Safari ya Rioba: Kutoka mwandishi wa habari hadi Msemaji Mkuu wa Serikali
- Alikulia katika familia ya kawaida ambako wali na sukari vilikuwa adimu.
- Aliiongoza TBC kwa miaka 10, sasa anarejea katika uongozi wa mawasiliano akiwa Ikulu.
Dar es Salaam. Katika maisha ya baadhi ya watu, safari ya mafanikio huanza katika mazingira ambayo hayatoi uhakika wa kufika mbali.Â
Wakati mwingine, vitu vinavyoonekana vya kawaida kwa wengine huwa anasa kwa familia nyingine. Hata hivyo, mazingira ya utoto hayalazimishi mwisho wa safari ya mtu.
Hiyo ni sehemu ya simulizi ya Dk Ayub Rioba Chacha, ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Kabla ya kupewa jukumu hilo na Rais Samia Suluhu Hassan, jana Novemba 25, 2026, Rioba alikuwa amepitia safari ndefu katika tasnia ya habari, kuanzia kuwa mwandishi wa magazeti hadi kuongoza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Lakini nyuma ya vyeo hivyo kuna simulizi la mtu ambaye mwenyewe amewahi kueleza kuwa hakutoka katika mazingira ya maisha ya kitajiri.
Alikotoka
Machi 2026 baada ya kumaliza uongozi wake TBC, Rioba alieleza kuwa alikulia katika familia ya kawaida ya mwalimu wa shule ya msingi, ambako baadhi ya mahitaji kama wali na sukari yalikuwa adimu na mara nyingi yalipatikana wakati wa sikukuu.
Alisema alijijengea njia kupitia elimu na juhudi zake zlizomfikisha katika shule za Mara na Ilboru, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
Rioba alisoma Shule ya Sekondari Mara mwaka 1986, kabla ya kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Ilboru, ambako alihudhuria kati ya mwaka 1987 na 1989.
Baada ya hapo, mwaka 1990 alishiriki mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hatua iliyotangulia safari yake ya elimu ya juu.
Mwaka 1993, alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere kilichopo Kampala, Uganda, ambako alisomea shahada ya kwanza ya Mawasiliano ya Umma akijikita katika uandishi wa habari za utangazaji.
Mwaka 1997 alihitimu shahada ya uzamili ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Wales, Cardiff, nchini Uingereza.
Safari yake ya elimu iliendelea nchini Finland katika Chuo Kikuu cha Tampere, ambako mwaka 2009 alipata shahada ya juu ya uzamili ya Mawasiliano ya Umma.
Oktoba 29, 2012, alitunukiwa shahada ya uzamivu katika Mawasiliano ya Umma na Chuo Kikuu cha Tampere, baada ya kutetea utafiti wake kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya habari katika demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania.
Aliingia kwenye uandishi wa habari mwaka 1993
Rioba alianza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1993 na mwaka uliofuata alifanya kazi katika Kampuni ya Magazeti ya Tanzania (TSN).Â
Baadaye alijiunga na Shule ya Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ), ambako alipanda hadi kuwa Mkurugenzi wa Masomo mwaka 1998.Â
Mwaka 2003 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama mhadhiri na baadaye kuwa Naibu Mkuu wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma.Â
Mbali na kufundisha, alijihusisha na utafiti, uandishi wa makala na uchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii.
Alikuwa mtangazaji wa kipindi maarufu ITV
Kabla ya kuingia katika uongozi wa TBC, Rioba alikuwa pia na uzoefu wa moja kwa moja katika utangazaji wa televisheni.
Kati ya mwaka 2003 na 2007, aliendesha kipindi cha kila wiki cha Sema Usikike kupitia kituo cha televisheni cha Runinga Huru (ITV).Â
Pia aliandika makala za uchambuzi na kutoa maoni kuhusu masuala ya kisiasa na kijamii.
Katika tasnia ya habari, Rioba anafahamika pia kwa utafiti wake wa uzamivu wa mwaka 2012 kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya habari katika demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania.Â
Utafiti huo ulijikita katika nafasi ya vyombo vya habari kujisimamia na kuwajibika, ukiangazia Baraza la Habari Tanzania (MCT).Â
Akiwa mwanataaluma, alijikita katika kuchunguza uwajibikaji wa vyombo vya habari na nafasi yake katika demokrasia ya vyama vingi.
Sasa, akiwa katika nafasi hiyo mpya anakuwa sehemu ya upande mwingine wa mawasiliano, akitarajiwa kusimamia uwasilishaji wa taarifa za Serikali kwa umma.
Mabadiliko hayo yanaweka mbele yake jukumu la kujenga mawasiliano yanayoweza kujibu mahitaji ya wananchi ya kupata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi.
Mwaka 2016 akabidhiwa TBC
Machi 19, 2016, Rais wa wakati huo, Dk John Pombe Magufuli, alimteua Rioba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Alichukua nafasi ya Clement Mshana aliyestaafu.
Katika nafasi hiyo, alisimamia shughuli za redio na televisheni, uzalishaji wa maudhui, maendeleo ya teknolojia na ushirikiano wa TBC na taasisi nyingine za utangazaji.
Katika uongozi wake, TBC ilitekeleza miradi ya kuboresha studio, mitambo na vifaa vya uzalishaji wa maudhui, ikiwemo ujenzi wa studio za TBC2 kwa ushirikiano na Serikali ya Korea Kusini.
Pia, mwaka 2021 TBC iliingia makubaliano ya ushirikiano na Voice of Nigeria yaliyolenga kubadilishana maudhui na kuimarisha utangazaji wa Afrika, ushirikiano ulioendelezwa mwaka 2024.
Hata hivyo, uongozi wake haukukosa mijadala na ukosoaji kuhusu utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo.
Machi 2026, Rioba alimaliza kipindi chake cha uongozi TBC baada ya kuhudumu kwa takribani miaka 10.
Baada ya kuondoka kwake, Rais Samia alimteua Asha Dachi Mbaruk kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa TBC Julai 14, 2026.
Lakini kuondoka kwake TBC hakukumaanisha kumalizika kwa safari yake katika sekta ya mawasiliano.
Alikataa fursa za kazi nje ya nchi
Katika ujumbe wake wa Machi 2026, Rioba alisema alipata fursa za kufundisha katika vyuo vikuu vya nchini Kanada na Namibia mwaka 2012, lakini akaamua kuendelea kuitumikia Tanzania.
Alisisitiza umuhimu wa juhudi, nidhamu, maono na ubunifu katika kufikia mafanikio.Â
Kwa sasa Rioba atakuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na umma katika kueleza sera, maamuzi, mipango na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.
Ni nafasi inayokuja katika kipindi ambacho mitandao ya kijamii imebadili kasi ya upashanaji habari, huku matarajio ya wananchi kuhusu upatikanaji wa taarifa na uwazi yakizidi kukua.
Uzoefu wake katika uandishi, ufundishaji, utafiti na utangazaji sasa utakutana na changamoto mpya ya kusimamia mawasiliano ya Serikali katika mazingira hayo.