Burundi, Tanzania zasaini makubaliano ujenzi reli ya kisasa
- Itagharimu zaidi ya Sh1 trilioni na itakuwa na urefu wa kilomita 282.
- Itaunganisha kipande cha Uvinza – Malagarasi na Musongati – Gitega nchini Burundi.
- Reli hiyo itarahisisha shughuli za biashara na ugavi katika nchi hizo.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Burundi zimetia saini za makubaliano ya awali ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa (SGR) kutoka Uvinza Tanzania hadi Gitega, Burundi yenye urefu wa kilomita 282.
Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania mkoani Kigoma.
Serikali ya Burundi imewakilishwa na Waziri wa Miundombinu, Ujenzi na Makazi, Dk Deogratius Nsanganiyumwami na Waziri wa Fedha, Bajeti na Mipango ya Uchumi Dk Domitien Ndihokubwayoi.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha inaeleza kuwa, gharama za mradi huo zitatolewa baada ya kukamilika kwa taarifa za kihandisi lakini inakadiriwa kuwa hazitazidi Dola za Marekani milioni 900 (takriban Sh 2.1 trilioni).
Dk Nchemba amesema, Serikali ya Tanzania na Burundi zimeanza kuangalia maeneo ambayo watapata fedha za kutekeleza mradi huo.
“Mimi na Waziri wa Fedha wa Burundi tunaanza kuangalia maeneo ambayo tunadhani tunaweza kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu, tutawaambia Watanzania, Warundi na maeneo mengine yatakayonufaika na reli hii kiuchumi kuwa fedha zitapatikana,” amesema Dk Nchemba.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (wakwanza kulia), Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba (wa pili kulia) wakiwa na Waziri wa Miundombinu, Ujenzi na Makazi, Dkt. Deogratius Nsanganiyumwami pamoja na Waziri wa Fedha, Bajeti na Mipango ya Uchumi, Dkt. Domitien Ndihokubwayo (kushoto) wa Burundi, wakitia saini za awali za makubaliano ya pamoja ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR). Picha Wizara ya Fedha na Mipango.
Ujenzi wa reli hiyo ni muendelezo wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na kisha Kigoma itakayounganisha nchi za maziwa makuu ikiwemo Burundi na Rwanda.
Lengo la reli hiyo ni kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji nchini ususani sekta ya reli ambapo itabeba mzigo wa mpaka tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa maroli 500 ya mizigo na kuokoa muda wa usafirishaji abiria na mizigo.
Pia itachangia katika ongezeko la ajira kwa wazawa katika sekta na fani mbalimbali na uboreshaji wa huduma za kijamii ikihusisha ujenzi wa shule, vituo vya afya na ujenzi wa barabara katika maeneo yanayopitiwa na mradi huo.
Prof Mbarawa amesema reli hiyo itajengwa kwa kushirikiana na Burundi na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni huku ikikadiriwa kuwa reli hiyo itatumia treni za kisasa zenye mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa.
Reli hiyo inatarajiwa kuunganisha kipande cha Uvinza Malagarasi chenye urefu wa kilomita 156 huku Burundi ikihusika katika kuunganisha kipande cha Malagarasi hadi Musongati – Gitega chenye urefu wa kilomita 126.
Waziri huyo amesema mradi huo unanufaisha Tanzania, Burundi na Congo ambazo hutumia bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo.
“Kukamilika kwa reli kutarahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda katika nchi hizo,” amesema Prof Mbarawa.
Soma zaidi:
- Suluhu ya kuongeza ufaulu somo la hisabati Tanzania
- Mbinu zitakazowasaidia wahudumu kuvuta wateja wengi mgahawani
- Mwanafunzi bora kidato cha nne 2021 ataja siri za ushindi
Waziri Nsanganiyumwami na Waziri Dk Ndihokubwayo wamesema Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi, Jenerali Evariste Ndayishimiye walikubaliana kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo ujikite pia katika masuala ya kiuchumi.
Utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika kufungua nchi hizo kiuchumi.
Mawaziri hao wamesema reli hiyo itasaidia kusafirisha takribani tani zaidi ya milioni 1 za mizigo na madini zaidi ya tani milioni 3 kutoka Burundi kupitia reli hiyo na itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuchochea ukuaji wa viwanda, kilimo na uchumi kwa ujumla.
Latest
