Chande aeleza sababu tume kutotaja majina ripoti ya vurugu Oktoba 29

April 28, 2026 4:20 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Tume yasema ushahidi uliokusanywa ni wa pande moja.
  • Vyama vya siasa, asasi za kiraia zakosoa vikali ripoti ya uchunguzi matukio Oktoba 29. 

Dar es Salaam. Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29 imesema uamuzi wa kutotaja majina ya wanaodaiwa kuhusika katika ripoti yake ulitokana na kuzingatia sheria na haki ya kusikilizwa licha ya baadhi ya majina kutajwa na mashahidi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 28, 2026, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mohamed Chande Othman amesema ushahidi uliokusanywa na tume ulitoka upande wa waathirika pekee na haukutoa fursa kusikiliza upande wa watuhumiwa.

Aidha, amebainisha kuwa jukumu la tume lilikuwa ni kufanya uchunguzi kwa kuzingatia hadidu za rejea na kutoa mapendekezo badala ya kutoa hukumu. 

“Kuna mtu amepigwa risasi anasema ‘mimi nilikuwa dukani’. Tumeukubali ushahidi wake kwa sababu upo chini ya kiapo. Lakini sio kamilifu kwa sababu hajaojiwa kidodoso. Ukienda mahakamani unahojiwa pande mbili,” amefafanua Jaji Chande.

Hata hivyo, ameeleza kuwa ushahidi uliokusanywa unatosha kuendelea na hatua inayofuata endapo tume nyingine itaundwa kwa ajili ya uchunguzi wa jinai.

“Ushahidi upo, waliopigwa risasi nje ya maeneo ya ghasia, upo, wengine wamesema wamepigwa sebuleni. Na ndio maana kuna mapendekezo tumewasilisha” amefafanua Jaji Chande.

Mkutano wa Jaji Chande na wanahabari, unakuja ikiwa ni siku tano tangu tume hiyo kukabidhi ripoti kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan baada ya siku 153 tangu ilipoanza kazi yake Novemba 20, 2025.

Tangu kuwasilishwa kwake, ripoti hiyo imepokea ukosoaji mkubwa kutoka kwa wananchi, asasi za kiraia  pamoja na vyama vya siasa.

Aprili 27, 2026, asasi za kiraia 14 zinazotetea masuala ya haki za binadamu na utawala bora nchini ikiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) zilieleza kubaini kasoro katika ripoti ya Jaji Chande.

Katika tamko lao, asasi hizo zinadai kuwa ripoti ya Jaji Chande ina udhaifu katika ukusanyaji wa taarifa za uchunguzi na kudai kuwa tume ilisita kuwataja Watanzania waliohusika katika machafuko hayo.

Kasoro nyingine zilizotolewa ni pamoja tume kushindwa kueleza mazingira ambayo mafunzo ya kufanyika vurugu yaliratibiwa kufuatia madai ya uwepo wa makambi na mafunzo kwenye ripoti ya tume.

Teknolojia iliwaweka waratibu mbele ya muda

Akitoa ufafanuzi kuhusu namna tume ilivyojiridhisha kuwa matukio hayo yalipangwa, pamoja na sababu za vyombo vya ulinzi na usalama kushindwa kuyadhibiti mapema, IGP mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa tume hiyo, Said Ally Mwema amesema mabadiliko ya teknolojia ni miongoni mwa sababu zilizochangia vyombo vya usalama kushindwa kudhibiti matukio hayo mapema.

Mwema amefafanua kuwa, tofauti na zamani ambapo watu ilibidi wakutane ana kwa ana kupanga au kujadili masuala matukio yaliyotokea yaliratibiwa kwa mtandao jambo lilofanya vyombo vya usalama kuzidiwa kete.

“Mbinu walizotumia ni tofauti na mbinu za kawaida… fujo zilikuwa zinasambaa kwa haraka sana na kutawanyika maeneo mengi kiasi kwamba kuzuia ikawa ngumu,” amefafanua Mwema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
BALOZI JAMES: Hakuna mtanzania aliyeshambuliwa Afrika Kusini

BALOZI JAMES: Hakuna mtanzania aliyeshambuliwa Afrika Kusini

Nukta TV

🔴LIVE: TUME YA UCHUNGUZI MATUKIO OKTOBA 29, USO KWA USO NA WAANDISHI WA HABARI

🔴LIVE: TUME YA UCHUNGUZI MATUKIO OKTOBA 29, USO KWA USO NA WAANDISHI WA HABARI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI WIZARA YA KILIMO IKIWASILISHWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI WIZARA YA KILIMO IKIWASILISHWA BUNGENI

Nukta TV