Nyambizi ya Titan ilivyogeuza safari ya utalii kuwa msiba
- Watu watano wapoteza maisha akiweno bilionea Hamish Harding.
- Mlipuko watajwa kama sababu ya nyambizi hiyo kupoteza mawasiliano.
Dar es Salaam. Walikuwa na matumaini kuwa wangefanya moja ya safari adimu za kitalii duniani. Kwa kutumia nyambizi ndogo tu wangesafiri mpaka kilomita nne chini ya bahari na kushuhudia mabaki ya meli kubwa ya Titanic iliyozama miaka zaidi ya 110 iliyopita.
Hata hivyo, safari yao ya kitalii ya watu watano akiwemo bilionea wa Uingereza Hamish Harding waliokwenda kufanya utalii katika sakafu za bahari ya Atlantic imegeuka kuwa msiba baada ya chombo chao kulipuka.
Hadi sasa hakuna anayefahamu bayana iwapo walifanikiwa kushuhudia mabaki ya Titanic ama la kutokana na kupoteza mawasiliano na meli ya kuongozea chombo hicho saa moja na dakika 45 tangu kuanza safari yake iliyotarajiwa kuwa ya masaa mawili kufika mahali ilipo meli ya Titanic.
Chombo hicho kinachomilikuwa na kampuni ya Oceangate ya Marekani kiliripotiwa kupotea Jumapili ya Juni 18, 2023 kiasi cha kuushtua ulimwengu na kuacha maswali lukuki juu ya dhima ya safari yao, usalama wa nyambizi hiyo na mustakabali wa maisha yao baada ya kutoweka.
Jitihada kubwa zilifanyika kukitafuta chombo hicho pamoja na watu waliokuwemo ndani yake lakini matumaini ya kuwapata wakiwa hai yalizima rasmi jana Juni 22, 2023 baada ya wataalamu kuona vipande vitano vya nyambizi hiyo.
John Maugure, Mkuu wa Kamandi ya Maji ya Marekani aliwaambia wanahabari kuwa nyambizi hiyo iliripuka baada ya roboti kubaini sehemu ya mkia (tail cone), stendi (landing frame) pamoja na sehemu ya mbele ya nyambizi hiyo (porthole window).
“Kwa niaba ya kamandi ya wanamaji ya Marekani na vikosi vya utafutaji tunatoa pole kwa wanafamilia, tunaendelea kukusanya taarifa zaidi ili kubaini muda halisi wa ajali hii kubwa,” alisema Maugure.
Kwa mujibu wa Maugure, vipande vya nyambizi hiyo vilionekana futi 1,600 kutoka yalipo mabaki ya meli ya Titanic na kilomita nne Kaskazini mwa sakafu za bahari ya Atlantic.
Titan ni nini?
Hii ni nyambizi ndogo iliyotengenezwa na Kampuni ya kutengeneza nyambizi ya nchini Marekani ya OceanGates ambayo huzitengeneza kwa ajili ya shughuli za utafiti, kijeshi, pamoja na biashara.
Kwa mujibu wa Ocean Gates nyambizi ya Titan ilikuwa na urefu wa mita 6.7 na uzito wa tani 10.4 ikiwa na uwezo wa kuzama mita 4,000 sawa na kilomita nne hini ya bahari ikiwa imeizidi nyambizi ya Marekani ya USS Dolphin ambayo ina uwezo wa kwenda mita 900 tu chini ya bahari.
Nyambizi hii ilianza majaribio mwaka 2018 na ikafanya safari yake ya kwanza rasmi mwaka 2021 ambapo kwa mwaka 2022 pekee tayari imeshafanya safari 10 za chini ya bahari na kwa mwaka 2023 ilipanga kufanya safari 18.
Wakati manowari au nyambizi kubwa zikiwa na uwezo wa kukaa majini kwa miezi kadhaa nyambizi ya Titan ilikuwa na uwezo wa kukaa majini kwa saa 10 mpaka 11 tu kwa kila safari ambapo huwa na oksijeni inayoweza kutosheleza kwa masaa 96 ikiwa kuna dharula.
Nauli safari moja ni Sh600 milioni
Kwa kuwa nyambizi hii haikuwa na vifaa maalumu vya kuiwezesha kutoa mawasiliano ikiwa chini ya maji (GPS) huwasiliana moja kwa moja na meli ya kuongozea ambayo hutuma ujumbe mfupi kila baada ya dakika 15.
Hata hivyo, ili upate siti katika nyambizi ya Titan utalazimika kulipia Dola za Marekani 250,000 sawa na Sh601 milioni za Tanzania kwa safari moja.

Sehemu za nyambizi ya Titan zilizoonekana. PichalBBC
Waliokuwepo ndani yake
Kwa mujibu wa Oceangates Titan ilikuwa na watu watano akiwemo Mmiliki na Mwanzilishi wa kampuni hiyo Stocton Rush ambaye ndiye alikuwa muongozaji wa chombo hicho.
Wengine ni Bilionea wa Uingereza Hamish Harding mwenye umri wa miaka 58, mfanyabiashara Shazhada Dawood aliyekuwa na mwanae Suleiman pamoja na mtafiti wa masuala ya chini ya maji Paul Henri Nargeolet.
Hii ndio ajali ya majini iliyofuatiliwa zaidi duniani kutokana na uzito iliopewa na vyombo vya habari pamoja na vikosi vya utafutaji na uokozi kutoka mataifa ya Marekani pamoja na Kanada.
Hata hivyo, kumekuwepo na malalamiko kadhaa kuwa wamiliki wa nyambizi hiyo hawakuchukua hatua za kutosha za kuhakikisha usalama wa chombo hicho pamoja na abiria wake kwa kuwa baadhi ya mapungufu yalishawahi kuripotiwa awali.
Kamapuni NBC ya Marekani imemnukuu aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya OceanGates David Lochridge kuwa chombo hicho hakikuwa kimefanyiwa majaribio ya kutosha kuzama umbali wa mita 4,000 mahali yalipo mabaki ya meli ya Titanic.
Lochridge ambaye alifukuzwa kazi miaka mitano iliyopita aliishtaki kampuni hiyo kwa kumfuta kazi bila utaratibu baada ya kutoa onyo kuwa nyambizi hiyo bado haina uwezo wa kuzama kina hicho cha maji.