya iPhone 12 na iPhone13

September 15, 2021 8:22 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Licha ya muundo kufanana, simu hizi zinatofautiana ukubwa wa macho ya kamera.
  • Kamera za toleo la 13 zina uwezo zaidi na teknolojia mpya.
  • Kupata simu hizi andaa zaidi ya Sh2 milioni.

Dar es Salaam. Bila shaka umesikia kuwa kampuni ya Apple imeingiza sokoni bidhaa zake zikiwemo saa, simu na padi maana mtandaoni huko hakukaliki.

Kwa upande wa simu, Apple imezindua rasmi simu mpya ya iPhone 13 ambayo inaambatana na sifa lukuki za teknolojia.

Toleo la 13 limeambatana na simu nne ambazo ni iPhone 13, iPhone 13 Pro, iPhone 13 Pro Max na iPhone 13 mini.

Matoleo ya mini, na 13 ni mjadala wa siku nyingine. Kwa leo, wacha tuangalie Pro na Pro max zina nini hasa.

Baadhi ya watumiaji wa simu za iPhone wanasema kuwa simu hiyo haina tofauti ya kimuonekano na mtangulizi wake, iPhone 12 pro na pro max kwani kamera ni macho matatu na mpangilio wa kamera hizo ni kama sawa.

Hata hivyo, isisahaulike kuwa toleo la iPhone 7 plus na 8 plus pia hazikuwa na tofauti kubwa mbali na 8 kuwa na malighafi ya kioo kwenye upande wa nyuma ya simu na muonekano unaoelekea kwenye usawa upande wa mbele.

Kwa kuzilinganisha iPhone 13 Pro, Pro max na iPhone 12 pro na Pro max, huenda ukapitia changamoto hizo hizo kwani licha ya kufanana kwa simu hizi, zina tofauti kubwa. 

Mbali na tofauti zisizoonekana kwa macho ikiwemo uwezo wa uhifadhi na uwezo wa kamera, iPhone 12 na 13 ni kama mayai mawili yanayozidiana ukubwa. Na hizi ndiyo tofauti za simu hizo.

Bampa za kamera ya iPhone13 zimeinuka zaidi. Picha| Apple.

Muundo na uwezo wa kamera

Bila shaka hauwezi kuona uwezo wa kamera kwa macho lakini hauwezi kushindwa kuuona utofauti wa muundo na muonekano wa kamera za iPhone 13 unavyotofautiana na iPhone12.

“Macho” ya kamera za toleo la 13 ni makubwa ikilinganishwa na ya toleo la 12. Pia bampa ya kamera za toleo la 13 zimeinuka zaidi ikilinganishwa na za iPhone 12.

Mbali na muonekano wa nje, kamera za toleo la 13 zimeongezewa ubora wa utendaji kazi. Ukubwa wa macho haujaja kama pambo bali umekuja kuongeza ubora wa video na picha zinazopigwa na simu hizo.

Kwa mujibu wa Apple, kamera mpya zinafanya kazi nzuri kwenye mwanga hafifu, huku muundo wa sinema ukiwezesha umakini kwa hadhira (subject) muda wote wakati wa kurekodi video.

Katika simu hizi pia, sasa muundo wa “potrait” (muundo wa upigaji picha unaoweka umakini kwa hadhira) unaweza kutumika kwenye simu za video za “Facetime” (simu za video za kwenye iphone).


Maisha ya betri

Kila mtumiaji wa simu, anatamani wakati wote simu yake iwe na chaji ya kutosha kumuwezesha kufanya shughuli zake bila kuhofia simu yake kuzima.

Ikija kwenye upande wa betri, kwa sasa uwezo wa betri la toleo la iPhone 13 ni ongezeko la saa moja na nusu la kutumia ikilinganishwa na toleo la 12.

Kwenye uzinduzi wa simu hizo, Apple haikuweka wazi uwezo wa betri za simu zake mpya lakini ilisema “utapata nyongeza ya saa moja na nusu” ikilinganishwa na iPhone 12.

Hiyo ni kusema, kama kwenye matumizi yako ya iphone 12 Pro na Pro Max ulitumia saa 12, sasa utatumia kwa saa 13 na nusu.

Muundo wa kuvuta hadhira kwenye iphone 13 umeongezwa. Picha| Apple.

Uhifadhi wa kumbukumbu

Kwa watengeneza maudhui wanaotumia simu, huenda ikawa ni “jackpot” kwao kwani simu ikiwa na kamera nzuri na uhifadhi wa kutosha, hiyo ni ndoto iliyotimia.

Simu za iphone 12 Pro na Pro Max zilikuwa na uhifadhi wa hadi GB512, kwa matoleo ya iPhone 13 Pro na Pro Max, yana uwezo wa hadi Terabaiti (TB) moja, uhifadhi unaotosha mtu kuweka hadi picha milioni 4 na filamu 250 zenye ukubwa wa GB nne.

Unaweza kuzipata simu hizi zikiwa na uhifadhi kuanzia GB128, GB256, GB512, na TB1.

Mengine yanayokuja na simu hizi ni ulinzi zaidi wa skrini kupitia teknolojia ya ‘Ceramic Shield’ ambayo inapatikana kwenye simu za iPhone pekee.

Panga la mfukoni

Simu za iPhone matoleo mapya hayajawahi kuacha mifuko salama. Kwa simu za Pro na Pro Max, Apple imeandika bei za kuanzia Sh2 milioni huku bei ikipanda kulingana na uhifadhi.

iPhone13 Pro inanzia Sh2.3 milioni huku Pro Max zikianzia bei ya Sh2.5. Fahamu kuwa bei hizo ni kabla ya kodi na usafirishaji.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW