Hesabu zawatoa jasho watahiniwa kidato cha nne, Kiswahili chawabeba

January 10, 2020 7:32 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Licha ya kuwa somo hilo ni muhimu kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, bado limekuwa likiwatesa zaidi wanafunzi katika ngazi zote za elimu ikiwemo kidato cha sita. Picha|Mtandao.


  • Watahiniwa katika somo la hisabati katika mtihani wa kidato cha nne 2019 ndiyo wamefeli zaidi kuliko masomo yote.
  • Ufaulu wake umefikia asilimia 20.03 ukiwa chini ya wastani wa kitaifa.
  • Kiswahili kimefaulisha kwa asilimia 91.31.

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa juhudi zaidi zinahitajika kuboresha ufundishaji wa somo la hisabati ili kuwazesha wanafunzi kufanya katika somo hilo, ambalo watahiniwa katika mtihani wa kidato cha nne 2019 ndiyo wamefeli zaidi kuliko masomo yote. 

Hilo limejihirisha baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutangaza  matokeo ya mitihani wa kidato cha nne iliyofanyika Oktoba mwaka jana na kuonyesha kuwa asilimia 20.03 tu ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wa somo hilo ndiyo wamefaulu. 

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila wanafunzi 10 waliofanya mtihani wa hisabati mwaka jana, nane kati yao wamefeli. 

ufaulu wa somo hilo kwa mujibu wa takwimu za Necta uko chini zaidi ya mara ya wastani wa kitaifa uliowekwa na baraza hilo kwa masomo ambao ni asilimia 50. 

Hata hivyo, ufaulu katika somo hilo umeongezeka kidogo ikilinganishwa na ilivyokuwa katika matokeo ya mwaka juzi ambapo watahaniwa waliofaulu walikuwa asilimia 20.02 kutoka asilimia 19.19 ya mwaka 2017. 

Licha ya kuwa somo hilo ni muhimu kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, bado limekuwa likiwatesa zaidi wanafunzi katika ngazi zote za elimu ikiwemo kidato cha sita.

Kwa mujibu wa takwimu za matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2018 somo lililowatesa zaidi wanafunzi lilikuwa ni “Basic Mathematics” (hisabati) ambalo ufaulu wake ulikuwa wa chini zaidi ya masomo mengine wa asilimia 55.3.

Somo lingine ambalo watahiniwa wa kidato cha nne 2019, wamefanya vibaya ni Fizikia ambalo ufaulu wake ni asilimia 48.38 au sawa na kusema karibia ya nusu ya watahiniwa katika somo hilo walifaulu. 

Hata hivyo, ufaulu wa somo uko chini ya wastani wa kitaifa wa silimia 50, japokuwa ufaulu wake umekuwa ukiimarika kila mwaka

“Takwimu za matokeo zinaonyesha watahiniwa hawakufanya vizuri katika masomo mawili ya Physics (Fizikia) na Basic Mathematics (Hisabati), japokuwa ufaulu katika somo la Physics umeendelea kuimarika kutoka asilimia 45.50 mwaka 2018 hadi asilimia 48.38 mwaka 2019,” inaeleza sehemu ya taarifa ya matokeo yaliyotolewa na Necta Januari 9, 2019.


Zinazohusiana


Masomo yaliyobaki tisa, ufaulu wake uko juu ya wastani wa kitaifa. 

Wakati masomo ya Hisabati na Fizikia yakiwatesa zaidi wanafunzi, upande pili somo la Kiswahili limewatoa kimasomaso watahiniwa hao baada ya kufaulu kwa asilimia 91.31 au sawa kusema kwa kila wanafunzi 10 basi tisa wamefaulu somo hilo.

Ufaulu wa Kiswahili ni zaidi ya mara nne ya ule wa somo la hisabati, somo ambalo ni lugha ya Taifa na ambayo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu nchini, wamekuwa wakipendekeza itumike kama lugha ya kufundishia darasani ili kuwaongezea wanafunzi uelewa wa masomo.

Somo ambalo linatumika kama lugha ya kufundishia katika shule za sekondari la English Language (Kiingereza), wanafunzi wamefaulu kwa asilimia 65.78.

Pia Kemia (Chemistry) ambalo ni miongoni mwa masomo ya sayansi, limekuwa somo la pili ambalo wanafunzi wamefaulu zaidi baada ya Kiswahili, ambapo ufaulu umefikia asilimia 76.76. 

Civics ufaulu umekuwa asilimia 64.17, History (asilimia 51.25), Geography (asilimia 53.15), Biology (asilimia 55.26), Commerce (asilimia 51.57) na Book Keeping (asilimia 53.06).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW