Filamu kali za kutupia macho kabla ya kuuaga 2024

December 24, 2024 3:35 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Zimesheheni wakongwe wa tasnia ya uigizaji wakiwemo Cynthia Erivo, Ariana Grande na Dwayne Johnson.
  • Kama hauna pa kwenda kufurahia sikukuu basi zifanye filamu hizi kuwa rafiki msimu huu.

Dar es Salaam. Unafahamu kuwa msimu wa mwisho wa mwaka ndio muda ambao watu wengi huchukua mapumziko kwa ajili ya kufurahia na familia, ndugu, jamaa na marafiki?

Lakini pia baada ya mapumziko ndio muda pekee wa wewe kurudi kazini ukiwa na mawazo na nguvu mpya ya kufanya kazi.

Filamu (movies) zinaweza kuwa njia ya kupumzisha akili na kukusanya nguvu kwa ajili ya mwaka 2025. Unaweza kwenda katika kumbi za sinema zilizopo karibu na eneo lako. Kama hupendi mikusanyiko ya watu basi unaweza kutazama ukiwa nyumbani. 

Siku hizi kila kitu kimerahisishwa kwani unaweza kumiliki ukumbi wa filamu ukiwa ndani na bado ukafurahia mapumziko yako. Tumia jukwaa la Netflix kutazama filamu mbalimbali. Ukiwa nyumbani. 

Kabla ya mwaka 2024 kuisha usikose kutazama filamu hizi zilizokonga mioyo ya watu, zitaenda kukonga moyo wako pia:

Wicked

Jambo la kwanza unalopaswa kuelewa kuhusu toleo jipya la sinema ya Wicked ni kwamba, ina urefu wa muda zaidi kuliko tamthilia nzima ya muziki wa Broadway. Picha /Slate.com.

Filamu hii inaelezea wachawi wawili maarufu kutoka mandhari ya kufikirika, Emerald City. Nao ni Elphaba (Mchawi Mbaya) na Glinda (Mchawi Mzuri). 

Hadithi inaangazia maisha yao ya mapema walipokuwa wanafunzi katika Chuo cha Shiz. Urafiki wao wa ajabu ulianza baada ya Glinda, mtoto wa kishua ambaye anajiona yeye ni wa matawi ya juu kuliko wengine kujikuta anakubali kuchangia chumba na Elphaba.

Alifanya hivyo ili kupata nafasi ya kufundishwa na mwalimu aliyemchangua Elphaba baada ya kuonesha nguvu zake za ajabu mbele ya wanafunzi .

Elphaba anapata uwezo wake wa kichawi na kugundua madhira ya wanyama wenye uwezo wa kuongea katika mji wa Oz, jambo linalomsukuma kuwa mpinzani dhidi ya unyanyasaji huo kutoka kwa mchawi mkuu wa Oz anayetaka utawala pasipo kuwa na uwezo wa kusoma kitabu cha kichawi.

Pamoja na Glinda, ambaye anachukua njia tofauti, hadithi inaacha maswali ya wazi juu ya nini kitaendelea baada ya Elphaba kuanzisha vita juu wa mchawi mkuu hasa ikiwa alimtazamia kwa mapana kama kiongozi ama vile wenzetu husema “inspiration”.

Ataweza kuvuka daraja hilo alilochagua kupita ikiwa Elphaba hapendwi na karibu kila mtu?

Nisimalize uhondo wa filamu hii nenda kaingalie ujionee utamu wake huku ukiburudika na nyimbo mbalimbali kutoka kwa wahusika.

Filamu hii inawaleta pamoja wanavokali na waigizaji machachari akiwemo Cynthia Erivo, Ariana Grande, Jonathan Bailey na Michelle Yeoh. Ambao bila shaka unewaona kwenye filamu kadha wa kadha awali.

Moana 2

Moana 2 imeweza kuleta ladha inayofanana na ile ya awali huku ikiboresha mambo mengi kwa njia mbalimbali. Picha / Jo blo.

