Uchaguzi wa Spika waendelea bungeni Dodoma

February 1, 2022 6:50 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wagombea tisa waanza kunadi sera mbele ya Wabunge.

Dar es Salaam. Wagombea tisa wameanza kunadi sera zao mbele ya Wabunge wa Bunge la Tanzania ili kupata fursa ya kuchaguliwa katika nafasi ya spika iliyoachwa wazi baada ya Job Ndugai kujiuzulu mwezi uliopita.

Ndugai alijiuzulu baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa watu mbalimbali la kumtaka kujiuzulu kutokana na kauli yake iliyokosoa uamuzi wa Serikali kukopa zaidi mikopo kugharamia miradi ya maendeleo.

Uchaguzi huo unafanyika leo Februari 1, 2022 bungeni jijini Dodoma. 

Wagombea wanaogombea nafasi hiyo ni Abdullah Mohamed Said kutoka chama cha NRA,  Injinia Ivan Maganza (TLP), David Mwaijojele (CCK), Georgies Busungu (ADA-TADEA) na Kunje Ngombale Mwiru kutoka chama cha SAU.

Wengine ni Maimuna Said Kassim (ADC), Ndonge Said Ndonge (AAFP), Saidun Abdallahman Khatib (DP) na Dk Tulia Ackson kutoka CCM.

Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi  amesema wagombea wote tisa wamekidhi vigezo vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kanuni za kudumu za Bunge toleo la mwaka Juni 2020

Amesema utaratibu wa uchaguzi huo wa spika unahusisha kila mgombea kufika mbele ya wabunge ili kujieleza na kuulizwa na kujibu maswali kama yatakuwepo pamoja na kuomba kura.

Baada ya zoezi hilo kukamilika, kila Mbunge atapewa karatasi ya kura yenye majina ya wahusika na atatakiwa kumpigia kura mgombea mmoja tu kwa kuweka alama ya vema pembeni ya jina lae. 

Mgombea atakuwa amechaguliwa kuwa spika endapo atapata zaidi ya nusu ya kura za wabunge wote.

Tayari wagombea wote wameanza kunadi sera zao mbele ya Wabunge.

Enable Notifications OK No thanks