Dk Mabula awaonya wanaobadili matumizi ya hati za ardhi
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula (Kulia) akigawa hati za ardhi kwa wakazi wa Halmashauri ya Ilemela mkoani Mwanza. Picha | Mariam John.
- Asema zinaharibu muonekano wa miji na mipango yake.
- Awaonya wenye tabia hiyo kuwa watachukuliwa hatua.
Mwanza. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amewataka wananchi wanaokabidhiwa hati miliki za ardhi kuhakikisha wanazingatia masharti yaliyopo kwenye hati hizo na kufuata mipango kabambe ya maeneo husika ikiwemo kutobadili matumizi ya hati hizo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hati 570 kwa wakazi wa kata ya Shibula wilayani Ilemela katika Mkoa wa Mwanza, Waziri Mabula amesema ipo tabia ya baadhi ya wananchi wanaaomba hati hizo kubadilisha matumizi, kitu ambacho hakikubaliki.
“Huwezi kupata hati leo, kesho unaenda kubadili matumizi mwisho wake miji inaonekana haina maana na haipendezi na sisi tunataka jiji la Mwanza na Ilemela iwe ya mfano,” amesema Dk Mabula.
Waziri huyo amewetaka watendaji wa sekta ya ardhi na uongozi wa Serikali wasimamie matumizi sahihi ya hati hizo na kuzuia kila namna ya kubadili kwa matumizi.
Hata hivyo, Waziri huyo ameshtushwa na idadi ndogo ya wamiliki waliojitokeza kuchukua hati ambao ni 50 kati 570 wenye hati hizo.
Amewataka wamiliki wa ardhi walioshindwa kuchukua hati kuandaliwa utaratibu maalumu wa kupatiwa hati hizo na kuitaka idara ya ardhi katika Halmashauri ya Ilemela kwa kushirikiana na ofisi ya Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza kuchagua sehemu moja na kutumia wiki mbili kutoa hati hizo kwa wahusika ili ziishe na kuendelea mchakato wa hati nyingine.
“Watu tuna tabia ya kulalamikia hati hazitoki hapa tuna hati 570 lakini waliojitokeza ni 50 tu wengine wako wapi? Ni kitu ambacho hakieleweki hati zinaandaliwa lakini hawaji kuchukua naomba zile zinazobaki muangalie namna mtakavyotoa,” amesema Dk Mabula.
Hezroni Simon ni mkazi wa kata hiyo amesema ana furaha kwa kuwa amekuwa akifuatilia hati hiyo kwa muda wa miezi sita sasa lakini hatimaye leo ameipata.
“Nimekuwa nikifuatilia hati kwa muda mrefu lakini leo nimefanikiwa kupata hati yangu ambayo itanisaidia katika kulinda eneo langu lakini ni mtaji ambapo naweza kuitumia katika kupata mikopo kwenye taasisi za kibenki,” amesema Simon.