Dk Kilahama: TRA iweke kipaumbele zaidi elimu kwa mlipa kodi

April 13, 2019 10:54 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Elimu ya kulipa kodi iwe kwa wote na TRA kuweni rafiki na mlipakodi na kwa lugha inayohamasisha kulipa kodi.
  • Tunapolipa kodi tena kwa wakati muafaka, Serikali itatekeleza shughuli zake ikiwemo kulipa mishahara kwa watumishi wa umma.

Nina kila sababu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema mengi anayotujalia ikiwa ni pamoja na zawadi ya uhai. Kadhalika nipongeze Wajumbe wa Bodi, Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Kodi nchini (TRA) kwa juhudi zinazofanyika kutimiza wajibu wao.

Ukusanyaji kodi ni jukumu muhimu kwa ajili ya maendeleo yetu na Taifa kwa ujumla. Nikiri kwamba wengi hatuifahamu vizuri sheria zinazosimamia ulipaji kodi.

Isitoshe tumerithi mfumo wa wakoloni na utaratibu wa kuziandika sheria kwa lugha ya Kiingereza kiasi kwamba kuzitafsiri inakuwa vigumu sana. Hivyo suala la kulipa kodi bila kuifahamu na kuielewa vizuri sheria husika ni shida sana jambo linalofanya baadhi yetu kuona kama tunaonewa.

Elimu kwa mlipa kodi ni suala muhimu sana kwa Tanzania, wakati huu ambao nchi ipo kwenye harakati za kujiletea maendeleo endelevu kupitia rasilimali kama madini, wanyamapori, misitu, ardhi-kilimo na ufugaji bila kusahau rasilimali watu.

Ili yote haya yawe ya manufaa kwa Taifa, usimamizi na uelewa kwa wananchi uwe wa hali ya juu na kwa viwango vya kuridhisha. Inapotokea kuwa usimamizi unasuasua matokeo hayatakuwa mazuri.

Vivyo hivyo kama uelewa ni mdogo na kiwango cha elimu kikawa chini, matokeo hayataridhisha na badala yake ni kulalamika kwa mtazamo kuwa haki haitendeki.  Kwa sasa hali ndivyo ilivyo kwa upande wa kulipa kodi.

Sehemu nyingi ninazojaliwa kutembelea ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam wengi tunalalamika kuwa maisha ni magumu sana na wajasiliamali wadogo pamoja na wakulima wanalazimishwa kulipa tozo kwa shughuli wanazofanya au kulipa ushuru wa mazao. 

Hili linaonekana kuwa ni kero kubwa kwa Watanzania na kulazimu hatua za kisiasa zichukuliwe.

Baada ya kuona malalamiko ni mengi kupita maelezo ndipo Mheshimiwa Rais Dk John Magufuli akachukua maamuzi ili kupunguza malalamiko. Kwanza, kwa kutoa agizo kuwa kwa mkulima anayepeleka mazao yake sokoni yasiyozidi uzito wa tani moja asilipe ushuru wala kubughudhiwa na mtu yeyote. 

Kwa maana hiyo, awe na uhuru na amani anapopeleka mkungu wake mmoja, miwili au mitatu ya  ndizi sokoni auze na apate fedha kidogo za kujikimu.

Pili, kuhusu wajasiriamali wadogo mapato chini ya Sh4 milioni kwa mwaka, Rais Magufuli aliagiza wasisumbuliwe iwapo mamlaka husika hazijaweka utaratibu mzuri unaokubalika kuhusu wapi au mahali pa kufanyia shughuli zao ili maisha yasonge mbele kama kawaida bila kuathirika kisaikolojia na kimapato. Kadhalika, alichukua hatua zaidi kwa kuwapatia vitambulisho kwa gharama yaSh20,000 ambavyo baadhi ya mikoa inaendelea kuvigawa japo kwa kusuasua.

Foleni katika barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam imepungua baada ya Serikali kuruhusu kutumika kwa barabara ya juu (flyover) katika eneo la Tazara. Picha|Mtandao.

Pamoja na Serikali kuchukua hatua kama hizo kwa maslahi ya waliowengi bado kuna haja kubwa ya kutoa elimu na kufanya uhamasishaji endelevu kwa Watanzania juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa faida ya maendeleo yetu.

Kwa nini nasema hivyo? Hii ni kutokana na ukweli kwamba Serikali na shughuli zake huendeshwa kwa kupata fedha kutokana na kodi au mikopo ambayo itarejeshwa kupitia mapato ambayo kwa kiasi kikubwa ni kutokana na kodi.

