Fahamu faida za kutunza mikoko

July 31, 2024 4:50 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kupunguza hewa ya ukaa na kuchochea ongezeko la samaki.

Dar es salaam. Huenda umeshawahi kuona mkusanyiko wa miti au vichaka kando ya fukwe za bahari na ukawa unajiuliza ni aina gani ya miti, kama ulikuwa hufahamu miti hiyo ndiyo huitwa mikoko.

Kwa mujibu wa Frank Sima, Mhifadhi Mkuu wa Mikoko na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), mikoko ni miti yote ambayo huota katika makutano ya maji chumvi na maji baridi yanayotoka katika mikondo ya mito.

Sima anabainisha kuwa kuna zaidi ya aina 70 za mikoko duniani kote ambako kati ya hizo aina 10 zipo Tanzania Bara na Zanzibar.

Chanzo cha kupunguza hewa ukaa

Mikoko inatajwa kama miongoni mwa mimea muhimu zaidi duniani ambapo kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) unabainisha kuwa kila hekta moja  ya msitu wa mikoko inakadiriwa kuwakilisha dola za Marekani kati ya elfu 33 na 57,000 kwa mwaka ambazo ni sawa na Sh 89 milioni hadi Sh 153.7 milioni za Tanzania.

Aidha, UNEP wanabainisha kuwa mikoko inasaidia kufyonza na kupunguza kiwango cha hewa ukaa inayozalishwa kwa kiwango kikubwa na viwanda pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu.

Sima aliyekuwa akizungumza na Azam TV katika kipindi cha Morning Trumpet Julai 26, 2024 alibainisha kuwa mikoko ina uwezo wa kufyonza hewa ya ukaa mara nne zaidi ya misitu ya kawaida.

“Mikoko ina uwezo wa kufyonza hewa ya ukaa katika anga mara nyingi zaidi kuliko misitu ya kawaida, kwa mfano misitu ya Amazon ambayo ndio mikubwa zaidi duniani inazidiwa kupunguza hewa ya ukaa na mikoko mara nne zaidi,” alibainisha Sima.

Huchochea ongezeko la samaki

Said Mohamed, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira Kisiwa cha Kwale kilichopo mkoani Pwani, ameiambia Nukta Habari kuwa mikoko huchochea ongezeko la samaki kwa kuwa hutumika kama sehemu ya mazalia ya samaki jambo linalochochea uwepo wa viumbe hao muhimu kwa sekta mbalimbali ikiwemo uvuvi.

Hupunguza mmomonyoko wa udongo

Kwa mujibu wa Sima, kwa kiasi kikubwa mikoko huwa kama ngao dhidi ya athari za mmomonyoko wa udongo kwa kuwa huzuia mawimbi ya maji kuathiri nchi kavu pamoja na kupunguza kasi ya upepo.

“Ufukwe wa Tanzania Bara na Zanzibar ambao una urefu wa kilomita 1,400 kilomita 800 zimefunikwa na mikoko, hii inakupa tafsiri kwamba mikoko inazuia madhara yatokanayo na mmomonyoko wa maji ya bahari pamoja na upepo mkali unaotoka Kaskazini na upepo wa Kusini,” amebainisha Sima.

Kwa kutambua umuhimu wa mikoko duniani Umoja wa Mataifa ulitangaza kila ifikapo Julai 26, kila mwaka kuadhimishwa kwa siku ya mikoko kwa dhumuni la kukumbushana kuhusu umuhimu wa mimea hiyo kwa ikolojia na ustawi wa ulimwengu.

Aidha, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuwa mwaka 2021 hadi 2030 kama Muongo wa UN wa Kuboresha Mifumo ya Ikolojia

Muongo huo unaoongozwa na UNEP pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ulibuniwa ili kuzuia, kukomesha na kukabiliana na uharibifu wa mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni.  

Enable Notifications OK No thanks