Rais Samia avunja wizara mbili, afanya uteuzi, uhamisho wa viongozi
- Ameigawa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa wizara mbili.
- Wizara ya Mifugo na Uvuvi nayo yagawanywa, Mwinjuma ateuliwa kuwa Waziri wa Uvuvi.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko ya uongozi katika muundo wa Wizara mbili huku akiteua na kuhamisha viongozi mbalimbali ili kuimarisha utendaji wa Serikali.
Taarifa ya Bakari Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu iliyotolewa Novemba 25, 2026 inaeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imegawanywa na kuunda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
“Halikadhalika, amegawanya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa Wizara mbili ambazo ni Wizara ya Mifugo na Wizara ya Uvuvi,”imesema taarifa ya Machumu iliyorejea taarifa ya Katibu Mkuu Moses Kusiluka.
Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akitokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Nafasi ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni miongoni mwa wizara iliyovunjwa imepewa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Wakati huo huo, Balozi Dk Bashiru Ally Kakurwa ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo, akitokea Wizara ya Mifugo na Uvuvi, huku Hamis Mohamed Mwinjuma akiteuliwa kuwa Waziri wa Uvuvi.
Kabla ya uteuzi huo Mwinjuma alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katika nafasi nyingine za uwaziri, David Ernest Silinde ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kabla ya uteuzi huo Silinde alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, huku Beng’i Mazana Issa akiteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Naibu Mawaziri wapya
Mbali na mabadiliko ya Mawaziri, Rais Samia amefanya uteuzi wa Naibu Mawaziri watano katika Wizara mbalimbali.
Dk Ngwaru Jumanne Maghembe ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambapo awali alikuwa akihudumu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Pia, James Kinyasi Millya ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akitokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wengine ni Ng’wasi Damas Kamani aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo, akitokea Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na Subira Khamis Mgalu aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uvuvi.
Aidha, Cecilia Daniel Paresso ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Pangapangua makatibu wakuu
Katika hatua nyingine, Rais Samia amefanya uteuzi na uhamisho wa Makatibu Wakuu saba katika Wizara mbalimbali.
Agnes Meena ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, akitokea Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Profesa Mohammed Ali Sheikh ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia masuala ya uvuvi.
Eliakim Chacha Maswi amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Naye Gerson Msigwa amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Kwa upande mwingine, Abdallah Hassan Mitawi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akitokea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.
Katika mabadiliko ya uongozi wa Wizara zinazohusika na diplomasia, Balozi Dk Samwel William Shelukindo amepangiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akitokea nafasi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Charles Ngeleja Kadonya amepangiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Awali, alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Naibu makatibu wakuu watano wateuliwa
Rais Samia pia amefanya mabadiliko ya Naibu Makatibu Wakuu watano katika Wizara mbalimbali.
Balozi Said Shaib Mussa amepangiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akitokea nafasi hiyo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Dk Fabian Magawa Madele amepangiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, akitokea nafasi hiyo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambako alikuwa akishughulikia masuala ya mifugo.
Wengine ni Dadi Horace Kolimba aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Aidha, Elijah Greenton Mwandumbya amehamishwa kutoka Wizara ya Fedha kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.
Dk Amos James Ibrahim ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayeshughulikia masuala ya usimamizi wa uchumi. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo cha Kodi.
Rioba kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali
Katika nafasi nyingine, Rais Samia amemteua Dk Ayub Rioba Chacha kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Kabla ya uteuzi wake Dk Rioba alikuwa amemaliza kipindi chake cha uongozi TBC baada ya kuhudumu kwa takribani miaka 10.
Katika nyanja za kidiplomasia, Balozi Meja Jenerali Wilbert Augustin Ibuge amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil.
Kabla ya kupangiwa kituo hicho cha kazi, Ibuge alikuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).
Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Mhandisi Gilbert Godfried Mwoga kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura).
Kabla ya uteuzi huo, Mwoga alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Miundombinu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mwoga anachukua nafasi ya Mhandisi Victor Hudson Seff ambaye amemaliza muda wake.
Ndunguru kuwa Mwenyekiti wa Baraza la MUST
Katika uteuzi mwingine, Rais Samia amemteua Katibu Mkuu Mstaafu, Adolf Hyasinth Ndunguru, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Ndunguru anachukua nafasi ya Zakhia Hamdani Meghji ambaye amemaliza muda wake.
Hata hivyo, kulingana na taarifa hii, uapisho wa viongozi hao utafanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.