Sijajua nikuambie nini kama haujaiona sehemu ya kwanza ya filamu ya Moana. Nakosa maneno kwani najua kwa jinsi nyimbo zake zilizotamba mwaka 2016, lazima utakuwa ulivutiwa nayo kimtindo hata kama hutaki kukiri.

Moana 2 ni filamu, iliyozalishwa na Walt Disney Animation Studios. Hii ni filamu ya 63 katika orodha ya filamu za michoro za Disney ambayo imekuja machoni kwako Novemba 27, 2024.

Miaka mitatu baada ya filamu ya kwanza, Moana anaanza safari ya kugundua siri za kisiwa cha Motufetu kilichozikwa na Mungu wa dhoruba, Nalo.

Akisaidiwa na Maui, mababu zake, na marafiki wapya, Moana anakabiliana na changamoto za baharini. 

Hebu katupie macho filamu hii wakati tukisubiri msimu wa tatu ili kujua nini kitatokea mwaka 2025.

Spellbound

‘Spell bond’ ni neno linatokana na maneno ‘kufungwa,’ ambalo linamaanisha kushikiliwa au kuzuiliwa, na ‘uchawi. Picha /The toy insider.

Katika filamu hii utamuona binti wa kifalme Ellian ambaye anatakiwa kuanza safari ya kijasiri. Anatakiwa kuikoa familia yake baada ya uchawi wa ajabu kuwageuza wazazi wake, Mfalme na Malkia wa Lumbria, kuwa majitu ya kutisha (monsters).

Kama bado hujaitazama filamu hiii basi unakosa uhondo kwani ina ujumbe mzuri uliojificha ndani ya hadithi yake ya kusisimua inayozungumzia madhara ya talaka na jinsi inavyoweza kuvunja familia.

Katika ufalme wa kichawi wa Lumbria, binti mfalme Ellian anapaswa kukubaliana na ukweli kwamba wazazi wake, Mfalme Solon na Malkia Ellsmere, waligeuzwa kuwa ‘monsters’ wa porini mwaka mmoja uliopita, baada ya safari katika msitu mweusi wa giza la milele. 

Washauri wa kifalme, Mawaziri Bolinar na Nazara Prone, wanamsaidia kusimamia na kuficha monsters hawa kutoka kwa umma, lakini bila mafanikio ya kuwageuza tena, wanadhani Ellian anapaswa kuwa Malkia mpya kwani atatimiza umri wa miaka 15.

Kama jaribio la mwisho la kuwarejesha wazazi wake, Ellian anapanga mkutano na miungu wawili, Sunny na Luno, Oracles wa Jua na Mwezi mtawalia, mpango ambao unakosa mafanikio baada ya Monsters kuwatisha na hivyo kukimbia.

Binti mfalme hakukata tamaa kwani anaimani kuwa ipo njia ya kuwaokoa wazazi wake na hapo ndio safari inaanza.

Akiwa njiani, anaongozwa na ndimi za moto kufikia sehemu ya nuru ambako anaamini wazazi wake watabadilika tena kuwa wanadamu. Magomvi ya hapa na pale, usaliti, na kuvunjika moyo ni sehemu tu ya safari ambayo anaipitia binti mfalme Ellian.

Unakosaje kutazama filamu hii iliyojaa ujumbe wa kufunza juu ya maisha ya upendo na familia? Kazi ni kwako.

Elevation

‘Elevation’ imeongozwa na George Nolfi na kuandikwa na Kenny Ryan na Jacob Roman. Inaigizwa na Anthony Mackie, Morena Baccarin, na Maddie Hasson. Picha / When to Stream.

Miaka mitatu nyuma wanyama wakali na hatari waliotambulika kama ‘reapers’ walitoka kwenye mashimo ya ardhini na kuangamiza sehemu kubwa ya binadamu. 

