Fahamu undani wa kusajili nembo ya pekee ‘Trade Mark’ Tanzania – 1

August 25, 2020 7:59 am · Hamza Yusuph
Share
Tweet
Copy Link
  • Moja ya faida ya nembo ya kipekee (trade mark) ni kuwa nembo yako ya biashara sasa italindwa kisheria. 
  • Ukisajili nembo yako Tanzania Bara unapaswa pia kusajili Zanzibar.

Huenda umesikia habari za nembo ya kipekee au maarufu kwa Kiingereza ‘Trade Mark’ katika masuala ya biashara na huduma. Je, trade mark ni kitu gani? Trade mark ni alama au nembo ya kipekee ambayo inatumiwa na mtu au kampuni kwenye bidhaa au huduma zake. Utumikaji wake ni lazima uwe unahusiana na bidhaa au huduma.

Lengo kuu la alama hii ni kuweza kuitofautisha na nembo zinazotumika kwenye bidhaa au huduma nyingine. Umiliki wa nembo hiyo utamfanya mmiliki wa nembo hiyo kuwa na uhalali na mamlaka ya kutumia nembo au alama hiyo katika huduma au bidhaa zake na kutoa utambulisho pindi inapoonekana au kutumika kwenye bidhaa au huduma fulani.

Katika makala hii neno TM litatumika kama kifupisho cha Trade Mark au nembo ya kipekee pale inapobidi.

Kwa Tanzania mambo yote yanayohusu nembo za biashara linasimamiwa na sheria zifuatazo:

  •  The Trade and Services Marks Act Cap 326 R.E 2002 (Sheria ya Nembo za huduma na biashara ya mwaka 2002)
  • The Trade and Service Marks Regulations, Government Notice No.40 of 2002 (Kanuni za Nembo za biashara na Huduma za mwaka 2002)
  • The Zanzibar Industry Property, Act of 2008 (Sheria ya mali za viwanda ya Zanzibar ya mwaka 2008)

Suala hili la trade mark sio la muungano na linasimamiwa na mamlaka mbili tofauti hivyo basi ukisajili nembo ya kipekee au trade mark Tanzania Bara unapaswa kusajili pia Tanzania Visiwani. Kwa maana nyepesi nembo ambayo imesajiliwa Tanzania Bara haitakua na ulinzi wa kisheria Zanzibar.

Nembo au alama ambayo inatakiwa kusajiliwa lazima iwe inaonekana. Hii inamaanisha kuwa nembo hiyo inaweza kuwa alama, maneno, herufi au namba. TM ili isajiliwe lazima iwe ya muonekano wa kipekee. Muonekano huo utaweza kuifanya iwe tofauti na nembo zingine ambazo zinatumika kwenye biashara zingine au huduma. Muonekano wa nembo yako lazima uweze kutofautishwa na nyingine. Lengo kuu ni kuweza kuhakikisha walaji wa kawaida hawababaishwi na muonekano wa nembo hiyo.

Kwa sasa usajili wa nembo unafanyika mtandaoni kupitia mfumo wa usajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA Online Registration System”.

Kupitia njia hii ya mtandao unaweza kusajili kwa urahisi sana nembo yako. Ni vyema ukatumia wakili mbobevu wakati wa usajili ili aweze kufanya mambo kiweledi kwa sababu suala la nembo ni suala nyeti sana katika nyanja za biashara na huduma.


Vitu vya kuzingatia wakati wa usajili

Muombaji au muwakilishi wa muomboji anapaswa kuwa na vitu au nyaraka zifuatazo wakati wa kufanya usajili au kutuma maombi ya usajili:-

(a)Anuani ya makazi na taarifa za mmiliki wa nembo hiyo, utaifa, kama mmiliki ni partnership (Ushirika) au company (kampuni) na taarifa za kampuni au ushirika.

(b)Kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa (NIDA)

(c) Nembo au logo ya TM na rangi zake ambazo zitatumika

(d)Huduma au bidhaa ambayo nembo hiyo itatumika baada ya usajili unaoombwa

(e)Orodha ya bidhaa au huduma ambazo nembo hiyo itatumika.

(f)Tamko kwamba nembo hiyo itatumika kwa huduma au bidhaa ndani ya Tanzania.


Nani anaweza kufanya usajili?

Kwa mujibu wa sheria ya TM inatamka wazi kuwa zoezi zima la usajili litafanywa na wakala. Hivyo basi muoambaji anatakiw akumchagua wakal ambaye atafanya kazi ya usajili wa nembo hiyo. Wakala anatakiwa kufanya usajili akiambatanisha na fomu No TM/SM1 kwa mujibu kifungu cha 11 cha Trade and Service Marks Regulations za 2002.

Kifungu cha 13 Trade and Service Marks regulation ya 2002 kimeweka sifa zifuatazo za mtu kuwa wakala;

(a) Mtanzania

(b) Wakili wa Mahakama Kuu

(c) Mtu aliyeidhinishwa na Msajili baada ya kufaulu mitihani maalumu

(d) Mtu mwenye makazi Tanzania au anayefanya shughuli zake Tanzania

(e) Mwanachama wa taasisi wa mawakala wa nembo za huduma na bidhaa


Umuhimu wa nembo ya kipekee au trade mark

Usajili wa TM ni muhimu sana na una faida nyingi kibiashara na kihuduma. Zifuatazo ni baadhi tu ya faida hizo:-

(a) Mmiliki kulindwa kisheria na ndiyo faida kubwa sana anayoweza kuipata mmiliki wa TM.

(b) Mmiliki kuwa na haki ya kuitumia nembo yake kwa huduma au bidhaa.


Itaendelea wiki ijayo. 

Hamza Yusufu Lule ni Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini. Kwa msaada wa kisheria wasiliana nami kupitiaTwiter@Hamzaalbhani. Simu: 0717521700. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW