Hakuna uhaba wa mafuta Tanzania – Makamba

November 12, 2021 10:16 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya taarifa kuenea kuwa mafuta yaliyopo yanatoshwa kwa matumizi ya wiki mbili.
  • Amesema meli mbili zinashusha mafuta sasa bandarini.
  • TPDC nao wakanusha madai hayo.

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kuwa hakuna uhaba wa mafuta nchini kwa sasa baada ya taarifa kuenea mtandaoni kuwa mafuta yaliyopo Tanzania yanatosha kutumika kwa wiki mbili tu.

Mafuta hayo ya petroli na dizeli hutumika kuendesha vyombo vya moto yakiwemo magari na mitambo ya uzalishaji viwandani.

“Hakuna uhaba wa mafuta nchini. Hakuna sababu ya kuwa na taharuki. Utaratibu wa kuingiza mafuta unahakikisha kwamba mahitaji yapo wakati wote. Serikali inaendelea kuchukua hatua kuongeza uhakika wa upatikanaji na unafuu wa bei,” amesema Makamba katika ukurasa wake wa Twitter leo Novemba 12, 2021.

Kauli ya Makamba imekuja baada ya gazeti moja la kila siku kumnukua Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio katika semina ya waandishi wa habari kuwa mafuta yaliyopo yanatosha kutumika kwa wiki mbili, hali inayoiweka nchi katika hali ya hatari endapo hatua zinazokwenda kuchukuliwa hazitafanikiwa.

“Kauli ya uhakika ni ya Serikali. Mkurugenzi wa TPDC atatoa taarifa kuhusu taarifa yake hii maana yake aliitoa kwenye semina ya wanahabari lakini ni gazeti moja tu ndiyo limeandika. Pia atakuja ofisini kutoa maelezo kabla hatujachukua hatua za ziada,” amesema Makamba kuhusu kauli ya Dk Mataragio.

Aidha, Makamba amesmea dizeli iliyopo kwenye matenki nchini hadi leo asubuhi ni lita milioni 90.7 na kubainisha kuwa meli inayoitwa Sloane Square iko katika bandari ya Dar es Salaam inashusha lita milioni 60.9.

Hiyo ina maana kuwa mafuta ya dizeli yataongezeka na kuwa lita milioni 151.6 na kutosheleza kwa siku 24, kwa mujibu wa waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga.

“Petroli iliyopo kwenye matenki nchini hadi leo asubuhi ni lita milioni 100.3. Meli iitwayo James Cook inashusha lita milioni 22.4; meli iitwayo Jag Punit  iko njiani na lita milioni 30.5 hivyo kupeleka mafuta ya petroli kuongezeka na kuwa lita milioni 153.4 yanayotosheleza kwa siku 34,” amesisitiza Makamba.

Muda mfupi baada ya waziri huyo kutoa ufafanuzi huo, TPDC katika akaunti yake ya Twitter nayo imeeleza kuwa hakuna uhaba wa mafuta nchini.

“Hakuna uhaba wa mafuta nchini,” imeeleza TPDC ikumnukuu Dk Mataragio.

Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta (TAOMAC) nacho kimeeleza kuwa kinafahamu kwa sasa kuna hifadhi ya kutosha ya mafuta kwa sasa na hakuna upungufu.

“Tunafahamu kuwa wanachama wetu tayari wameagiza hifadhi ambayo yanaweza kutosheleza ahadi Desemba 2021,” imeeleza taarifa ya TAOMAC katika mtandao wa Instagram na kubainisha kuwa meli za mafuta zimetua nchini kupakua mafuta.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW