Fahamu chanzo na namna unavyoweza kutibu ‘kikwapa sugu’

January 31, 2023 11:51 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuoga mara kwa mara pamoja na kunyoa vinyweleo maeneo ya kwapani.
  • Kutumia vidhibiti harufu (vipodozi) nako kwatajwa.

Dar es salaam. Bila shaka inatia aibu na unyonge wakati fulani pale unapoambiwa unanuka kikwapa, au unapobaini sehemu ya nguo yako pendwa imebadilika rangi kutokana na jasho linalotoka sehemu ya kwapa.

Ingawa baadhi ya watu huhusianisha kikwapa na uchafu lakini wapo baadhi ya watu ambao hata baada ya kujisafi na kutumia manukato bado kikwapa kiko pale pale.

Kama wewe ni miongoni mwao usijari. Makala haya yanaangazia  chanzo cha kikwapa na njia mbalimbali unazoweza kutumia ili kuepukana na kadhia hiyo.


Jasho ndio chanzo

Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya tiba ya Medical News Today (MNT) ya nchini Uingereza, mwili wa binadamu una tezi zaidi ya milioni 2 ambazo kazi yake ni kutoa jasho ili kuupoza mwili.

Mwili hutoa jasho pale joto la mwili linapoongezeka. Mfano mtu anapofanya mazoezi, anapotembea eneo lenye joto hususan juani na baadhi ya watu hutokwa na jasho wakiwa na hasira au wasiwasi.

Kelvin Lotti ambaye ni Daktari kutoka zahanati ya Arafa iliyopo Mbezi Kibamba jijini Dar es Salaam anasema kwa kawaida  mwili  hutoa jasho  ambalo halina harufu, ila harufu hutokea mara baada ya jasho  kukutana na bakteria ambao huanza kuchakata jasho hilo.

“Harufu husababishwa na hawa bakteria ambao tunawaita normal flora (bakteria rafiki kwa binadamu) ambao hupatikana katika ngozi zetu, jasho linapotoka huanza kuvunja vunja kemikali zilizopo kwenye jasho na hapo ndipo harufu hutokea,” anasema Dk Lotti.


Njia za kuepuka kikwapa

Kuoga

Mtu anayesumbuliwa na tatizo la kikwapa anashauriwa kuoga mara kwa mara kwa kutumia sabuni za kuondoa harufu na kuhakikisha anajikausha vizuri eneo la kwapa mara baada ya kuoga.

Kunyoa kwapani ni miongoni mwa njia itakayokusaidia kupunguza harufu. Picha l Popsugar .

Kunyoa kwapani

Kwa mujibu wa Dk Lotti, vinyweleo vinapokuwa vingi katika eneo la kwapa vinawapa nafasi bakteria kutumia muda mwingi kuvunja vunja kemikali na hivyo harufu inakaa kwa muda mrefu zaidi.

Mtu mwenye mwenye tatizo hilo anashauriwa kunyoa vinyweleo vya kwapani muda wote ili kuepusha kwapa kuwa na unyevu muda mwingi.


Kutumia vidhibiti harufu (vipodozi)

Kwa mujibu wa tovuti ya MNT, vidhibiti harufu vimegawanyika katika makundi mawili perspirants (dawa) pamoja na deodorant (vipodozi) ambavyo vyote husaidia kukabiliana na harufu ya kikwapa.

Antiperspirants huziba vitundu vya jasho kwa muda na kupunguza kutoka jasho kwa wingi. Kwa mujibu wa MNT hii huwafaa wale ambao wanakabiliwa na kutokwa na jasho muda wote hata joto la mwili lisipongezeka.

Deodorant hufanya kazi ya kubadili jasho kuwa asidi na hivyo kuwazuia bakteria kuchakata na jambo ambalo husababisha harufu isizalishwe.


Kuzingatia ulaji wa vyakula

Ndio! , baadhi ya vyakula husababisha jasho  kuzalishwa kwa wingi kutokana na aina ya virutubisho ambavyo huwa navyo. Vyakula vilivyotajwa na tovuti ya afya ya healh.com ya nchini Marekani ni pamoja na vitunguu, tangawizi, nyama pombe na samaki hivyo inashauriwa kula kwa kiasi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW