Hatua za kufuata unapojenga ‘brand’ katika maisha yako
- Kubali kufundishika na jenga mtandao wa marafiki watakaokuhamsisha kuwa bora kwa kile unachokifanya.
- Uvumilivu na kutokataa tamaa ni silaha nyingine ya kuimarisha brand yako.
Dar es Saalam. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Branding Africa Limted, Charles Nduku maarufu kama “Mr Brand’ amewashauri vijana wenye ndoto za kutimiza malengo ya maisha kujenga utambulisho binafsi (Personal Brand) kwa kukubali kufundishika na kutengeneza mtandao wa marafiki wenye maono ya kufanikiwa.
Nduku aliyekua akizungumza leo (Agosti 9, 2019) jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumza na wafanyakazi wa kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa, amesema ‘brand’ ndiyo utambulisho wa mtu katika majukumu ya kila siku anayofanya.
“Personal Brand ni jinsi watu wanavyokuzungumzia kwa sifa zako ukiwa haupo ambazo zinategemea unavyoongea, unavyotenda na unavyoonekana,” amesema Nduku.
Amesema ili mtu ajenge brand imara inayoheshimika na kuthaminiwa anatakiwa kufuata hatua sita ambazo zinajengwa katika msingi ujuzi, maarifa na mtazamo.
Katika hatua ya kwanza ya kujenga brand ni lazima mtu awe na kitu kitakachomtambulisha kwa watu ambapo inaweza kuwa ujuzi, tabia na hata uwezo fulani wa kufanya mambo ambayo yanaweza kuleta matokeo chanya kwenye jamii.
Nduku ambaye amekua akitoa mafunzo mbalimbali ya jinsi ya kujenga utambulisho binafsi, amesema kufundishika ni hatua nyingine inayoweza kuimarisha brand ya mtu. Ikiwa mtu ataacha kujifunza katika maisha yake anakuwa sawa na mtu aliyekufa.
“Tujifunze kila siku, kama hujifunzi utakua mwongo bila kujali umri wako. Tenga hata nusu saa kwa siku kujifunza kipya,” amesema Nduku.
Charles Nduku akifundisha wakizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa | Picha na Tulinagwe Malopa.
Jenga mazoea ya kuongea mbele za watu na kuandika vitu vinavyoendana na taaluma au maisha yako ili kuwaelimisha watu wengine. Kuongea na kuandika kutakupa shauku ya kujifunza na kutafuta taarifa sahihi zitakazoongeza ujuzi wako kwa kile unachokifanya.
Amesema katika kuongea ni muhimu pia kujifunza jinsi ya kutumia lugha ya mwili na maneno mazuri yanayoweza kufikisha ujumbe kwa urahisi kwa watu wanaokusikiliza.
“Asilimia kubwa ya ujumbe unaoutoa, unaelezwa zaidi na lugha ya mwili. Kuna muda maneno mtu anayosema yanatofautiana na matendo ya mwili wake,” amesema Charles.
Aidha, Nduku amebainisha kuwa brand inajengwa kwa kujichanganya na kuimarisha mahusiano mazuri na jamii inayokuzunguka kwa sababu watu wana sehemu kubwa ya kuchangia kukua kwako au anguko lako.
Anasema kaa na watu wanaokuhamasisha na kukusaidia kufanya mambo makubwa yakayokusaidia kutimiza ndoto zako na kutoa mchango unaohitajika katika jamii.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
- Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
Hata hivyo, amesema safari ya kujenga brand inahitaji uvumilivu na kutokukata tamaa kwa sababu changamoto haziepukiki katika maisha.
“Muda mwingine, mtu wako wa karibu ndiye atakayekukatisha tamaa! Endelea mbele,” amesema Nguku.
Nduku amekutana na wafanyakazi wa www.nukta.co.tz ili kubadilishana uzoefu wa juu ya kujenga brand imara ya kampuni na watu binafs.
Mkurugenzi wa kampuni ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema uzoefu uliotolewa na nduku ni muhimu siyo tu kwa shughuli za kitaaluma na kikazi bali hata maisha binafsi ya mtu katika ngazi ya familia kwa sababu unaezea njia sahihi za kua bora katika maeneo yote ya utendaji wa shughuli za kila siku.
Amemshukuru Nduku kwa kuitembelea kampuni hiyo huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa kampuni yake ya Branding Africa Limited hasa katika miradi inayolenga kukuza uelewa wa utambulisho wenye manufaa.
Mkurugenzi wa kampuni ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen (kulia), Afisa Utawala, Maphosa Banduka (katikati) na Mwanahabari, Rodgers Raphael wakimsikiliza Charles Nduku ambaye hayuko kwenye picha wakati alipotembelea kampuni hiyo leo. Picha| Tulinagwe Malopa.
Latest