Hisa za Serikali kampuni ya Airtel Tanzania zaongezeka
Rais John Magufuli alipokutana na Mwenyekiti wa kampuni ya Bharti Airtel Sunil Mittal, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania. Picha| Michuzi.
- Hiyo ina maana kuwa hisa zinazomilikiwa na Bharti Airtel katika kampuni hiyo zimepungua hadi kufikia asilimia 51 kutoka asilimia 60 ambazo ilikuwa inamiliki hapo awali.
- Baada ya mazungumzo kukamilika kampuni hiyo kutoa gawio kwa Serikali.
Dar es Salaam. Kampuni ya Bharti Airtel imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali katika kampuni ya simu ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi 49 baada ya kuridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa yatakayozinufaisha pande zote mbili.
Hiyo ina maana kuwa hisa zinazomilikiwa na Bharti Airtel zimepungua hadi kufikia asilimia 51 kutoka asilimia 60 ambazo ilikuwa inamiliki hapo awali.
Hatua hiyo imefikiwa leo (Januari 11,2019) wakati Rais John Magufuli alipokutana na Mwenyekiti wa kampuni ya Bharti Airtel Sunil Mittal, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.
Mittal amesema kampuni yake imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali katika kampuni ya Airtel Tanzania kwasababu kampuni hiyo imeridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa yanayolenga kuzinufaisha pande zote mbili na kuboresha huduma za mawasiliano ya kampuni hiyo.
Inayohusiana: NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo
Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalianza Machi 12, 2018 baada ya Rais Magufuli kuunda kamati inayoongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi ili kutafuta suluhisho la umiliki wa hisa katika kampuni hiyo ya simu nchini.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema pamoja na kuongeza hisa za Serikali katika umiliki wa Airtel Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa gawio kwa Serikali mara baada ya mazungumzo hayo kukamilika hapo baadaye.
“Jambo zuri ni kuwa wamekubali kutoa gawio kwa Serikali ambapo kwa muda wa miaka minane hadi kumi hatukupata, kiasi cha asilimia ya gawio nacho watajadili leo, kwahiyo mimi naona ni mwanga mzuri wa kwenda mbele kwa kampuni ya Barti Airtel na Serikali ya Tanzania pamoja na kampuni zingine,” amesema Rais.
Juni 2016, Bharti Airtel pia ilisaini na kuingia makubaliano na Serikali ya kuachia hisa zao za asilimia 35 walizokuwa wakimiliki katika kampuni ya mawasiliano ya Tanzania (TTCL) ambapo sasa kampuni hiyo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.