Biashara kati ya Tanzania na nchi za SADC yazidi kupaa
- Ndani ya mwaka mmoja uuzaji wa bidhaa za Tanzania katika nchi hizo ulipaa kwa asilimia 12.
- Uingizaji wa bidhaa kutoka nchi hizo nao wapaa kiduchu kwa asilimia 0.61.
- Nchi za SADC zinazoongoza kuiuzia Tanzania bidhaa ni pamoja na Afrika Kusini, Zambia na Mauritius.
Dar es Salaam. Serikali imesema Tanzania inafanya vizuri katika biashara na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kwamba kuna fursa lukuki ambazo bado hazijatumika ipasavyo katika soko la jumuiya hiyo yenye watu zaidi ya milioni 350.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amewaeleza washiriki wa maonyesho ya nne ya viwanda ya SADC kuwa mauzo ya Tanzania katika jumuiya hiyo yalipaa kwa asilimia 12.16 ndani ya mwaka mmoja hadi Dola za Marekani 999.64 milioni (Sh2.3 trilioni) mwaka 2018 kutoka Dola za Marekani 877.8 milioni (Sh1.99 trilioni) mwaka 2017.
“Wakati huo uingizaji wa bidhaa kutoka nchi za SADC uliongezeka kidogo kutoka Dola za Marekani 600.64 milioni(Sh1.38 trilioni) mwaka 2017 hadi Dola za Marekani 604.32 milioni (Sh1.39 trilioni) ikiwa na sawa na ongezeko la asilimia 0.61,” ameeleza Bashungwa katika hafla ya uzinduzi wa maonyesho hayo yaliyozinduliwa leo (Agosti 5, 2019) na Rais John Magufuli.
Maonyesho hayo ya viwanda yanayohusisha washiriki zaidi ya 3,000 yanajumuisha waonyeshaji bidhaa na huduma 1,576 kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Viwanda na Biashara.
Soma zaidi: Maagizo matano ya Magufuli kukuza uchumi wa viwanda nchi za SADC
Baadhi ya bidhaa ambazo Tanzania imeuza katika jumuiya hiyo, kwa mujibu wa Bashungwa, ni pamoja na madini kama dhahabu na Tanzanite, bidhaa za kilimo kama chai na kahawa.
Waziri huyo ameeleza kuwa bidhaa nyingine ambazo Tanzania iliuza ni zile za viwandani zikiwemo plastiki, sigara, saruji, marumaru, na madawa na vifaa tiba.
“Bidhaa ambazo Tanzania imenunua kutoka katika nchi za SADC zinahusu magari, mbegu za mahindi, gesi, mabati, vilainishi mitambo (lubricants), bia, na sukari,” amesema Bashungwa na kuongeza kuwa bidhaa hizo nyingi zinatoka katika nchi za Afrika Kusini, Zambia, Mauritius na Malawi.
SADC ina nchi wanachama wapatao 16 wenye soko lenye jumla ya watu milioni 350.
Amesema pamoja na nchi kufanya vizuri katika jumuiya hiyo bado kuna fursa lukuki ambazo hazijatumika vizuri na kuwanufaisha Watanzania.
Latest