Barakoa maalum kitendawili kwa wanafunzi wenye uziwi Tanzania

February 12, 2022 9:30 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakosa barakoa maalum kujikinga na Uviko-19 ambazo ni tofauti na za kawaida.
  • Barakoa hizo ni zile ambazo haziathiri mafunzo darasani.
  • Serikali yasema bado inalifanyia kazi suala hilo.

Iringa. Katika Shule ya Msingi Viziwi Iringa iliyopo katika Mkoa wa Iringa walimu wanaendelea kufundisha darasani huku kukiwa na mazingira ni tulivu. 

Hakuna sauti kubwa wala kelele za wanafunzi kama ilivyozoeleka kwenye shule za wanafunzi mchanganyiko.

Katika kila mlango wa kuingilia darasani, pamewekwa ndoo ya maji na sabuni. Kila mwanafunzi anayeingia darasani hulazimika kunawa mikono yake ikiwa ni njia mojawapo ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19). 

Tofauti na shule za kawaida, ndani ya darasa la V wanafunzi wa darasa hilo wamekaa kwa mtindo wa nusu duara huku wakiwa wameachina nafasi ya zaidi ya mita moja hivi.

“Mwalimu wa viziwi unatakiwa ukae mbali kidogo na wanafunzi wako ili waweze kukuona mwili wako kwa sababu wakati wa kufundisha karibu viungo vyote vinahusika ikiwemo mikono,” anasema Logan aliyekuwa umbali wa zaidi ya mita mbili kutoka kwa wanafunzi wake.

Mwalimu huyo hajavaa barakoa na darasa analofundisha lina wanafunzi 12 tu ambao nao hawajavaa barakoa.

Hali hiyo ya kutokuvaa barakoa iko katika madarasa yote ya shule hiyo ambayo Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imepita huku walimu wakiendelea kufundisha wanafunzi bila wasiwasi.

Hata hivyo, walimu na wanafunzi hao hawavai barakoa kwa bahati mbaya.

Wanafunzi wa shule ya Msingi Viziwi Iringa wakiendelea kujifunza darasani bila kuwa na barakoa licha ya kuzingatia kukaa umbali wa walau mita moja. Picha| Daniel Samson.

Hadi sasa uongozi wa shule hiyo ya bweni yenye wanafunzi 116 unazingatia tahadhari zote za kujikinga na Corona ikiwemo kuwa na vifaa vya kunawia mikono, vitakasa mikono na kuepuka misongamano ya wanafunzi darasani. 

Pamoja na kutekeleza tahadhari hizo lakini kuna kifaa kimoja tu muhimu wanakosa barakoa maalum. 

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Alinanuswe Mwakosya anasema kutokana na aina ya ulemavu walionao wanafunzi hao wa kutokusikia, wanahitaji mawasiliano ya karibu na mwalimu hasa kumtazama usoni na anavyochezesha midomo na viungo vingine.

Ikiwa mdomo na pua ya mwalimu itafunikwa na barakoa zinazotumika sasa na wengi, itazuia wanafunzi kumuelewa anachokizungumza.

“Nikivaa mimi barakoa ya kawaida maana yake mtoto hatanielewa. Kumbuka wengi wanasoma kupitia mdomo, nikivaa barakoa nitakuwa nimepoteza mawasiliano kabisa,” anasema Mwakosya.

Amesema wanafunzi nao hawawezi kuvaa barakoa za kawaida kwa sababu mwalimu anatakiwa kuwaangalia mdomoni wanachozungumza.

Ifahamike kuwa mawasiliano ya watu wenye uviziwi hufanyika kwa kutumia lugha ya alama, sauti (licha ya kuwa hawasikii), ishara na lugha ya mwili ambayo huusisisha viungo vya mwili hasa mikono. 

Mwakosya anasema mwalimu na wanafunzi hao wanahitaji barakoa maalum ambazo hazitakuwa kikwazo kwa wao kuwasiliana ambazo Serikali ilipendekeza zitumike katika shule za viziwi.

Wanafunzi wa shule hiyo wamewekewa matanki na ndoo za kunawia mikono kila wanapoingia darasani ili kuwakinga na Uviko-19 lakini changamoto yao hawana barakoa maalum. Picha| Daniel Samson.

Mpaka sasa, shule hiyo iliyopo kata ya Mtwivila, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa haijawahi kupokea barakoa hizo maalum tangu Corona iingie Tanzania Machi 2020. 

Hata kama zitafika na kutumiwa zinaweza kuathiri ufundishaji na ujifunzaji darasani kwa sababu zitafunika baadhi viungo usoni na hivyo kutatiza mawasiliano ya mwalimu na wanafunzi, amebainisha mwalimu huyo mkuu.

Walimu wanafahamu barakoa maalum?

“Sisi tunahitaji barakoa maalum, mimi bado umaalum sijaujua kwa sababu wanasema hiyo barakoa inaziba pua, mdomo unabaki wazi. Wengine wanasema waweke kifuniko kinachoonyesha mdomo.“Shida itabaki bado haijatatulika ndiyo maana tumekaa tu hivi,” anasema Mwakosya.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa zaidi ya asilimia 5 ya watu wana matatizo ya kutokusikia ikiwemo uziwi. Ili kuwasiliana na watu hao vizuri, mtu anatakiwa kutumia vizuri mawasiliano ya mdomo, muitikio wa uso na mikono ikicheza kama lugha ya alama.

                             

Ni barakoa zipi zinawafaa viziwi?

