Ajira zaidi ya milioni 2 zinawasubiri wasichana wanaosoma masomo ya sayansi

April 27, 2019 9:32 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Inakadiria kuwa katika kipindi cha miaka 10 ijayo kutakuwa na ajira zaidi ya milioni 2 za teknolojia ambazo hazitajazwa kwa sababu ya ukosefu wa wataalam wa digitali.
  • Changamoto hiyo inafungua mlango kwa wasichana duniani kufaidika na fursa hiyo kwa kuongeza kasi ya kusoma masomo ya sayansi.
  • Baadhi ya wasichana wa Tanzania wameanza kuchangamkia fursa hizo kwa kubuni mifumo ya utatuzi ya kidijitali.

Dar es Salaam. Huenda wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi katika shule za sekondari na vyuo vikuu wakaboresha maisha yao, baada ya kubainika kuwepo kwa pengo la wataalam wa dijitali duniani. 

Kwa mujibu wa Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) unakadiria kuwa katika kipindi cha miaka 10 ijayo kutakuwa na ajira zaidi ya 2 milioni za teknolojia ambazo hazitajazwa kwa sababu ya ukosefu wa wataalam wa digitali.

ITU inasema changamoto za ajira zinafungua mlango kwa wasichana duniani kufaidika na fursa hiyo kwa kuongeza kasi ya kusoma masomo ya sayansi ili kujaza pengo la ajira katika sekta ya teknolojia na mawasiliano.

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Mawasiliano la ITU, Doreen Bogdan akizungumza Aprili 25, 2019 katika maadhimisha siku ya  kimataifa ya wasichana walio kwenye tasnia ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), amesema ujuzi bora wa wasichana unawapa fursa ya kuwa na nafasi za juu katika soko la ajira, mshahara mzuri na pia kuongeza uhamiaji wa kikazi.

Siku hiyo inayoadhimishwa Aprili 25 kila mwaka ni mahususi kwa ajili ya kutathmini juhudi za Umoja wa Mataifa  katika kuziba pengo la kijinsia katika ulimwengu wa kidijitali, lakini  kuhamasisha kizazi kipya cha wasichana kutafuta fursa zaidi katika tasnia ya teknolojia ya mawasiliano.


Soma zaidi:


Hata hivyo, baadhi ya wasichana nchini Tanzania wameanza kuchukua hatua muhimu kutumia mifumo ya kidijitali kutatua changamoto za jamii zao wakati huo huo wakipata kipato kwa ajili ya kuboresha maisha yao. 

Msichana Queen Mtega ametengeneza tovuti ya FundiPopote inayofanya kazi kama jukwaa linalowaunganisha mafundi wa fani mbalimbali na wateja wanaohitaji kupata huduma kutengenezewa au  kukarabatiwa vifaa vyao vya nyumbani na ofisini. 

Pamoja kuunganisha mafundi Mtega hajaacha kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter na Instagram ili kujitangaza na kumfanya aweze kujulikana na kuwafikia watu katika maeneo mbalimbali nchini..

“Vilevile kwenye tovuti ya FundiPopote tumetumia ramani za Google hivyo inakuwa rahisi kwa mteja kumpata fundi wa eneo lake na mawasiliano ya fundi huyo,” amesema Mtega wakati akihojiwa na Mwanahabari wa www.nukta.co.tz.

Msichana Queen Mtega aliyejikita kutumia teknolojia kuwainua mafundi stadi kimaisha. Picha|Mwananchi.

Wakati Queen akiwaunganisha mafundi na wateja, mwenzake Rahma Bajun (29) ambaye ni  Mwanzilishi na Mkurugenzi wa kampuni ya ushonaji nguo ya MnM Clothing Line kwa kutumia vitenge yenye makao yake jijini Dar es Salaam amefungua duka la mtandaoni ili kuwafikia wateja wake katika ukanda wa Afrika Mashariki. 

“I ‘think’ (nafikiri) ni njia nyingine ya kuongeza thamani ya biashara, kwa kuwa watanzania na ambao sio watanzania wengi nje ya Tanzania wangependa kuona na kununua nguo au bidhaa zetu. Kwa hiyo kuweka mtandaoni  bidhaa hizo kumetufanya tuweze kuwafikia wale ambao watashindwa kuja dukani kwetu kununua basi wataona mtandaoni na kuchagua wanachokitaka,” amesema Rahma.

Kutokana na bidii na kuamini anachokifanya, Rahma alitajwa katika Jarida la Forbes mwaka 2018 kuwa miongoni mwa vijana wajasiriamali 30 wa Afrika ambao biashara zao zinakuwa kwa kasi (30 Most Promising Young Entrepreneurs in Africa 2018) na jarida la Forbes la Marekani. 

Queen na Rahma wanatoa changamoto kwa wasichana waliopo shuleni kuongeza bidii ya kusoma masomo ya sayansi ili kufaidika na fursa za tehama zilizopo mbele yao.

Enable Notifications OK No thanks