Hii ndiyo zawadi unayoweza kumpatia mama yako
- Zaidi ya zawadi zote, ni upendo ambayo unaweza kuionyesha kwa kutumia muda wa kutosha na mama yako.
- Hakikisha unafahamu vitu ambavyo mama yako anapenda.
- Zingatia rangi na vitu vya muhimu vinavyodumu kwa muda mrefu.
Dar es Salaam. Kama wewe ni kati ya watu wanaojiuliza ni zawadi gani inamfaa mama yako, basi tambua kuwa haupo peke yako.
Hata hivyo, sintofahamu hiyo huenda inawakumba watu ambao hawajatumia muda wao mwingi na mama zao ikilinganishwa na ambao wametumia muda wao na mzazi huyo, hakika wanafahamu kipi kinaweza kumpatia tabasamu.
Je, ni vitu gani unavyotakiwa kuzingatia unapotaka kumnunulia mama yako zawadi?
Kabla ya kuwaza zawadi za vitu, zawadi kubwa ambayo unaweza kumpa mama yako ni upendo.
Allan Kipondya (23) amesema kwa upande wake, kutumia muda wa kutosha na mama yake humpatia faraja. Kumsumbua na kumtania kwa heshima, huweka tabasamu kwenye sura ya mama yake na inaongeza ukaribu baina yao.
“Mama yangu ni muhimu kwangu. Kwahiyo lazima nihakikishe ana furaha muda wote hivyo ninapenda kutumia muda wa kutosha kuwa pamoja naye na kumtania ili atabasamu,” Amesema Kipondya.
Zaidi, kijana huyo amesema kumsaidia mama yake kazi, kumheshimu na kutilia maanani ushauri wake ni kati ya vitu vinavyomfanya mama yake kuwa na furaha.
Baada ya kuhakikisha mama yako ana ufahamu upendo wako kwake, sasa unaweza anza kuangazia vitu ambavyo vinaweza kuongeza tabasamu usoni kwake.
Akina mama wengi wanapenda urembo. ukimnunulia mafuta na marashi apendayo, hakika tabasamu litashamiri usoni mwake. Picha| Mtandao.
Mwasisi wa shirika la Sanzuka Africa, Jessica Mtoi (24) amesema mbali na uwepo wako unahitaji kufahamu vitu ambavyo mama yako anavipenda pamoja na rangi ambazo anazifurahia.
Binti huyo amesema mama yake anapenda urembo, nguo na mikoba hivyo muda wote anapohitaji kununua zawadi ya mama yake, anajua pa kuanzia.
“Na vitu vingine ambavyo anapenda lakini hivyo ndivyo vipo ndani ya uwezo wangu,” amesema Jessica.
Zaidi, Jessica amesema unaweza kufikiria kumpeleka mama yako kwenye sehemu ya chakula na mkapata chakula cha pamoja.
Naye Mwandishi wa habari za kidijitali Detricia Pamba amesema kuikamilisha furaha ya mama yake, huchagua kuambatana na mama yake na kumpeleka sehemu za manunuzi ili ajichagulie anachokita.
“Mama yangu anapenda urembo hivyo mara nyingi huenda kwenye vitu vinavyohusiana na urembo.” amesema Detricia.
Huenda unajihoji vipi kama bajeti yako haitoshi kufanya hivyo lakini mwanadada huyo amesema ni ajabu kuwa mama yake anaelewa uwezo wake hivyo kuna vitu vingine anashika na akiona bei siyo rafiki huvirudisha.
Detricia baada ya hapo hujipanga na kisha kukinunua kitu kile na kumpelekea mama yake kama “suprise”.
Zinazohusiana
- Zawadi za kielektroniki unazoweza kumpatia umpendae msimu wa sikukuu
- Zawadi zinazowafaa wanawake sikukuu ya wapendanao
- Zingatia haya unapofanya manunuzi siku ya “Black Friday”
Naye Praxeda George mkazi wa Dar es Salaam amesema kwa upande wake hupenda mama yake amkumbuke kwa muda mrefu kwani mara nyingi anakuwa mbali naye hivyo hupenda kumnunulia zawadi ya vitu ambavyo vinadumu kwa muda mrefu.
“Nikimnunulia kiatu kizuri, kitenge na hata vifaa muhimu vya nyumbani mara nyingi tukiongea utasikia “nilikua nimevaa vile viatu ulivyoniletea” nikaenda sehemu fulani. Inanipa faraja,” amesema Praxeda.
Kwa vifaa vya nyumbani, Praxeda ameshauri kuangazia vitu vitakavyomrahisishia kazi kwa mfano mtungi wa gesi na jiko lake kuepuka matumizi ya mkaa.
Pia vyombo visivyopoza chakula ili apunguze kuhangaika jikoni na vitu vingine anavyovihitaji kwa mujibu wa mawazo yako.