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), watu wenye uziwi hasa wanafunzi wanaweza kukingwa na Uviko-19 kwa kuwatengenezea barakoa maalum za kitambaa ambazo zina kifuniko cha plastiki kinachoonyesha mdomo na pua.

Miongoni mwa barakoa hizo ni zile zilizobuniwa na taasisi ya Royal Woluwe ya nchini Ubelgiji na zinasambazwa katika shule na maeneo wanayoishi wenye uziwi nchini humo.

UN imesema kwa sehemu, barakoa hizo zimesaidia walemavu hao lakini utafiti unahitajika zaidi katika eneo hilo. 

Mfano wa barakoa maalum ambazo zina plastaki inayoruhusu mdomo na pua kuonekana. Barakoa kama hizo zinaweza kutumiwa na wanafunzi viziwi wakati huu wa janga la Corona. Picha| Revista Vidasana.

Ni wakati gani wanavaa barakoa?

Licha ya kuwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo, hawavai barakoa wakiwa darasani, hilo halijawazuia kutumia barakoa za kawaida hasa wanapokuwa wamemaliza vipindi na wanafanya shughuli nyingine.

“Siyo kwamba hatuvai barakoa kabisa, tukiwa huko nje tunacheza tunazivaa ili kujikinga,” anasema Stanslaus Baraka, mwanafunzi wa darasa la tano ambaye alikuwa akiongea kwa ishara na akitafsiriwa na mwalimu wake, Joshua Logan.

Pia walimu na wafanyakazi wengine shule hiyo yenye darasa la I hadi VII wameonekana wakiwa wamevaa barakoa zao wakati wakiendelea na majukumu yao isipokuwa wakati wakiwafundisha wanafunzi.

Uongozi wa shule hiyo ambayo ilianza mwaka 1993 umeeleza kuwa ugonjwa wa Uviko-19 wameupa kipaumbele cha hali ya juu kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama wakati wote.

Mwalimu Mwakosya anasema wameweka utaratibu mzuri kuhakikisha madarasani umbali wa mita moja kati ya wanafunzi unazingatiwa huku walimu wakikaa umbali walau mita mbili kutoka kwa wanafunzi.

Mkao huo, kwa mujibu wa mwalimu huyo mkuu, unapunguza uwezekano wa maambukizi kutokea kwa sababu miongozo ya wataalam wa afya inazingatiwa kikamilifu. 

Baadhi ya wanafunzi wenye uziwi shuleni hapo ambao Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imeongea nao wamesema wamepewa elimu ya jinsi ya kujikinga na Uviko-19.

“Hatuna hofu ya kupata huu ugonjwa, shule yetu ina wanafunzi wachache na kila mmoja yuko makini kuzingatia maelekezo ya walimu kujikinga ugonjwa huu,” anasema Prisca Nkwela, mwanafunzi wa darasa la V shuleni hapo. 

Pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo ya Uviko-19 tangu Machi 2020, wanafunzi wa shule hiyo wameendelea kufanya vizuri kimasomo kutokana na bidii na msaada wanaopata kutoka kwa walimu. 

Mathalan, katika matokeo mtihani wa darasa la saba mwaka 2020, wanafunzi wote 11 waliofanya mtihani huo walipata wastani B na hivyo kuwawezesha kujiunga na sekondari mwaka huu ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa, Tosamaganga na Njombe. 

Pia shule hiyo ilishika nafasi ya 1,176 kati ya shule 6, 641 kitaifa kwa kundi la shule zenye wanafunzi chini ya 40, kwa mujibu wa matokeo ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta).

Katika kila mlango wa darasa la Shule ya Msingi Viziwi Iringa kuna ndoo ya maji tiririka na sabuni kwa ajili ya walimu na wanafunzi kunawa mikono wakati wakiingia darasani. Picha| Daniel Samson.

Serikali yaendelea kusaka mwarobaini

Serikali mkoani Iringa imesema inaendelea kulifuatilia suala la kuwa na barakoa maalum kwa ajili ya watu wenye uziwi kwa sababu linahitaji utafiti ili hata zikitolewa zisiwe kikwazo katika utoaji elimu.

Afisa Elimu Maalum wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Christopher Hinju anasema suala bado liko kwenye majadiliano na shule za watu wenye  ulemavu hasa wenye uziwi.  

“Waendelee kuchukua tahadhari za kawaida ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono na kuepuka msongamano,” anasema Hinju.

 Tahadhari hizo za kiafya, anasema, zikizingatiwa zitasaidia sana kuwakinga walimu na wanafunzi wenye uziwi na Uviko-19 katika shule zao.

Hata hivyo, jitihada za kuwapata viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hazikufanikiwa kuelezea mikakati iliyopo ya kuwapatia barakoa maalum wanafunzi wenye uziwi nchini.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
5 Oct, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
5 Oct, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
WORD BANK: Tanzania haina upungufu wa ajira, changamoto tija yake

WORD BANK: Tanzania haina upungufu wa ajira, changamoto tija yake

Nukta TV

CEOs kung'oka baada ya miaka 10, BoT yarudisha mjadala

CEOs kung'oka baada ya miaka 10, BoT yarudisha mjadala

Nukta TV

Onyo la wachumi ikiwa ukomo wa miaka 10 hautoondolewa kwa CEOs wa benki

Onyo la wachumi ikiwa ukomo wa miaka 10 hautoondolewa kwa CEOs wa benki

Nukta TV