Wanaosalia wanaishi katika jamii ndogo zilizo juu ya mlima, mwinuko ambao viumbe hawa hawafiki. Moja ya jamii hizo ndogo ni ‘Lost Gulch Refuge’ ambapo baba mmoja, Will, anaishi na mtoto wake, Hunter, ambaye ana ugonjwa wa mapafu. 

Will anateseka kutokana na kifo cha mkewe,Tara, ambaye aliuawa na reapers akiwa safarini na Nina, mwanasayansi wa zamani, kutafuta udhaifu wa viumbe hao. 

Hunter anakuwa mwepesi baada ya miezi ya kutengwa na jamii za majirani. Majirani hao wanazima redio zao ili kuhifadhi umeme uliobaki na kutumia bendera kuwasiliana. Will anakubaliana na ukweli kwamba anamaliza mitungi ya oksijeni kwa Hunter.

Nina anajaribu kumzuia Will asiende mpakani Colorado kutafuta mitungi zaidi, lakini Will anamshawishi aje pamoja naye ili kufikia maabara yake ya zamani na kupata njia ya kuua reapers.

Nina ana kifaa cha kompasi alichovumbua kinachoweza kugundua reaper aliye karibu kutokana na mawimbi yao makubwa ya bayoelectromagnetiki. 

Je unahisi watafanikiwa katika safari yao licha ya uwepo wa wanyama hatari? Jibu maswali hayo kwa kuitazama filamu hii kabla ya mwisho wa mwaka wa 2024.

Red one

‘Red One’ ni chaguo la kwanza la kwanza la vijana wa kiume. Picha / Tv insider.

M.O.R.A ni shirika la kijeshi la kimataifa lenye usiri mkubwa. Linadhibiti na kulinda mkataba wa amani wa siri kati ya viumbe vya kihistoria na wanadamu. 

Callum Drift, kamanda wa ELF ambaye ni mkuu wa kikosi cha ulinzi wa Santa Claus, anaomba kustaafu katika msimu wa mwisho wa Krismasi, akiwa amevunjika moyo kutokana na ongezeko la tabia mbaya ulimwenguni.

Usiku wa Krismasi, timu ya operesheni za siri inavunja usalama wa eneo la North Pole na kumteka Santa. Callum anamjulisha mkurugenzi Zoe Harlow kuhusu utekaji huo. Timu yake inagundua kwamba eneo la siri la North Pole lilivujishwa na Jack O’Malley, mdukuzi wa kijasusi ambaye anadai anaweza kupata chochote duniani.

Zoe anamkamata Jack kwa mahojiano. Jack, ambaye kwa muda mrefu hakuwa akiamini uwepo wa Santa, hakujua kwamba taarifa alizodukua zilihusiana na Santa na alizituma tu kwa mnunuzi asiyejulikana. 

Zoe anatoa ofa ya kumlipa Jack mara mbili ya malipo aliyopokea ikiwa atawasaidia kumpata Santa, lakini anaweka kifaa cha kumfuatilia ndani yake.

Callum kwa shingo upande anakubaliana kufanya kazi na Jack kumtafuta Santa kwa kufuatilia wakala aliyeandaa mpango kati ya Jack na mtekaji huko Aruba. 

Wakala huyo anawaambia kwamba mtekaji ni mchawi wa majira ya baridi, Grýla. Grýla anapata taarifa kuhusu mazungumzo yao na kutuma snowmen wake kuwaangamiza lakini Callum na Jack wanawashinda.

Je Callum na Jack watafanikiwa kujinasua kwenye mtego wa Grýla? 

Usikose kufuatilia mkasa huu wa kusisimua ili muone bwana Santa akifanya vitu vyake.

Filamu hizo ni miongoni mwa filamu nyingi unazoweza kuzitazama katika mapumziko ya mwisho wa mwaka. Kazi ni kwako kuburudika katika ulimwengu wa filamu kupitia majukwaa ya mtandaoni ikiwemo Netflix. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks