BMW yafichua magari mapya yanayoweza kubadilika rangi
- Rangi hizo za kuelektroniki hulifanya gari kuwa na mwonekano wa kipekee.
- Lengo ni kumuunganisha kihisia dereva na gari kwa kutumia dijiti.
Dar es Salaam. Kampuni maarufu ya utengenezaji wa magari ya BMW ya Ujerumani imefichua teknolojia yake mpya itakayomwezesha dereva kubadili rangi ya gari lake kama kinyonga ili kukipatia muonekano tofauti kifaa hicho cha usafiri.
BMW imetambulisha teknolojia hiyo ya “BMW i Vision Dee” kwenye maonyesho ya biashara ya teknolojia ya CES 2023 huko Las Vegas, Marekani.
Teknolojia hiyo iliyotambulishwa Januari 5, 2023 imeundwa kuwezesha paneli 240 tofauti za wino za kielektroniki kwenye mwili wa gari, kuwawezesha madereva kubadilisha mwonekano usio na kikomo wa nje wa gari kwa sekunde.
Jina “Dee” linawakilisha uzoefu wa kihisia dijiti yaani kuunda uhusiano wenye nguvu zaidi kati ya watu na magari yao.
“Kwa BMW i Vision Dee, tunaonyesha kile kinachowezekana wakati mundo (Hardware) na programu vinapounganishwa. Kwa njia hii, tunaweza kutumia uwezo kamili wa ujanibishaji wa kidijitali ili kubadilisha gari kuwa mwonekano dhahiri,” amesema Oliver Zipse, Mwenyekiti wa kampuni ya BMW AG.
Teknolojia hiyo pia inamuwezesha dereva kubadirisha rangi za madirisha na kumpa muonekano wa kipekee wakati akitumia aiana ya magari hayo.
Lengo la kuwezesha teknolojia hiyo ni kuunganisha hisia binafsi za madereva wa gari hizo kwani zinaweza kubadilishwa mwonekano ili kuendana na mtindo, hisia au hata mavazi.
\\ hey everyone!! meet the guy that brought me here from the virtual world! // ➡️ https://t.co/gBRegHpvJP
#DEEMW
#THEiVisionDee
#TheUltimateCompanion
pic.twitter.com/32qKLBPPlV— BMW (@BMW) January 5, 2023
Hii ina maana kwamba BMW i Vision Dee inaweza kuzungumza na watu na, wakati huo huo, kueleza hisia kama vile furaha, mshangao au idhini kwa macho. Pia inaweza kuonyesha picha ya dereva kwenye dirisha la pembeni ili kubinafsisha zaidi hali ya kukaribisha.
“Tukiwa na BMW i Vision Dee, tunaonyesha jinsi gari linavyoweza kuunganisha kwa urahisi katika maisha yako ya kidijitali na kuwa mteja mwaminifu. Gari lenyewe linakuwa lango lako kwa ulimwengu wa kidijitali – huku dereva akidhibiti kila wakati,” amesema Adrian van Hooydonk, Mkuu wa Usanifu wa BMW.
“Ikitekelezwa kwa njia sahihi, teknolojia hii itaunda uzoefu mzuri, kukufanya dereva kuwa bora na kuleta wanadamu na mashine karibu,” amesisitiza Hooydonk.
Kampuni ya BMW inafanya uwekezaji wa kutengeneza magari yatumiayo nishati ya umeme na yanayoweza kuunganishwa kwenye huduma za kidijitali. BMW i Vision Dee inawakilisha kipengele cha dijitali kama hatua muhimu kwenye matoleo yajayo ya magari yaitwayo Neue Klasse.
Kampuni ya BMW itatoa maarifa zaidi na mwangaza wa dhana ya magari ya hayo mapya ya Neue Klasse wakati wowote mwaka huu 2023.
Latest
