Agenda ya amani, usalama vyatawala mkutano wa SADC Dar
- Nchi wanachama zimetakiwa kushirikiana katika kutunza na kuendeleza amani na usalama ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuwaletea wananchi maendeleo.
- Rais Magufuli awa Mwenyekiti mpya wa SADC.
- Kiswahili nacho kimeidhinishwa kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya SADC.
- Jumiya za kimataifa zawakumbusha wanachama wa SADC kutekeleza mikataba ya kimataifa.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana katika kutunza na kuendeleza amani na usalama ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, tangu mwaka 2010, uchumi wa nchi za SADC haujawahi kukua kwa zaidi ya asilimia tano huku pato halisi la ndani la jumuiya hiyo limekua likishuka kila mwaka.
Rais Magufuli aliyekua akizungumza leo (Agosti 17, 2019) baada ya kukabidhiwa kuwa Mwenyekiti mpya wa SADC katika mkutano wa wakuu wa nchi wa 39 uliofanyika jijini Dar es Salaam, amesema bado baadhi ya nchi za SADC zinakabiliwa na machafuko ya kisiasa na mapigano ya ndani.
Amesema changamoto hiyo ya ukosefu wa amani na usalama imekuwa ikikwamishwa shughuli za utengamano wa biashara na hivyo kuathiri dhana nzima ya ukuaji wa uchumi wa viwanda wa jumuiya hiyo yenye nchi 16.
“Licha ya mafanikio makubwa ya jumuiya yetu, bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Katika baadhi ya nchi zetu bado kuna mapigano ya ndani,” amesema Rais Magufuli ambaye amepokea nafasi ya uenyekiti kutoka kwa Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob.
Amezitaja changamoto zingine ambazo zinatakiwa zishughulikiwe ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ukame, ugaidi wa kimataifa, uhalifu wa kimtandao na magonjwa.
Soma zaidi:
- Tanzania inavyofaidika na mahitaji ya kiuchumi ya SADC
- Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC
- Maagizo matano ya Magufuli kukuza uchumi wa viwanda nchi za SADC
Aidha, Rais amesema ili kuzitokomeza changamoto hizo, nchi wanachama hazina budi kushirikiana kwa karibu kuweka kipaumbele katika kujenga amani na usalama kwa wananchi wa SADC ili kuhakikisha mabadiliko ya kweli ya uchumi yanapatikana.
Katika hatua nyingine, amewashukuru wakuu wa nchi kwa kumuamini na kumpa jukumu la kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Amesema nafasi hiyo ni heshima na fahari kubwa kwa Tanzania na watu wake huku akibainisha kuwa jukumu hilo ni kubwa lakini yuko tayari kuitumikia SADC ili mipango iliyowekwa itekelezwe kwa wakati.
“Kuwa mwenyekiti wa SADC ni heshima siyo tu kwangu bali kwa Tanzania na watu wake. Najua hiyo siyo kazi ndogo imekuja na matarajio mengi lakini nimekubali majukumu haya, ninaamini kwa ushirikiano wenu wakuu wa nchi nitaweza kutimiza matarajio ya jumuiya yetu,” amesema Rais Magufuli.
Mkutano wa wakuu wa nchi wa 39 uliofanyika jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.
Mkutano huo wa SADC ambao unafanyika kwa siku mbili, pia umeridhia na kukipitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya mawasiliano ya shughuli za SADC kikiungana na Kiengereza, Kireno na Kifaransa.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dk Geingob amesema anampongeza Rais Magufuli kuwa mwenyekiti mpya na ameahidi kumpa ushirikiano mzuri ili kufanikisha matarajio ya SADC hasa katika kuimarisha uhusiano wa biashara na kukuza uchumi wa nchi wa jumuiya hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, Dk Vera Songwe amezitaka nchi za SADC kuhakikisha zinashirikiana na kuboresha mazingira ya kufanya biashara huku zikitekeleza mikataba ya kimataifa ya maendeleo ikiwemo Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya 2030.
Pia amezitaka kuboresha mazingira ya utoaji elimu ili kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma katika matumizi ya rasilimali za nchi.
Latest