Dereva wa basi lililoua tisa, kujeruhi, apandishwa kizimbani Mwanza
- Asomewa mashtaka 64 ikiwemo kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa miundombinu.
- Mshtakiwa arejeshwa rumande, kesi kusomwa tena Novemba 5, 2024.
Mwanza. Dereva wa basi Shedrack Swai (37) aliyesababisha ajali Oktoba 22 mwaka huu katika kijiji cha Ukiligulu, Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Misungwi na kusomewa shtaka la kuendesha gari kwa uzembe katika Barabara ya Umma lenye makosa 64 yakiwemo ya kusababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa miundombinu na mali.
Akisoma shtaka hilo katika kesi ya Trafiki namba 30855/2024, linalomkabili dereva huyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi, Esther Marick, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ramson Salehe akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Lilian Meli amesema mshtakiwa alitenda makosa hayo kinyume na Kifungu cha 41, 63 (2) (b) na 27 (1) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002.
Salehe, jana Oktoba 29, 2024 ameieleza mahakama hiyo kuwa mshakiwa anashtakiwa kwa makosa 64 yakiwemo ya kuendesha gari kwa uzembe katika barabara ya umma na kusababisha vifo vya watu tisa, kujeruhi 54 na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na miundombinu.
“Oktoba 22,2024, katika barabara ya Mwanza- Shinyanga Dereva huyo wa gari lenye namba za usajiri T. 458 DYD aina ya Yutong basi aliendesha gari hilo kwa uzembe ambapo ulilipita gari lingine bila kuchukua tahadhari na matokeo yake akaligonga gari lingine lenye namba za usajiri T. 281 EFG aina ya You tong basi na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali,” amesema Salehe
Baada ya kusomewa makosa hayo, mshtakiwa amekiri kutenda makosa hayo yote 64 huku Wakili wa Serikali Mwandamizi Lilian Meli akiiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi, Esther Marick amemweleza mshtakiwa kuwa shtaka linalomkabili linadhaminika na kumtaka kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali ya Mtaa, Kitambulisho cha Taifa (Nida) na bondi ya maneno ya Sh5 milioni kila mmoja.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana baada ya mdhamini mmoja kukosa kitambulisho halisi cha Nida hivyo mshtakiwa akarudishwa rumande katika Gereza la Butimba jijini Mwanza hadi masharti hayo yatakapokamilika
Hakimu, Esther ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 5,2024 litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali.
Dereva wa basi la Asante Rabi, Shadrack Swai(37) akipandishwa kizimbani kusomewa nmashataka yanayomkabili ya kukiuka Sheria za Usalama Barabarani .Picha na Mariam John/Nukta