Dk Tulia achaguliwa Spika mpya wa Bunge la Tanzania

February 1, 2022 1:50 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson. Picha| Mtandao.


  • Apata kura kati zote 376 zilizopigwa na wabunge
  • Awabagwa wagombea wenzake tisa.
  • Anachukua nafasi ya Job Ndugai aliyejiuzulu. 

Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amechaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania baada ya kupata kura 376 kati ya 376 zilizopigwa na Wabunge sawa na asilimia 100. 

Amewabwaga wagombea wenzake nane ambao alikuwa akichuana nao ambapo hakuna hata mmoja aliyepata hata kura moja. 

Dk Tulia ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini alikuwa akichuana na wagombea wengine nane: Abdullah Mohamed Said kutoka chama cha NRA,  Injinia Ivan Maganza (TLP), David Mwaijojele (CCK), Georgies Busungu (ADA-TADEA) na Kunje Ngombale Mwiru kutoka chama cha SAU.

Wengine ni Maimuna Said Kassim (ADC), Ndonge Said Ndonge (AAFP), Saidun Abdallahman Khatib kutoka chama cha DP.

Uchaguzi huo umefanyika leo Februari Mosi 2022 jijini Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wa uchaguzi, Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi ambaye amepitishwa na wabunge kuongoza uchaguzi huo.

Tulia ambaye alipitishwa na chama chake cha CCM kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, anachukua nafasi ya Job Ndugai ambaye alijiuzulu Januari 6 mwaka huu.

Ndugai alijiuzulu baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa watu mbalimbali la kumtaka kujiuzulu kutokana na kauli yake iliyokosoa uamuzi wa Serikali kukopa zaidi mikopo kugharamia miradi ya maendeleo.

Mara baada ya kuchaguliwa, Spika Tulia ameapa mbele ya Bunge na kutia saini nyaraka muhimu.

2010-2015

Kwa kuchaguliwa huko, Dk Tulia anakuwa Spika wa pili mwanamke kushika wadhifa huo baada ya Spika Anne Makinda aliyehudumu kati ya Novemba 2010 hadi Novemba 2015. 


Soma zaidi:

Uchaguzi wa Spika waendelea bungeni Dodoma


Atoa ahadi kuisimamia Serikali

Dk Tulia ambaye ni mwanasheria kitaaluma amesema Bunge na wabunge ni daraja ambalo linatakiwa kuhakikisha Serikali inapeleka maendeleo kwa wananchi, pia linatakiwa kutumika  kuhakikisha halikwamishi shughuli za Serikali.

Amesema katika uongozi wake hatakubali  Bunge kuendeshwa kinyonge na atahakikisha linatimiza wajibu wake kikamilifu. 

“Mkinipa ridhaa ya Uspika nitahakikisha tunaisimamia Serikali ili kutekeleza wajibu wake wa kuwaletea wananchi Maendeleo,” amesema Tulia ambaye anakuwa Spika wa 8 wa Bunge la Tanzania. 

Amewashukuru Wabunge kwa kumchagua kwa kura zote 376 na wote waliofanikisha mchakato wa uchaguzi wa uspika kikiwemo chama chake cha CCM kumteua kama mgombea pekee katika nafasi hiyo.

“Naomba mpokee shukrani zangu za dhati kwa kunipa kura za kishindo zilizoniwezesha kupata heshima hii kubwa ya Spika. Imani mliyoniwezesha itakuwa chachu ya utendaji wangu katika kulitumikia na kuliongoza Bunge letu.

“Kama tulivyoshikamana leo basi tuendelee kushikamana katika kuwatumikia wananchi wenzetu na kusimamia maslahi ya Taifa letu,” amesema Spika Tulia. 

Amesema mafanikio aliyoyapa mpaka kufikia kuwa Spika yamechangiwa na watu wengi wakiwemo wazazi, viongozi wa Serikali na chama.

“Mheshimiwa Spika Ndugai alinifunza mengi, alinielekeza, alinishauri na aliniongoza vizuri kama mbunge na kama msaidizi wake katika uendeshaji wa Bunge letu,” amesema na kubainisha alimpa fursa mbalimbali ambazo zililenga kuboresha utendaji wake.

Awali Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi  amesema baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa Spika, hatua itakayofuata ni kumchagua Naibu Spika baada Dk Tulia kujiuzulu nafasi hiyo. 

Enable Notifications OK No thanks