Maambukizi ya VVU Tanzania yashuka, vijana hatarini

Dar es Salaam. Kasi ya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) nchini Tanzania imepungua kwa asilimia 66.1 ndani ya miaka 15, suala linalotoa muelekeo chanya wa afya ya jamii nchini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi maambukizi hayo yameshuka kutoka watu 98,754 mwaka 2010 hadi kufikia 33,511 mwaka 2025.
Hata wakati idadi hiyo ikipungua Kabudi aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Novemba 19, 2026 amesema vijana wako hatarini zaidi kulinganisha na makundi mengine.
Kabudi amebainisha kuwa kundi la vijana linachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya ya VVU nchini, huku wasichana wakiongoza ndani ya kundi hilo kwa kuchangia asilimia 77.7.