Tunapolipa kodi tena kwa wakati muafaka, Serikali itatekeleza shughuli zake ikiwemo kulipa mishahara kwa watumishi wa umma. Shughuli zote za kutengeneza na kukarabati miundombinu iwe ni barabara, madaraja, kuzalisha na kusambaza umeme, mitaro/mifereji ya umwagiliaji na kadhalika ni wajibu wa Serikali.

Pamoja na Serikali kutekeleza masuala muhimu kama hayo, inabidi pia itoe huduma muhimu kwa jamii za elimu, afya, maji, kilimo na ufugaji kama kuweka miundombinu ya majosho, kusambaza pembejeo na huduma za ugani. Mahitaji yote hayo yanahitaji Serikali kuwa na fedha nyingi kuweza kutimiza malengo ya Taifa.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, Watanzania wameanza kuona umuhimu wa kulipa kodi ingawa wengi bado tunalalamikia suala hili. Inawezekana malalamiko yetu ni sahihi au inakuwa hivyo kwa kukosa uelewa mzuri na kutopata miongozo sahihi ili kuondoa mawazo potofu ya kwa nini tulipe kodi wakati Serikali ni wajibu wake kutekeleza yote kwa niaba yetu.

Baadhi yetu tunadhani kuwa Serikali itatoa huduma tunazopata bila kuiwezesha kupitia kodi na tozo mbalimbali.  Badala yake tunailalamikia na kuona tunaonewa tunapotakiwa kufanya hivyo. Kwa mathalani, suala la wajasiriamali wadogo kupewa vitambulisho kupitia TRA linaonekana ni kuwatoza kodi na unyanyasaji.

Iwapo mjasiriamali mwenye kipato kisichozidi Sh5 milioni kwa mwaka akielewa vizuri kuwa Sh20,000 anazotozwa kwa ajili ya kitambulisho zitasaida Serikali kuboresha maisha ya waliowengi kwa kuimarisha miundombinu na kutekeleza majukumu mengine, itakuwa jambo la kheri kuwa hata wenye kipato kidogo wanachangia maendeleo ya Taifa letu.

Tozo ya Sh20,000 kwa mwaka ni sawa na kutoa takriban Sh60 kwa siku hivyo Watanzania tuchangie maendeleo yetu bila kutegemea misaada.

Nitoe rai kwa TRA kwamba kitengo cha elimu kwa umma na mlipakodi kiimarishwe na kifanye kazi ipasavyo. Watanzania waelimishwe umuhimu wa kulipa kodi na faida zake. Sasa ni wakati muafaka kwa TRA na vyombo vingine vya Serikali kufanya hivyo kwa faida ya wote.

Hakuna sababu Wafanyabiashara kukataa kutumia mashine za EFD, ni kutofahamu vizuri faida zake kwa Watanzania. Inashangaza unaponunua lakini ukapewa bidhaa bila risiti na ukauliza mbona hunipi risiti mhusika anakuangalia kama wewe ni mtu wa ajabu. Ndipo anapokurupuka na kusema “samahani nimepitiwa” wakati huo huo wanunuzi wengi wanaondoka bila matumizi ya EFD kufanyika. 

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo akitoa elimu kwa walipa kodi katika Ofisi ya TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam kuhusu kulipa kodi za mapato, majengo na kodi za ongezeko la thamani kwa wakati ili kuepuka usumbufu, riba na faini. Picha| Mtandao.

 Kwa vitendo kama hivyo tunajidanganya wenyewe kwa kuwa maisha bila miundombinu imara hayatakuwa mazuri.  Mkulima atapata faraja iwapo mazao yatauzwa akapata fedha. Miundombinu mizuri na imara itamfanya mkulima achangamkie fursa kwa kuona viwanda vya mazao (agro-processing industries) vimekuwa karibu naye. Wasafirishaji pia wanakuwepo hivyo kilimo kitamnufaisha mkulima.

Vilevile, wakazi wa mijini watanufaika kutokana na mazao ya chakula toka vijijini kusafirishwa kiurahisi na kwa ushindani kibiashara hatimaye bei za vyakula kuvutia mnunuzi.  

Elimu ya kulipa kodi iwe kwa wote na TRA kuweni rafiki na mlipakodi na kwa lugha inayohamasisha kulipa kodi. TRA kama chombo muhimu cha kuchochea maendeleo yetu, fanyeni kazi kwa bidii na kutokata tamaa. Penye nia pana njia tusonge mbele: uchumi wa viwanda ni wetu pia ni jambo linalowezekana kutokana na rasilimali tulizo nazo.

Uwepo wa elimu kwa mlipa kodi ni muhimu sana na pia tusibeze juhudi zinazoendelea za kujenga uchumi imara bila kutegemea sana misaada kutoka nje.

Dk Kilahama ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Makala haya ni maoni yake binafsi wala hayahusiani na taasisi anazoziongoza au nukta.co.tz.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW